Wednesday, April 16, 2014

UFAFANUZI ZAIDI KUHUSU MATANGAZO YA KAZI - UTUMISHI.

Waombaji wa fursa za ajira Serikalini kupitia Sekretarieti ya Ajira wametakiwa kuweka kumbukumbu sahihi za matangazo ya kazi wanazoziomba ili kurahisisha kujua ni tangazo gani aliomba pindi matangazo ya kuitwa kwenye usaili yanapotolewa.
Hayo yamesemwa  na  Bw. Lucas Mrumapili ambae ni  Naibu Katibu wa Idara ya Ajira katika Sekretarieti ya Ajira wakati akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya wasailiwa waliofika  ofisini kwake ili kujua majina ya kuitwa kwenye usaili wa nafasi za kazi za PPRA utafanyika lini.
Akijibu swali hilo alisema kuwa ofisi yake imejipanga vyema kuhakikisha kila tangazo linalotolewa usaili wake unafanyika kwa wakati. Hivyo kuwataka waombaji wa fursa za ajira kuwa wavumilivu wakati mchakato huo ukiendelea, ambapo alitolea ufafanuzi wa usaili wa matangazo husika akianzia tangazo la kazi la tarehe 28 Desemba, 2013 ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 14 Januari, 2014 kuwa usaili wake utafanyika mwisho mwa mwezi Aprili mwaka huu.
Mrumapili amesema kwa tangazo la tarehe 30 Desemba, 2013 ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 13 Januari, 2014 kuwa mchakato wake bado unaendelea kutokana na kuhitaji uchambuzi wa kina kwa kila kada maana baadhi ya waombaji kazi  wa tangazo hilo kujirudia zaidi ya mara mbili.

Aliongeza kuwa kwa tangazo la kazi la tarehe 23 Januari ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 6 Februari, 2014 kuwa usaili wake nao utafanyika mwisho mwa mwezi Aprili mwaka huu. Aidha, aliwataka waombaji wa nafasi iliyokuwa imetangazwa kwa ajili ya TACAIDS kuwa  nafasi hiyo mchakato wake ulisitishwa kutokana na nafasi hiyo kujazwa kwa kibali cha ajira mbadala, hivyo ofisi yake inaomba radhi kwa usumbufu ulijitokeza kwa waombaji wa nafasi hiyo.
 
Naibu Katibu amesema kwa tangazo la kazi la tarehe 22 Januari, 2014 ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 5 Februari, 2014 kuwa usaili wake umeshaanza kwa baadhi ya kada na kwa kada zilizobakia mchakato wa kuwaita waombaji wenye sifa kwa ajili ya usaili unaendelea.
Pia amefafanua kuwa kwa waombaji wa tangazo la tarehe 17 Februari, 2014 ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 3 Machi, 2014 mchakato wake nao uko katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuitwa kwenye usaili.
 
Aidha, amesema kuwa ofisi yake imefunga kupokea maombi ya kazi kwa  tangazo  la tarehe 18 Machi, 2014  kwa kuwa mwisho wa kupokea maombi  hayo ilikuwa tarehe 3 Aprili, 2014. Aliongeza kuwa kwa tangazo la tarehe 1 Aprili, 2014 nalo mwisho wa kupokea maombi ya kazi kwa tangazo husika ni leo tarehe 15 Aprili, 2014.
Mwisho amewataka waombaji wote wa fursa za ajira Serikalini kufuatilia taarifa zinazowekwa katika mtandao wa Sekretariti ya Ajira ili kupata ufafanuzi sahihi kadri unavyotolewa kila mara, kuliko kutegemea taarifa za kusikia kutoka kwa baadhi ya watu ambazo wakati mwingine huwa za kupotosha.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Ofisi ya Rais-Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
Kwa maelezo zaidi; wasiliana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Kwa barua pepe; gcu@ajira.go.tz  na Facebook-page ya “Sekretarieti Ajira”
au simu 255-687624975
15 Aprili, 2014

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...