Tuesday, April 2, 2013

RUFAA YA SERIKALI DHIDI YA ZOMBE KUANZA KUSIKIRIZWA APRILI 22.


Abdallah Zombwe akihamaki
RUFAA ya kupinga kuachiwa huru kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake, inatarajiwa kusikilizwa mfululizo kuanzia Aprili 22 na 23 mwaka huu.

Rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Jaji, Edward Rutakangwa, Jaji Mbarouk Mbarouk na Jaji Bernard Luanda.

Mbali na Zombe, wajibu rufani wengine ni polisi Christopher Bageni, Ahmed Makele, Jane Andrew, Koplo Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasab.

Serikali ilikata rufani hiyo kupinga hukumu iliyotolewa Agosti 17, mwaka 2008 na Jaji Salum Massati wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Jaji Massati katika hukumu hiyo aliwaachia huru Zombe na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini wa mkoani Morogoro na dereva teksi.

Zombe na wenzake walikuwa wakidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe na dereva teksi, Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam.

Katika hukumu hiyo, Jaji Massati alisema upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha mashitaka bila ya kuacha shaka yoyote na hivyo mahakama iliwaona washitakiwa hawakuwa na hatia na kuwaachia huru.

Alisema mahakama hiyo ilibaini wauaji halisi walikuwa hawajafikishwa mahakamani na hivyo mashitaka dhidi ya washitakwa yasingeweza kutengenezeka. Aliuagiza upande wa Jamhuri iwasake na kuwafikisha mahakamani wahusika.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali (DPP) aliamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani, iliyosajiliwa na kupewa namba 254/2009 kupinga hukumu hiyo akidai hakuridhika nayo.
Katika rufani hiyo, DPP aliwasilisha hoja 11 za sheria kupinga hukumu hiyo akidai kwamba kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washitakiwa wote walikuwa na hatia.

Miongoni mwa sababu nyingine, DPP anadai kulikuwa na upungufu katika hukumu hiyo kwa kila mshtakiwa.

Anadai Jaji Massati alipotoka na kushindwa kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu mashitaka ya jinai na kwamba alijichanganya katika hukumu hiyo.

DPP anadai kushangazwa na Jaji Massati kushindwa kuwatia hatia washitakiwa wote ikizingatiwa ulikuwapo ushahidi wa dhahiri na wa mazingira wa kutosha kuwatia hatiani.

Habari hii ni kwa hisani ya Mtanzania.

MAAFA, KIFUSI CHAUWA, 20 WAHOFIWA KUFA HUKO ARUSHA

Wakazi wa Arusha wakiwa eneo ambapo watu zaidi ya 20 wanahofiwa kufukiwa.
Siku tatu baada ya ghorofa kuanguka na kuua watu 36 jijini Dar es Salaam, maafa mengine yametokea jana mkoani Arusha ambako watu wapatao 20 wanahofiwa kufa baada ya kufunikwa na kifusi cha `moramu’ wakati wakifanya shughuli za uchimbaji eneo la Moshono, Arusha.

Maiti za watu 14 ndiyo zilikuwa zimeopoelewa hadi jana jioni wakati watu wawili tu ndiyo walikuwa wametoka wakiwa hai na kukimbizwa katika Hospitali ya Mt Meru kwa ajili ya matibabu kutokana na kuvunjika miguu.

Waliotolewa wakiwa hai walitambuliwa kuwa ni Matei Nenano na Lushooki Laizer wote wakazi wa jijini Arusha. Mwananchi lilishuhudia vikosi vya uokoaji kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi pamoja na wananchi wakitoa msaada wa kufukua kifusi hicho kwa ajili ya kutoa watu waliofunikwa.

Maiti zilizoopolewa ni za mmiliki wa magari ya kubeba kifusi hicho, Julius Peter, Alex Mariaki, Gerald Lutakata, Hassan Hamis, Sauli Raphael, Bariki Revelian na Kababuu Ruafela.
Wengine ni Mwenda Kiboliboli, Japhet Jivaline, Benard Masai, Gerald Jacob, Fredy Losileani, Julius Palangyo na mtu ambaye alijulikana kwa jina moja la Christopher.

Watu walioshuhudia tukio na taarifa hizo kuthibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Hemed Kilonge walisema lilitokea jana saa 5.00 asubuhi wakati shughuli za uchimbaji zikiendelea.

Kamanda Kilonge alisema wakati wachimbaji hao wakiwa ndani ya shimo wakiendelea na kuchimba ‘moramu’, ghafla gema liliporomoka na kuwafunika.

Mashuhuda walisema wachimbaji hao walikuwa wakifanya shughuli zao huku mvua kubwa ikinyesha na kwamba kuna uwezekano hiyo ni sababu ya kuanguka kwa kifusi hicho.
Mvua ilikuwa ikiendelea hata wakati wa uokoaji, hali iliyofanya kazi hiyo kuwa ngumu.

“Inasadikiwa kuwa zaidi ya wachimbaji 20 pamoja na magari mawili kwa ajili ya kubeba mzigo huo yalikuwapo ndani ya shimo hilo ambayo nayo yalifunikwa na kifusi hicho,”alisimulia Kamanda Kilonge.

Uhaba wa mafuta
Mwananchi lilishuhudia magari ya uokoaji kutoka jijini Arusha yakiwa yameishiwa mafuta na kusababisha uokoaji kuzorota.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amelazimika kusitisha safari yake mkoani Tanga baada ya kupata taarifa ya tukio hilo na baadaye alitangaza kwamba Serikali imeamua kufunga machimbo yote ya `moramu’ hadi pale itakapotoa tamko lingine.

Akizungumza eneo la tukio, Mulongo alisema tukio hilo ni la kusikitisha kwa kuwa vijana waliokufa ni wengi.
Kwa upande wake mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliitaka Serikali kuweka utaratibu wa kukabiliana na matukio ya aina hiyo ikiwa ni pamoja na kuweka viashiria vya usalama maeneo ya machimbo.
Godbles lema Mbunge wa Arusha Mjini
Kiongozi mwingine aliyefika katika eneo hilo ni Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo ambaye alisema kwa sasa ni muda mwafaka wa kufunga mgodi huo kwa kuwa mwaka 1997 tukio kama hilo lilitokea na kuua watu saba kwa kufukiwa na kifusi.
Joshua Nasari Mbunge wa Arumeru Mashariki.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari aliilalamikia Serikali kwa kutokuwa na ofisi ndogo za vitengo vya maafa mikoani na kudai kuwa endapo ofisi hizo zingekuwapo uokoaji ungekuwa rahisi.

Wananchi wafurika
Wananchi kutoka viunga mbalimbali vya Jiji la Arusha walijitokeza kwa wingi kushuhudia kazi za uokoaji zikiendelea bila kujali mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.
Wananchi hao walionekana kushirikiana katika uokoaji ambapo ilipofika saa 10.00 jioni, wanajeshi zaidi kutoka Kambi ya 977KJ na Sopa Monduli walifika kuongeza nguvu.
 Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya wananchi waliitupia lawama Serikali kwa kushindwa kuweka usimamizi mzuri wa machimbo hayo licha ya tukio kama hilo kuwahi kutokea siku za nyuma.

“Hii ni mara ya pili kwa machimbo haya kusababisha vifo. Mwaka 1997 tulishuhudia machimbo haya yakiporomoka na watu kufunikwa ndani lakini hakuna hatua iliyochukuliwa mpaka leo tunashuhudia haya tena. Ni lazima Serikali iwajibike kutokana na mauaji haya,”alisema mzee aliyejitambulisha kwa jina la Christoper Laizer.

Habari hii ni kwa hisani ya Mwananchi

Thursday, March 28, 2013

Breaking News: MBUNGE WA CHAMBANI ALIYEANGUKA JANA AFARIKI DUNIA.


Mbunge wa Chambani-Pemba Mh. Salim Hemed Khamis aliyeanguka ghafla jana katika kikao cha kamati ya Bunge Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa amefariki dunia.
Kwa taarifa zilizotufikia hivi punde, nikwamba mbunge huyo amefariki mchana huu na mpango wa kusafirisha mwili wa marehemu kuelekea visiwani Zanzibar zinafanyika.
Taarifa zaidi zitawajia kadiri tutakavyokuwa tunazidi kuzipata.

MENEJA MASOKO WA KAMPUNI YA VINGAMUZI VYA STAR TIMES APANDISHWA KIZIMBANI KWA UDANGANYIFU


Meneja Masoko wa Kampuni ya ving’amuzi ya Startimes, David Kisaka (37) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, kujibu shtaka la kujipatia vitu kwa njia ya udanganyifu.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nassoro Katuga alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 5, mwaka huu eneo la Akiba, Wilaya ya Ilala.
Katuga alidai siku hiyo ya tukio katika eneo hilo, mshtakiwa kwa njia ya udanganyifu alijipatia ving’amuzi 110 na Antena 30 za StarTimes vikiwa na thamani ya Sh8.4 milioni mali ya Jonathan Mkanaka.
Antena ya nje inayotumika na vingamuzi vya Startimes
 Mshtakiwa alikana shtaka na hakimu Joyce Minde aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 22, mwaka huu itakapotajwa tena. Mshtakiwa yupo nje ya dhamana baada ya kupata wadhamini wawili wa kuamina ambao walisaini bondi ya Sh6 milioni.

Habari  hii ni kwa hisani ya Mwananchi.

NAIBU WAZIRI ATETEA VITI MAALUM VISIONDOLEWE

Naibu Waziri wa  Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, ametilia shaka pendekezo la kuondolewa kwa nafasi ya Viti Maalumu Katiba Mpya.
Alisema kitendo hicho kinaweza kukwamisha malengo ya milenia  na yale ya itifaki ya jinsia na maendeleo katika  nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) ya kuwa na uwakilishi wa asilimia 50  ya wanawake  bungeni.
Naibu  waziri huyo alisema kama  nafasi hizo zitatolewa, kuna ulazima wa katiba kutamka wazi namna ambavyo itahakisha kuwa wanawake wanapata nafasi za uongozi katika ngazi zote za serikali. Alitolea mfano katiba ya Kenya ambayo inaeleza bayana namna viongozi wanawake wanavyopatikana katika nchi hiyo.
Alisema hayo katika kongamano la waandishi  wa habari na mashirika yasiyokuwa  ya kiserikali yanayojihusisha na  masuala ya kijinsia, jijini Dar es Salaam jana.
Kongamano hilo  lilikuwa na lengo la kutathimi itifaki ya  malengo 28 ya kijinsia ya Sadc ifikapo 2015.
Naibu waziri huyo aliwataka waandishi wa habari na wanaharakati, kuhakikisha kuwa masuala ya ujinsia yanafafanuliwa kwa kiasi kikubwa katika rasimu ya Katiba Mpya inayotarajiwa kuwasilishwa juni mwaka huu na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Pia aliwataka waandishi kutumia  wanawake kama vyanzo vya  habari  kwa sababu takwimu zinaonyesha  ni asilimia 21 tu wanawake ndio wanatoa sauti katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Habari hii ni kwa hisani ya Mwananchi.

TETE BEACH PUB KUWAKA MOTO PASAKA HII NA Y2K SOUND

Sikukuu ya Pasaka Y2K SOUND MOROGORO itawasha moto katika viwanja vya Tete Beach Pub iliyoko Kihonda- Mazimbu road.

MaDj waliobobea wa Y2K Sound akiwemo Dj.R,Dj.Shebi zee, Dj.Parein watakuwa wanabengisha na kuwaburudisha wakazi wa Morogoro.

Katika burudani hiyo, mtu atahitajika kununua kinywaji tuu na kuendelea kuburudika.

MANJI NA MWALUSAKO WAJISALIMISHA MAHAKAMA KUU

Mwenyekiti wa Yanga Yusuph Manji akiongea na waandishi wa habari
 MWENYEKITI wa Yanga, Yusuph Manji na Katibu wake, Laurence Mwalusako, wamejisalimisha Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi ili wajieleze kwa nini wasifungwe jela kwa kukaidi amri ya mahakama.

Viongozi hao walijisalimisha jana, mbele ya Msajili wa mahakama hiyo, Mohammed Gwaye, baada ya kutakiwa kufanya hivyo kwa sababu walishindwa kuwasilisha mahakamani hapo dhamana ya Sh 106,300,000.

Gwaye aliwaamuru kuwasilisha dhamana hiyo wakati wakisubiri hatima ya marejeo ya uamuzi uliotolewa na Kamisheni ya Usuluhishi wa Migogoro, iliyowataka Yanga kuwalipa wachezaji waliowafukuza jumla ya Sh 106,300,000 kwa kuvunja mikataba yao kinyume cha sheria.

Wachezaji hao ni Steven Malashi na Wisdom Ndlovu kutoka Malawi, waliochukuliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili wakati wakijiandaa kwa kipindi cha Ligi Kuu.

Malashi na Ndlovu walikimbilia Kamisheni ya Usuluhishi, mgogoro wao ulisikilizwa huku Yanga wakigoma, ambapo Mahakama iliamuru Ndlovu alipwe Sh milioni 57, zikiwa ni mishahara ya miaka miwili, Sh 1,800,000 gharama za usafiri kutoka Malawi, Sh milioni 20 fidia, wakati Malashi aliamuliwa kulipwa Sh milioni 18 za mshahara wa miaka miwili, Sh milioni 10 fidia na Sh 500,000 fedha zake za usajili zilizobaki kwa mwaka 2009 na 2010.

Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, Mohammed Gwaye, alitoa uamuzi wa maombi hayo Februari 4 mwaka huu, akiamuru Yanga kuwasilisha fedha hizo mahakamani wakati wakisubiri hatima ya marejeo, lakini hawakufanya hivyo hadi ilipotolewa amri ya kuitwa mahakamani kueleza kwa nini wasifungwe jela kwa kushindwa kutekeleza amri ya mahakama.

Manji na Mwalusako walifika mbele ya Msajili Gwaye kwa ajili ya kujieleza kwa nini wasifungwe, lakini msajili hakuwapa nafasi ya kuwasikiliza wala kuhoji kwa sababu jalada mama la kesi hiyo liko Mahakama ya Rufaa.

Katika kiapo kilichoapwa na Mwalusaka, anadai kwamba msuluhishi wakati akitoa uamuzi hakutilia maanani nafasi ya Yanga, kwani haina mali za kuiwezesha kulipa fedha hizo, hivyo wanaomba uamuzi ubatilishwe.

Habari hii ni kwa hisani ya Mtanzania.

KARDINALI PENGO AWATUPIA LAWAMA POLISI KUWA WANAFUGA UHALIFU


Mwadhamu Polycarp Kardinali Pengo
Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kile alichosema kwamba limeshindwa kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Kiongozi huyo akiongelea upepelezi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Zanzibar aliyepigwa risasi mwezi uliopita alisema, “Siwezi kusema naridhika au siridhiki lakini tulitegema kwamba polisi wangetegua kitendawili cha wauaji wa padri huyo.”
Mazishi ya Padre Evarist Mushi.
Kardinali Pengo alisema Serikali haipaswi kusema wanaovuruga amani ni wahuni wakati hilo ni jukumu lake kuhakikisha inadumisha amani. Pengo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za Pasaka.

“Watu wanaharibiwa mali zao, watu wanapoteza uhai wao, Serikali haiwezi kukaa pembeni na kufikiri ni kauli za viongozi wa dini peke yao, viongozi wa dini hawana jeshi au hawawezi kukamata watu, Serikali ndiyo wana jukumu hilo kuhakikisha wanaingilia kati,” alisema Pengo na kuongeza:

“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya Kikristu na Waislamu ila ni wahuni wachache wanajichukulia madaraka, lakini lolote liwavyo Serikali haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi kutegemea nchi itawaliwe na wahuni kama vile Serikali haipo.”

Kuhusu Padri Mushi aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kwenda kwenye misa huko Zanzibar, Pengo alisema:
“Watanzania tungeambiwa zimechukuliwa hatua zipi na aliyehusika na mauaji hayo ni nani, lakini hali inayoonekana sasa hatujui.”
Aliongeza: “Siyo mimi wala Askofu wa Zanzibar (Augostino Shao) au askofu yeyote anaweza kukwambia kuwa kuna mtu amekamatwa, ila inaonekana kama mambo yanataka kuisha kimyakimya na kufanya hivyo haiwezi kuwa chimbuko la amani.”
Kardinali Pengo alisema vyombo vya kulinda amani vinapokuwa chimbuko la kuharibu amani kwa vyovyote nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea.
Alisema kunahitajika kukutanishwa kwa pande zote mbili za Wakristu na Waislamu, lakini akatoa angalizo kwa kubainisha mambo mawili ambayo yanahitajika kuzingatiwa ili kufikia mwafaka.

Alisema pande zote mbili watu wakitaka kujadiliana ni lazima kila upande uwe tayari kujadiliana na kupokea ukweli sambamba na kusema ukweli na siyo kupotosha ukweli kwa masilahi binafsi.

“Pili kila upande uwe na mawazo kwamba upande wa pili una nia njema, lazima watu wawe tayari kuwasiliana kuwa upande wa pili una nia njema, lakini kinyume na hapo itakuwa bure na kudanganyana na mambo yataendelea kuwa mabaya zaidi,” alisema Kardinali Pengo.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa kwamba katika mkesha wa Pasaka kuna watu watafanya vurugu, alisema haogopi kwani vyombo vya usalama vina jukumu la kuhakikisha raia wanakuwa salama.
IGP Said Mwema
“Mimi kazi yangu si kujiandaa kushika bunduki kwani Serikali wana jukumu la kulinda amani iwe kanisani au msikitini.
“Wanatakiwa kuchukulia mazungumzo hayo ‘serious’ (makini) kwani baada ya Padri Ambrose kujeruhiwa kwa risasi walisema wataendelea na kweli ikatokea Padri Mushi akauawa. Mimi sitaacha kwenda kanisani hata kama nitaambiwa nitauawa na kama kufa nife katika kanisa langu,” alisema.

Kauli ya Polisi
 
Advera Senso Msemaji Mkuu wa Polisi

Msemaji Mkuu wa Polisi, Advera Senso alisema upelelezi wa tukio la kifo cha Padri Mushi unaedelea na kuwaomba wananchi kusubiri kujua kinachoendelea.
“Kunapotokea tukio la aina yoyote lile polisi ndiyo jukumu lao kujua chanzo na hatua za kuchukua. Tunaomba watu tuwaachie wanaohusika ili kuweza kufanya kazi hiyo vizuri na tutawaeleza kinachoendelea upelelezi utakapokamilika,” alisema Senso.

Kuhusu uvumi wa matukio ya uhalifu wakati wa Pasaka, Senso alisema wanafuatilia taarifa hizo.
“Tunawaomba wananchi ambao wanajua ni kina nani wanaeneza taarifa hizo, watupe ushirikiano ili tuwachukulie hatua kutokana na kutoa taarifa za kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisema Senso.

Pia Novemba mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhili Soraga alimwagiwa Tindikali na watu wasiojulika wakati akifanya mazoezi kwenye Viwanja vya Mwanakwerekwe.

Mapema mwezi ulipita, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God (TAG) mkoani Geita, Mathayo Kachila aliuawa katika ugomvi wa kugombea kuchinja, katika tukio ambalo watu sita walijeruhiwa vibaya kwa mapanga.

Habari hii ni kwa hisani ya Mwananchi,Alhamisi, Machi 28,2013

Wednesday, March 27, 2013

KIJANA UMRI WA MIAKA 17 AGUNDUA PROGRAMU YA SIMU IITWAYO SUMMLY NA KUWAUZIA YAHOO

Nick D'Aloisio kijana aliyegundua programu
Ni kijana aitwaye Nick D'Aloisio aliyegundua programu ya habari kwenye simu za mkononi iitwayo SUMMLY aliyoigundua Desemba 2011. Baada ya kugundua programu hiyo ameweza kuingia mkataba na kampuni ya YAHOO na atakuwa anafanya kazi katika Kampuni hiyo huku aendelea na masomo yake ya kidato cha 6.
Hata hivyo, kwenye blogu yake,ameweza kuandika maneno yafuatayo kuhusiana na programu hiyo:-
 
" In true Summly fashion, I will keep this short and sweet.

I am delighted to announce Summly has signed an agreement to be acquired by Yahoo!. Our vision is to simplify how we get information and we are thrilled to continue this mission with Yahoo!’s global scale and expertise. After spending some time on campus, I discovered that Yahoo! has an inspirational goal to make people’s daily routines entertaining and meaningful, and mobile will be a central part of that vision.  For us, it’s the perfect fit.

When I founded Summly at 15, I would have never imagined being in this position so suddenly. I’d personally like to thank Li Ka-Shing and Horizons Ventures for having the foresight to back a teenager pursuing his dream. Also to our investors, advisors and of course the fantastic team for believing in the potential of Summly. Without you all, this never would have been possible. I’d also like to thank my family, friends and school for supporting me.

Most importantly, thank you to our wonderful users who have helped contribute to us receiving Apple’s Best Apps of 2012 award for Intuitive Touch! We will be removing Summly from the App Store today but expect our summarization technology will soon return to multiple Yahoo! products - see this as a ‘power nap’ so to speak.

With over 90 million summaries read in just a few short months, this is just the beginning for our technology. As we move towards a more refined, liberated and intelligent mobile web, summaries will continue to help navigate through our ever expanding information universe.

Sincerely,

Nick
Founder"

Hata sisi Watanzania tuige mfano wa kijana huyu na tuweze kuvumbua vitu mbali mbali.

UTATA WA ELIMU YA NAIBU WAZIRI MULUGO WAZIDI KUZUA MENGI


Imebainika kuwa mmoja wa watu ambao Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo (pichani)anadaiwa kutumia jina lake kutafuta kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari ya Southern mkoani Mbeya ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu kishiriki cha elimu Mkwawa (Muce), kilichopo mkoani Iringa.

Mhadhiri huyo ni Dick Aron Mulungu ambaye alisoma na Mulugo katika Shule ya Sekondari ya Songea Wavulana kati ya 1994 na 1996 na alijiunga na shule hiyo baada ya kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kafule, ambayo iko mkoani Mbeya.

Taarifa zinaonyesha kuwa Mulungu alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata Shahada ya kwanza katika Elimu (BA Education) 2001 na baadaye alisoma na kupata Shahada ya Uzamili (MA Development studies ) 2007.

Alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, mahojiano yalikuwa hivi:
Mwandishi: Hallow…(mwandishi akajitambulisha)
Mulungu: Sawa, unasemaje?
Mwanishi: Nazungumza na Dick Mulungu?

Mulungu: Ndiyo mimi.
Mwandishi: Hivi unamfahamu mtu anayeitwa Hamimu Agustino?
Mulungu: Aah… hivi ulisema unaitwa nani?
Mwandishi: Si nimeshajitambulisha jina na ofisi ninayotoka?
Mulungu: Nipigie kesho naona hapa kuna kelele.

Mwandishi: Mbona nakusikia vizuri tu?
Mulungu: Nipigie baada ya nusu saa basi.
Baada ya nusu saa…….
Mwandishi: Haloo… naona nusu saa imekwisha, uko tayari kuzungumza?
Mulungu: Huyo simfahamu.
Mwandishi: Kwani wewe si ulisoma Songea Boys?

Mulungu: Ndiyo
Mwandishi: Kwa hiyo humkumbuki mtu aliyekuwa akitumia jina hilo?
Mulungu: Huyo mtu namkumbuka ndiyo.
Mwandishi: Kwa sasa yuko wapi?
Mulungu: Siwezi kujua, si unajua tumesoma siku nyingi sasa huwezi kujua mtu amekwenda wapi… ni siku nyingi mno.
Mwandishi: Ahsante.

Chuo Kikuu na siasa
Taarifa zinaonesha kuwa Waziri Mulugo alijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania 2002 akitumia majina ya Philipo Hamimu Augustino na alisomea Shahada ya Sanaa katika Elimu (BA. Ed). Namba yake ya usajili chuoni hapo ni 08652/T.02.
Alipokuwa akiendelea na kazi ya ualimu Mulugo alianza harakati za kisiasa na ndipo alipoamua kwenda kugombea ubunge katika majimbo ya wilaya ya Chunya.

Kada wa chama cha NCCR Mageuzi wilayani Chunya, Nyawili Kalenda aliyejitambulisha kama mlezi wa siasa wa Waziri huyo alisema walifahamiana naye 2004 wakati Mulugo na rafiki yake walipokwenda kumtaka ushauri wa kugombea ubunge katika jimbo la Songwe.
Katika nakala za wasifu wake zinaonyesha kuwa 2008 alishika nafasi ndani ya CCM ambazo ni pamoja na mjumbe wa baraza la jumuiya ya wazazi wilaya ya Chunya, Katibu wa Elimu, Uchumi, Malezi na mazingira wa jumuiya ya wilaya hiyo na mjumbe wa baraza la wazazi mkoa wa Mbeya.

Kauli yake
Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule. “Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo.

Licha ya kukiri kurudia darasa la saba, Waziri Mulugo alisema jina la Hamimu amekuwa akilitumia katika elimu tangu awali na kwamba hakuvunja sheria kufanya hivyo.

“Jina la Hamim ni la nyumbani Philipo ni jina langu la ubatizo, nadhani haya ni mambo ya kawaida na kweli nilipokuwa shule watu walikuwa wananifahamu kama Hamimu pia Philipo ni jina langu la ubatizo na kumbuka tukifika chuo huwa tunatumia jina la baba.

“Na pia ni kweli nilirudia shule kwa sababu wakati ule wa Mwalimu Nyerere na Mwinyi (Ali Hassan), sheria ilikuwa inaruhusu maana wanafunzi walikuwa wachache mno, fikiria katika darasa letu la saba tulimaliza watu saba tu. Baadaye sheria hiyo ilibadilishwa,” aliongeza.

Kuhusu jina la Dick Mulungu, alikiri kumfahamu mtu huyo na kwamba walisoma wote shule ya Sekondari ya Songea Boys. Hata hivyo, alipinga kutumia vyeti vyake.

 “Ni kweli Dick Mulungu tulisoma wote Songea Boys. Lakini hili jina la Mulungu ni jina letu la ukoo. Babu yangu alikuwa akiitwa Filipo Milambo Mulungu, kwa hiyo niliendelea kulitumia hivyo hivyo na hata jina la Mulugo ni letu pia,” alisema.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa Mwananchi Jumanne,Machi 26,2013.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...