Friday, March 15, 2013

UCHIMBAJI HARAMU WA MADINI KANDO MWA MTO RUVU

Wakazi wa kijiji cha Kibangile, Morogoro vijijini wakiwa wanaendelea na uchimbaji haramu wa madini.
 Kumekuwa na kasumba ya wananchi kulalamika kuwa mara mvua hamna, mara jua kali na pia tumekuwa tukiwasikia viongozi na wataalamu mbali mbali wakitueleza kuwa kuna mabadiliko ya tabia nchi ulimwenguni kote, lakini ukija kuchunguza zaidi utangundua kuwa tatizo hilo linaanzia kwa mtu mmoja mmoja hadi kikundi hatimaye kidunia.
Uchimbaji madini kando mwa mto Ruvu
Uharibifu wa mazingira mmojawapo unaoendelea ni uchimbaji haramu wa madini unaoendelea hasa kando kando mwa mito na zaidi mto Ruvu ambao ni mto tegemezi wa vyanzo vya maji kwa mikoa ya Pwani na Dar es salaam ambapo kingo za mto zinaharibiwa na kusababisha maji kusambaa na kuleta mafuriko ikinyesha mvua.
Ofisi ya Bonde la Wami/Ruvu imekuwa na juhudi mbali mbali katika kuhakikisha uchimbaji haramu wa madini hauendelei katika kingo za mito ili kuifanya rasilimali maji inakuwa endelevu.
Uharibifu wa kingo za mto
Mfano ni uchimbaji unaoendelea katika kijiji cha KIBANGILE Wilaya ya Morogoro Vijijini ambako makundi ya watu yamekutwa wakichimba madini, hapa swali ni je,viongozi wa vijiji na kata hawawaoni au nao wanashirikiana nao katika kazi hiyo?

Thursday, March 14, 2013

RAIS KIKWETE ATEMBELEA CHUO KIKUU CHA WAISLAM CHA MOROGORO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Mrisho Kikwete leo asubuhi ametembelea Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM)
Jengo la ITC la Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro lililowekwa jiwe la msingi na Rais Kikwete.
Katika ziara hiyo Rais ameweka jiwe la msingi katika jengo la kituo cha "Information Technology and Communication" (ITC) na kuzindua jengo la Kitivo cha Sayansi cha chuo hicho.

Ziara ya Rais hii leo itaendelea kwa kuelekea Magadu Mesi ambako atafanya halambee ya kuchangisha fedha za kujenga kanisa katoliki la Kigurunyembe.

PAPA MPYA APATIKANA HUKO VATICAN

Papa Jorge Mario Bergoglio akisalimiana na Papa aliyejiuzulu.
Hatimaye ile kazi ya kumchagua papa mrithi wa Papa Benedict XVI aliyejiuzulu mwezi Februari imekamilika baada ya Kadinali Jorge Mario Bergoglio kuchaguliwa na  anakuwa mtu wa kwanza kutoka Amerika kusini kuchaguliwa kuwa Papa na  mara tu baada ya kuchaguliwa alichagua jina la Papa Francis I. Awali moshi mweupe ulishuhudiwa ukifuka kutoka kwenye dohani katika kanisa la Sistine Chapel na kufuatiwa na kengele kupigwa.
Papa Fransisco I alipojitokeza kwa mara ya kwanza huko Vatikani
Makadinali 115 wamekuwa faraghani tangu siku ya Jumanne alasiri na wakaanza mchakato wao kwa kupiga kura mara nne kwa siku.
Maelfu ya watu kutoka sehemu mbali mbali duniani walikuwa wamekusanyika katika ukumbi wa Kanisa la St Peter tangu siku ya Jumanne. Muda mfupi kabla ya Kadinali Bergoglio kujitokeza , maelfu ya watu walionekana wakikimbia kuelekea ukumbi wa St Peters ili kuweza kumshuhudia Papa mpya akitangazwa

Monday, March 11, 2013

BALOZI WA IRELAND ATEMBELEA MIRADI YA MAJI MOROGORO

Balozi wa Ireland akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi mtendaji wa MORUWASA Ndg.John.K.Mtaita.
 Balozi wa Ireland leo asubuhi ametembelea miradi ya maji mjini Morogoro inayofadhiliwa na Millenium Challenge Account-Tanzania (MCA-T). Katika ziara hiyo Balozi huyo ametembelea chanzo cha maji cha Mambogo ambako kunaukarabati mkubwa unaoendelea chini ya mradi huo kwa kujenga makingio ya maji, sehemu ya kutibia maji na birika la kusambazia maji.
 
Kukamilika kwa mradi huu kutapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya upungufu wa maji iliyokuwa inawakabili wakazi wa Manispaa ya Morogoro kwa muda mrefu sasa kutokana na uchakavu wa miundombinu ya maji.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Ndg.Joel.N.Bendera akisaini kitabu cha wageni
 Pamoja na kutembelea miradi hiyo pia balozi huyo ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).
Balozi wa Ireland akipokea maelezo kutoka kwa Mtaalam Mshauri Ndg.Tom Killilea

Balozi akipokea maelezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Ndg.Joel.N.Bendera




Friday, March 8, 2013

KIKAO CHA BODI YA MAJI CHAFANYIKA MOROGORO

Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Bonde la Wami/Ruvu Ndg.Washington Mutayoba na kulia ni Katibu wa Bodi Bi.Plaxeda Kalugendo
Kikao cha Bodi ya Maji kimefanyika leo katika ukumbi wa Edema mjini Morogoro.
Baadhi ya wajumbe la Bodi ya Bonde la Wami/Ruvu wakisikiliza kwa makini.
Katika kikao hicho mambo mbali mbali yamejadiliwa na mikakati ya kuboresha utendaji wa Ofisi ya Bonde la Wami/Ruvu imewekwa ili kuifanya Rasilimali Maji iwe endelevu.
Rasilimali Maji katika Wizara ya Maji inasimamiwa na Ofisi za mabonde yapatayo tisa (9) katika nchi nzima.


SIKU YA WANAWAKE YAFANA MOROGORO

Baadhi ya wanawake wa MORUWASA na Ofisi Za Bonde la Wami /Ruvu wakiwa tayari kuelekea kwenye maandamano.
Katika kusherehekea siku ya wanawake Duniani,mwandishi wa blogu hii amepita sehemu mbali mbali za mji wa Morogoro na kuwakuta wanawake wakiwa na furaha isiyokuwa na kifani.

Sehemu mojawapo ni katika ofisi za serikali MORUWASA na Ofisi za Bonde la Wami/Ruvu ambapo baadhi ya wanawake wa Ofisi hizo wamekutwa wakijiandaa kuelekea kwenye maandamano.

UHAMASISHAJI JUU UTUNZAJI WA RASILIMALI MAJI BONDE LA WAMI/RUVU

Afisa Maendeleo ya Jamii Bonde la Wami/Ruvu Bi.Nickbar Mwanana Ally akitoa mada wakati wa uelimishaji juu ya zana shirikishi katika usimamizi wa pamoja wa rasilimali maji katika Shule ya Msingi Kisemu-Mtamba Morogoro vijijini.
Katika kuhakikisha rasilimali maji inakuwa endelevu,Bonde la Wami/Ruvu linafanya jitihada za kuwahamasisha na kuwaelimisha wanchi wa Mikoa ya Dodoma,Morogoro,Pwani,Tanga na Dar es salaam juu ya utunzaji wa rasilimali hiyo.
Wakazi wa Morogoro vijijini kutoka vijiji 13 wakishiriki mafunzo katika shule ya msingi Kisemu-Mtamba

Ofisi ya Bonde la Wami/Ruvu inaendesha mpango wa ZANA SHIRIKISHI KATIKA USIMAMIZI WA PAMOJA WA RASILIMALI MAJI.Mpango huu unaendeshwa katika vijiji vyote na wananchi wanahamasishwa kushiriki katika shughuli za utunzaji vyanzo vya maji.
Miti jamii ya Misederea ambayo wakazi wengi wa Morogoro vijijini na Mvomero wameipanda kwa wingi karibu na vyanzo vya maji bila kuelimishwa wapi mahali bora pakupanda.Ukweli nikwamba miti hii ni hatari kuipanda karibu na vyanzo vya maji maana inanyonya maji kwa kasi sana.
Maofisa wa ofisi za Bonde la Wami/Ruvu wakichota maji katika moja ya chanzo cha maji Morogoro vijijini.Vyanzo vya maji vikitunza vizuri ni hazina ya sasa na kwa kizazi kijacho.

Wednesday, March 6, 2013

TFF YASALIMU AMRI KWA SERIKALI JUU YA KATIBA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewasilisha rasmi maombi ya kuonana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ili kuzungumzia uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya 2012.
Maombi hayo yaliwasilishwa rasmi Wizarani Machi 4 mwaka huu ambapo TFF imependekeza kikao hicho kifanyike Machi 7 mwaka huu) au Machi 13 mwaka huu.
Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Machi 2 mwaka huu kujadili tamko ya Waziri kutengua matumizi ya Katiba ya 2012 ndiyo iliyopendekeza kikao hicho kwa lengo la kusikiliza upande wa TFF katika suala hilo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

WATAALAMU WA AFYA NCHINI SASA KUWASILIANA BURE

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika juhudi zake za kuboresha afya za wananchi imeanzisha mfumo mpya wa mawasilano kama taarifa ilivyotolewa kwenye vyombo vya habari.
 


Madaktari na wataalamu wengine wa afya kuanzia sasa wataanza kupata huduma ya kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi bila malipo yoyote kwa wataalamu wenzao popote nchini na kupokea taarifa, maelekezo na ushauri unaohitajika kupitia mtandao wa mawasiliano ya simu za mkononi wa Vodacom pekee.


Health Network Programme hii imeanzishwa mahsusi kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wa madaktari na kuboresha kiwango cha mawasiliano ya wao kwa wao, na kwamba usajili wa mtandao huo kuanzia sasa unatarajia kuhusisha wataalamu wa afya wapatao 9,000 nchi nzima, wakiwemo madaktari, madaktari wa meno, madaktari wasaidizi, madaktari wasaidizi wa meno, tabibu na tabibu wasaidizi kukote waliko, serikalini na wale wa binafsi.

Aidha ili daktari aweze kujiunga kwenye programu hiyo atahitajika kutumia simu yake ambayo itakuwa na kadi ya simu (simcard) ya Vodacom na kisha kupiga *149*24# na baadaye kupata maelekezo ya namna ya kujisajili.

Mbali ya kupiga simu bure wanachama wa mtandao huo kwa kushiriki katika programu hiyo watakuwa na uwezo wa kutuma ujumbe mfupi ‘sms’ 50 bure kila mwezi kuwasiliana na wenzao waliojisajili ndani ya programu.

Mpango huo utakwenda mbali zaidi na kupanua wigo wa fursa kwa sekta hiyo katika kukabiliana na changamoto zake kwa haraka ili kukidhi matakwa ya Watanzania walio wengi.

Switchboard kwa utaratibu kama huu pia imefaulu kuwaunganisha karibu madaktari wote wa nchi za Ghana na Liberia, na kwamba zaidi ya simu milioni 4 zimepigwa kutoka mwaka 2008 hadi sasa ambapo madaktari wamekuwa wakisaidiana katika kuboresha huduma stahiki anazohitaji mgonjwa.

Kwa sasa madaktari karibu wote wa nchi hizo ni sehemu ya Mtandao wa Afya unaowawezesha kupata huduma za bure za mawasiliano sambamba na wao kwa wao kushirikiana na kusaidiana kitaalamu katika kila pembe ya nchi hizo kwa manufaa yao na wagonjwa.

Programu hiyo inadhaminiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Switchboard na Kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom.

Kwa wale watakaojisajili wanaombwa kutoa kibali kwa Timu ya Tafiti ya Mpango huu ya Switchboard yaani Programme Research Team (PRT) na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuweza kutathmini matumizi ya simu zao za mkononi ili kujua imeleta mabadilko kiasi gani katika sekta ya afya kupitia programu hiyo.

PRT na Vodacom hawatavujisha wala kujihusisha na taarifa zako zozote binafsi za mawasiliano kupitia simcard yako na kwamba kushiriki ni hiari yako, na unaweza kujitoa kwenye programu wakati wowote ukihitaji na hautatozwa wala kulipishwa gharama yoyote,”

Kupitia programu hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeiomba Switchboard kuratibu na kuweka mpangilio mzuri wa mchakato wote wa programu husika kwa manufaa ya wataalamu wa afya na ustawi wa tiba nchini.

UBORA WA MAJI WALETA KIZAAZAA MORO,MBUNGE AITEMBELEA MORUWASA KUJIONEA HALI HALISI.

Mbunge wa Morogoro Mjini Mh.Azizi Abood.
Wakazi wa Manispaa ya Morogoro jana walimvamia Mbunge wao Mh.Azizi Abood wakilalamikia ubora wa maji yaliyosambazwa mtaani kwao kuwa yalikuwa chini ya kiwango.Kutokana na malalamiko hayo ilimlazimu mbunge wa Morogoro Mjini kufanya ziara ya ghafla katika ofisi za Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira MORUWASA ili kujua kulikoni.
Gari la Mh.Mbunge alipowasili MORUWASA.
Akielezea sababu zilizopelekea kupungua ubora wa maji Mkurugenzi mtendaji wa MORUWASA Ndg.John K.Mtaita alisema hali hiyo ilitokana ukarabati wa sehemu ya kutibia maji Mafiga na usafishaji wa machujio ya maji.Hata hivyo,mkurugenzi huyo aliwaahidi wakazi wa Morogoro kuwa ubora wa maji utaimarika maradufu baada ya mradi wa ukarabati wa miundombinu utakapokamilika.
Mafundi wakiendelea na matengenezo ya bomba Msamvu stendi ya Dodoma.
 Hata hivyo,mbunge huyo aliweza kutembelea hata eneo la Msamvu ambapo bomba linatengenezwa ili wakazi wa Kihonda waweze kupunguziwa adha ya ukosefu wa maji.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...