Thursday, January 31, 2013

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA MWANGOSI NA MAASKARI WENZAKE WAMCHEFUA HAKIMU.

Mtuhumiwa wa mauaji ya Mwangosi akiwa katika viwanja vya Mahakama

Askari waliomleta mahakamani mtuhumiwa askari  wa FFU mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (23)  wa mauwaji ya  aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten mkoani Iringa marehemu Daudi Mwangosi,   wamemtibua Hakimu aliyeagiza mtuhumiwa huyo kurudishwa tena kizimbani hapo kwa kudharau mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa mnyeti wetu kutoka mahakamani hapo,tukio  hilo lilitokea leo  majira ya saa 5.35 asubuhi mara baada ya mahakama hiyo kuombwa kutaja tarehe nyingine ya  kutajwa kesi hiyo. Askari  watatu, ambao majina yao hayakuweza kufahamika mara moja, walimshusha mtuhumiwa  kizimbani na kumkimbizia mahabusu kama njia ya kukwepa kupigwa picha na wanahabari waliokuwepo hapo .

Mahakama ikiwa  bado inaendelea na shughuli ya keshi hiyo kwa Hakimu Mkazi  wilaya ya Iringa, Dyness Lyimo kutaja tarehe ya kesi hiyo, mtuhumiwa alishuka kizimbani  huku akivaa kofia yake ya sweta (mzula) na miwani ya giza na kuanza  kushuka jukwaani. Hakimu alimtaka mtuhumiwa huyo kutovalia kofia hiyo kizimbani.

Wakati hakimu  huyo akijiandaa kusimama ili kuhitimisha shughuli za Kimahakama kwa siku  hiyo, ghafla alijikuta anabaki na Mwanasheria  wa Mahakama, Karani wake, Wanahabari, Askari mmoja na ndugu wawili wa mtuhumiwa, huku askari 3 wenye silaha  na mtuhumiwa huyo wakiwa tayari wameondoka ndani ya chumba cha mahakama hiyo.

Mbona hao askari wanamtoa mtuhumiwa  bila utaratibu wa mahakama hebu  mwanasheria waambie wamrudishe ndani mtuhumiwa ....huu si utaratibu mbona  wanafanya fujo mahakamani  hao.
Pamoja na jitihada za mwanasheria wa  serikali Adolf Maganda kuwaita  kwa  sauti,  askari hao  kuwataka  kumrudisha  ndani ya mahakama mtuhumiwa huyo  bali  walizidi kukimbia na mtuhumiwa kwenda naye mahabusu. 

Baada ya dakika kama 5 hivi, ndipo mwanasheria  huyo aliporejea na askari hao na mtuhumiwa ambaye hata  hivyo hakwenda kusimama  kizimbani na badala  yake alikwenda upande wa  kushoto wa mahakama ambako alikuwa amekaa mwanzoni kabla ya mahakama  kuanza na kuketi katika  kiti huku akiwa bado amevaa miwani na kofia  yake.

Kutokana na  tukio  hilo, Hakimu  huyo alilazimika  kuwahoji askari hao  watatu kwa vurugu  hizo  walizozifanya kwa kuwauliza swali moja  pekee , ikiwa wanaona walichofanya ni  sahihi, ambapo askari hao waliosema, “samahani mheshimiwa”.

Mwendesha mashtaka  wa Jamhuri, Adolf Maganda aliiomba mahakama kutaja tarehe nyingine ya kutajwa tena  kwa kesi hiyo ambayo awali ilikuwa imetajwa Januari 27, 2013 lakini mtuhumiwa alishindwa kufika Mahakamani kutokana na ugonjwa. Mahakama  hiyo  imeahirisha  kesi hiyo  hadi  Februari 14 mwaka huu.

Jinsi marehemu Mwangosi alivyokuwa akikabiliwa na maaskari kabla ya umauti kumkuta.
Mtuhumiwa  huyo anatuhumiwa  kumuua kwa makusudi kwa  bomu aliyekuwa  mwandishi  wa habari wa Chanel Ten  mkoa  wa Iringa  marehemu Mwangosi  septemba 2 Septemba mwaka jana  katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa  wakati  zilipozuka vurugu kati ya  Askari Polisi na wafuasi wa  CHADEMA.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...