Friday, July 26, 2013

MAJINA YA WALIOKIDHI VIGEZO, TANGAZO LA KAZI LA TAREHE 26 MACHI, 2013

Waombaji waliokuwa wametuma maombi ya fursa za ajira kwa ajili ya tangazo la kazi lililokuwa limetolewa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa niaba ya Waajiri mbalimbali nchini mnamo tarehe 26 Machi, 2013 katika lugha ya Kiswahili ambapo mwisho wa kutuma maombi ilikuwa tarehe 9 Aprili, 2013 wametakiwa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira  ili kuweza kuona majina yao kwa wale ambao watakuwa wamekidhi vigezo ili waweze kujiandaa kwa usaili.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Xavier Daudi amesema hayo leo alipokuwa akiongea na baadhi ya wadau waliomtembelea ofisini kwake wakitaka ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu mchakato wa Ajira Serikalini, pia wakitaka kujua ni lini majina ya waliokidhi vigezo kwa tangazo hilo yatatolewa.
“Najua tumeshatoa matangazo kadhaa hivi sasa yanayohusu fursa za ajira zilizopo ila ningependa nitolee ufafanuzi wa tangazo la tarehe 26 Machi, 2013 kuwa Waombaji wote waliokuwa wamewasilisha maombi kwa tangazo hilo watembelee tovuti ya Sekretarieti ya Ajira maana majina yameshatolewa kwa wale waliokidhi vigezo vya msingi. Ila kwa wale ambao hawataona majina yao wajue hawakuwa na sifa kulingana na vigezo vilivyokuwa vikihitajika katika nafasi hizo,” alisema Daudi.
Aidha, amewataka waombaji watakaoona majina yao kuendelea kutembelea tovuti  pamoja “facebook-page” ya Sekretarieti ya Ajira mara kwa mara ili kupata ratiba, tarehe ya usaili na mahali watakapofanyia usaili husika kulingana na nafasi walizoomba.
Daudi ametoa Rai kwa waombaji wote waliochaguliwa kwa ajili ya kwenda kufanya usaili kujiandaa vyema ikiwa ni pamoja na kuzingatia vitu muhimu wanavyopaswa kwenda navyo kwenye usaili siku husika, ikiwemo vyeti halisi na halali vya kitaaluma, pamoja na kuzingatia muda utakaokuwa umeainishwa.
“Naomba niweke wazi kuwa ili msailiwa aweze kufanya vizuri katika usaili pamoja na vigezo vya kitaaluma alivyonavyo bado     anapaswa kujiandaa vyema na kujiamini anapojibu maswali wakati anapokuwa kwenye chumba cha usaili, kwa kuwa hivi sasa dunia imekuwa ya utandawazi na fursa za ajira ni chache na za ushindani zaidi, na wahitimu ni wengi na hawana ajira, hivyo ni vyema wale wanaoitwa kwenye usaili wawe wamejiandaa vya kutosha ili waweze kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata ajira husika” alisisitiza Katibu wa Sekretarieti ya Ajira.
Aliongeza kuwa ofisi yake itaendelea na utaratibu wa kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu uendeshaji wa mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma ikiwemo majina na ratiba za usaili mapema kila mara ili kuwawezesha wasailiwa kuwa na muda wa kutosha kujiandaa kabla ya kwenda kwenye usaili husika.
Mwisho amewataka Waombaji wa nafasi wazi za kazi kwa Matangazo ya kazi yaliyotolewa kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Ajira tarehe  16 Aprili, Mei 22, Juni 18, Juni 29 pamoja na la tarehe 11 Julai, 2013  wanafahamishwa kuwa mchakato wa kuchambua maombi yao bado unaendelea na watapewa taarifa ya kuitwa kwenye usaili kwa wale waliokidhi vigezo kwa kila tangazo mara baada ya taratibu zote kukamilika.

Imetolewa na  Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Ofisi ya Rais-Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
Kwa maelezo zaidi; wasiliana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Kwa barua pepe;  gcu@ajira.go.tzThis e-mail address is being protected from spambots, you need JavaScript enabled to view it au simu 255-687624975
Tembelea pia “Facebook-page ya Sekretarieti ya Ajira”
24 Julai, 2013

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...