|
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na maofisa waandamizi wa
Wizara ya pamoja na wajumbe wa Chama cha Makampuni ya Simu za mkononi
alipokutana nao kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam jana Julai 23,
2013. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete ameagiza Wizara za Serikali zinahusika na kodi na
mawasiliano pamoja na makampuni ya simu za mikononi nchini kukutana mara
moja kutafuta jinsi gani ya kumaliza mvutano wa kodi mpya ya kadi za
simu hizo za mikononi.
Rais kikwete ametoa maelekezo hayo jioni
ya jana, Jumanne, Julai 23, 2013 wakati alipokutana na viongozi wa
Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na
wawakilishi wa makampuni ya simu ya TTCL, Airtel, Vodacom, Tigo na
Zantel katika kikao cha pamoja kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
|
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akitambulishwa kwa wajumbe wa Chama cha Makampuni
ya Simu za mkononi na Bw. Manoj Kohli wa Airtel ambaye pia ni Mkurugenzi
wa Pamoja wa chama hicho alipokutana nao kwa mazungumzo Ikulu jijini
Dar es salaam jana Julai 23, 2013. |
Rais Kikwete amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo wa pamoja kati ya
Wizara hizo za Serikali na makampuni ya simu yawe ya kupendekeza jinsi
gani ya kuziba pengo la Sh. Bilioni 178 ambazo zitapotea katika Bajeti
iwapo kodi hiyo kwa kadi za kuongelea za simu za mikononi italazimika
kufutwa na Serikali kupitia marekebisho kwenye Muswada wa Fedha wa
Bajeti ya Mwaka 2013/2014.
Rais Kikwete amewaambia wawakilishi
wa pande hizo mbili kuwa huwezi tena kuifuta moja kwa moja kodi hiyo
bila kutafuta njia nyingine za kupata fedha za kujaza pengo hilo la Sh.
Bilioni 178 ambazo tayari Bunge limezipangia matumizi.
“Nawaombeni
kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja
tutafute namna gani tunaweza kujaza pengo hili la Sh. Bilioni 178 endapo
tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito na kuwa
pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu,” Rais Kikwete amewaambia
wawakilisho hao.
|
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Bi Beatrice Singano, mmoja wa
wajumbe wa Chama cha Makampuni ya Simu za mkononi alipokutana nao kwa
mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam jana Julai 23, 2013.PICHA NA IKULU. |
Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014,
Serikali imeweka kodi ya Sh. 1,000/= kwa mwezi kwa kila mtumiaji simu
kwa ajili ya kufanya mawasiliano kwa kutumia simu ya mkononi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
23 Julai, 2013
No comments:
Post a Comment