Thursday, March 21, 2013

WACHIMBA MADINI NA WAVUVI HARAMU WASABABISHA MAPIGANO MOROGORO

Mkuu wa kituo cha polisi cha kati Morogoro ,Mkuu wa Upelelezi Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA wakiwa eneo la tukio bwawani Mindu
 Katika hali isiyokuwa ya kawaida wavuvi na wachimba madini haramu katika bwawa la Mindu walizua tafrani jana jioni baada ya wachimba madini watatu Andrea Michael, Juma Hassani na Yusuph Abdallah kukamatwa na Maaskari wa kampuni ya Mputa Security wanaolinda bwawa hilo.
Wachimba madini haramu waliokamatwa Mindu kutoka kulia Yusuph Abdallah,Juma Hassan na Andrea Michael
 Askari mmoja alipigwa na wavuvi baada ya kwenda kuwaondoa katika eneo lisiloruhusiwa kuvuliwa samaki, katika kujitetea wavuvi hao waliwapigia simu wenzao ambao walikuja na mapikipiki yapatayo 6 na kila pikipiki ikipakiza watu watatu watatu.
 Mkurugenzi mtendaji wa MORUWASA ilimbidi aende polisi kuchukua maaskari ili kuweza kuimarisha usalama katika bwawa hilo na wakati maaskari wanafika eneo la tukio wavamizi hao walikuwa wameshakimbia lakini walifanikiwa kupata mchimba madini mmoja aitwaye Juma Hassani na kwendanaye kituoni.
Awali Mkurugenzi mtendaji wa MORUWASA Ndg.John K.Mtaita akiongelea swala la kuzima mitambo ya maji na kusababisha mji karibu mzima kukosa maji alisema wamefikia hatua hiyo baada ya maji yaliyokuwa yakiingia kituo cha kutibia maji kuwa machafu sana na yananuka kutokana na mvua kuingiza maji machafu bwawani Mindu.
Mkurugenzi mtendaji wa MORUWASA akiongea na Chief Kingalu katika eneo la Mindu.

Waandishi wa habari wakiwahoji wachimba madini haramu waliokamatwa bwawani Mindu.


Wednesday, March 20, 2013

MVUA ZASABABISHA MITAMBO YA KUSAFISHA NA KUTIBIA MAJI KUZIMWA MOROGORO

Maji yakiwa yanamwagwa eneo la kutibia maji Mafiga.
 Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha wataalam katika kituo cha kutibu na kusafisha maji Mfiga iliyochini ya Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Morogoro (MORUWASA) kuzima mitambo na kumwaga maji yaliyokuwa yanaingia mitamboni hapo kutoka katika bwawa la Mindu kutokana na maji hayo kuwa machafu sana kwa kujaa tope.
Sampuli ya maji yaliyokuwa yanatoka bwawa la Mindu na kuja sehemu ya kutibia maji Mafiga.
 Hali hii ilizidi zaidi kutokana na mvua iliyonyesha jana jioni hadi usiku iliyoingiza tope jingi sana kwenye mdomo wa bomba la kuchukulia maji katika bwawa la Mindu.Hata hivyo wataalamu hao wamesema watawasha mitambo tu mara hali ya maji itakaporejea katika hali yake ya kawaida.
Kuzimwa kwa mitambo hiyo kumeathiri wakazi wa Maorogoro wanaotegemea chanzo cha Mindu kukosa maji ambao ni zaidi ya 70%.
Bi.Getrude Salema Afisa Uhusiano wa MORUWASA.
 Akiongea na Blogu hii Afisa Uhusiano wa MORUWASA Bi. Getrude Salema amesema hali hii ni changamoto kwa MORUWASA. Hata hivyo amewasihi wakazi wa Morogoro kuwa wawe wavumilivu na kuwa maji yatakayowafikia yatakuwa salama pale tu watakapokuwa wamewasha hiyo mitambo na kuruhusu maji yaanze kuingia na kutibiwa.
Mkondo wa maji ya mvua unaongiza tope bwawa la Mindu.
Blogu hii imefanya ziara hadi Mitambo ya kutibia maji Mafiga, Bwawa la Mindu na Sehemu ambako maji ya mvua yanavuka barabara ya Iringa na kuingia bwawa la Mindu.Kilichoonekana ni uchimbaji wa madini karibu na bwawa,mifugo kutifua ardhi pamoja na kilimo ndo sababu zilizochangia tope kuwa jingi.
Maji ya mvua yakiwa yametuama kando kando ya barabara ya Iringa eneo la Mindu
Hata hivyo,kando kando ya barabara ya Iringa kumeonekana madimbwi mengi ya maji yakiwa yametuama kutokana na makaravati yanayopitisha maji ya mvua kuziba kiasi cha kusababisha maji kukaa kwa muda mrefu na mvua zinaponyesha zinasomba hayo maji hadi bwawa la Mindu.

Wafanyakazi wa MORUWASA wakiwa wameenda kujionea halihalisi ya mikondo inayoingiza maji ya  mvua bwawani.

SAMAKI WA MAJITAKA WAHISIWA KUUZWA KWA WATU MJINI MOROGORO


Katika hali ya kushangaza na kusikitisha, nikwamba vijana wenyeji wa Manispaa ya Morogoro wamekutwa wakikusanya samaki aina ya kambale katika mabwawa ya majitaka yanayotolewa tope ya Mafisa.
 Walipoulizwa wakasema wanaenda kula lakini uwalakini unakuja pale walipoonekana kukazana kukusanya samaki wengi na kwenda kuwasafisha.
 Wito wangu kwa wakazi wa Morogoro kuweni makini na samaki wanaouziwa na watu mitaani na kwa wale wenye mabucha kuweni waaminifu kwa kutonunua samaki watakao letwa kwao na vijana wa mtaani.
Na maafisa afya kuweni makini kwa kukagua samaki wanaouzwa kwenye mabucha na mitaani.

Monday, March 18, 2013

WAZIRI MKUU PINDA AONGOZA HARAMBEE MAGOMENI



WAZIRI MKUU Ndg.Mizengo Pinda ameongoza harambee ya papo kwa papo na kufanikiwa kukusanya sh. milioni 31.5 zikiwa ni ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda la Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waumini wa Kanisa hilo Jumapili asubuhi, Machi 17, 2013 kabla ya kuendesha harambee hiyo, Waziri Mkuu aliusifu uongozi wa Kanisa Katoliki la Magomeni kwa kuamua kufanya upanuzi wa kanisa hilo ili liweze kuhudumia waumini wengi zaidi.
“Nia yao ni nzuri sana na wameona mbali mapema. Magomeni hii ya leo si ya wakati ule, na wala haitakuwa hivi katika miaka mingine 50 ijayo. Zamani usingeweza kuona hata ghorofa moja hapa Magomeni lakini sasa hivi maghorofa hayahesabiki,” alisema.
Aliwasisitiza waumini hao kujitoa kwa ajili ya kazi ya Bwana kwa sababu hakuna sadaka ambayo ni ndogo. “Hakuna sadaka iliyo ndogo mbele ya Mungu, kikubwa ni dhamira tu. Kanisa ni letu na litajengwa na sisi waumini ili mradi kila mmoja wetu aseme Kansa hili nitalijenga,” alisisitiza.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waumini hao, Baba Paroko wa kanisa hilo, Padri Sixfrious Rwechungura alisema wameanza kazi ya ukarabati tangu Agosti 15, 2011 na kwamba hadi sasa wamekwishakusanya sh. milioni 350 iliyotokana na nguvu za waumini wenyewe bila msaada wa kutoka nje.
Alisema wanahitaji kiasi cha sh. milioni 300 ili kukamilisha kazi hiyo ambayo inapaswa kukamilika katika miaka miwili ijayo ili iendane na maadhimisho ya miaka 50 ya kanisa hilo.
Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mkewe Mama Tunu Pinda waliahidi kuchangia sh. Milioni 10 na kutoa sh. Milioni mbili za kianzio. Pia aliendesha mnada wa mbuzi aliyenunuliwa kwa sh. 600,000/- na mkoba ulionunuliwa kwa sh. 150,000/-.
(mwisho)

Friday, March 15, 2013

RAIS KIKWETE AKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 250 KATIKA HARAMBEE YA KUJENGA KANISA MOROGORO

Rais Kikwete akiendesha harambee
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo jipya la Kanisa katoliki la Kigurunyembe iliyofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Magadu mjini Morogoro usiku wa kuamkia leo Machi 15, 2013 akiongozwa na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Mhashamu Telesphor Mkude. Zaidi ya Shilingi milioni 250 zilipatikana katika harambee hiyo, ikiwa ni zaidi ya lengo la kupata milioni 200 walilojiwekea.
Rais Kikwete akiwa na Askofu wa jimbo la Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude.

MICHEZO: TANZANIA YAPANDA NAFASI 8 KATIKA VIWANGO VYA FIFA

 
Timu ya taifa ya Tanzania imepanda kiwango kwa nafasi 8 na katika viwango vya Afrika imepanda kwa nafasi 33.Kwa sasa Tanzania ni ya 119 huku Hispania ikibakia kuwa ya kwanza kwa ubora Duniani.
Kupanda kwa Tanzania kumetokana na kufanya vizuri kwenye michezo yake ya kimataifa iliyo kwenye kalenda ya FIFA.


Breaking news:WAHAMIAJI HARAMU 32 WAKAMATWA MKOANI RUKWA

Taarifa zilizotufikia hivi punde nikwamba Idara ya Uhamiaji mkoani Rukwa inawashikilia watu 32 wanao tuhumiwa kuwa wahamiaji haramu walioingia nchini kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kumekuwa na matukio kadhaa ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu katika maeneo tofauti ya nchi hii.
Taarifa zaidi tutawalete kadiri tutakavyokuwa tunazipata.

UCHIMBAJI HARAMU WA MADINI KANDO MWA MTO RUVU

Wakazi wa kijiji cha Kibangile, Morogoro vijijini wakiwa wanaendelea na uchimbaji haramu wa madini.
 Kumekuwa na kasumba ya wananchi kulalamika kuwa mara mvua hamna, mara jua kali na pia tumekuwa tukiwasikia viongozi na wataalamu mbali mbali wakitueleza kuwa kuna mabadiliko ya tabia nchi ulimwenguni kote, lakini ukija kuchunguza zaidi utangundua kuwa tatizo hilo linaanzia kwa mtu mmoja mmoja hadi kikundi hatimaye kidunia.
Uchimbaji madini kando mwa mto Ruvu
Uharibifu wa mazingira mmojawapo unaoendelea ni uchimbaji haramu wa madini unaoendelea hasa kando kando mwa mito na zaidi mto Ruvu ambao ni mto tegemezi wa vyanzo vya maji kwa mikoa ya Pwani na Dar es salaam ambapo kingo za mto zinaharibiwa na kusababisha maji kusambaa na kuleta mafuriko ikinyesha mvua.
Ofisi ya Bonde la Wami/Ruvu imekuwa na juhudi mbali mbali katika kuhakikisha uchimbaji haramu wa madini hauendelei katika kingo za mito ili kuifanya rasilimali maji inakuwa endelevu.
Uharibifu wa kingo za mto
Mfano ni uchimbaji unaoendelea katika kijiji cha KIBANGILE Wilaya ya Morogoro Vijijini ambako makundi ya watu yamekutwa wakichimba madini, hapa swali ni je,viongozi wa vijiji na kata hawawaoni au nao wanashirikiana nao katika kazi hiyo?

Thursday, March 14, 2013

RAIS KIKWETE ATEMBELEA CHUO KIKUU CHA WAISLAM CHA MOROGORO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Mrisho Kikwete leo asubuhi ametembelea Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM)
Jengo la ITC la Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro lililowekwa jiwe la msingi na Rais Kikwete.
Katika ziara hiyo Rais ameweka jiwe la msingi katika jengo la kituo cha "Information Technology and Communication" (ITC) na kuzindua jengo la Kitivo cha Sayansi cha chuo hicho.

Ziara ya Rais hii leo itaendelea kwa kuelekea Magadu Mesi ambako atafanya halambee ya kuchangisha fedha za kujenga kanisa katoliki la Kigurunyembe.

PAPA MPYA APATIKANA HUKO VATICAN

Papa Jorge Mario Bergoglio akisalimiana na Papa aliyejiuzulu.
Hatimaye ile kazi ya kumchagua papa mrithi wa Papa Benedict XVI aliyejiuzulu mwezi Februari imekamilika baada ya Kadinali Jorge Mario Bergoglio kuchaguliwa na  anakuwa mtu wa kwanza kutoka Amerika kusini kuchaguliwa kuwa Papa na  mara tu baada ya kuchaguliwa alichagua jina la Papa Francis I. Awali moshi mweupe ulishuhudiwa ukifuka kutoka kwenye dohani katika kanisa la Sistine Chapel na kufuatiwa na kengele kupigwa.
Papa Fransisco I alipojitokeza kwa mara ya kwanza huko Vatikani
Makadinali 115 wamekuwa faraghani tangu siku ya Jumanne alasiri na wakaanza mchakato wao kwa kupiga kura mara nne kwa siku.
Maelfu ya watu kutoka sehemu mbali mbali duniani walikuwa wamekusanyika katika ukumbi wa Kanisa la St Peter tangu siku ya Jumanne. Muda mfupi kabla ya Kadinali Bergoglio kujitokeza , maelfu ya watu walionekana wakikimbia kuelekea ukumbi wa St Peters ili kuweza kumshuhudia Papa mpya akitangazwa

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...