Thursday, April 11, 2013

CHADEMA NA JUKWAA LA KATIBA KUJITOA KWENYE MCHAKATO WA KATIBA MPYA.

Mwenyekiti wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni Mh.Freeman Mbowe.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitajitoa katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo muhimu mawili hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu.

Wakati Chadema wakisema hayo, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limesema uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba uliomalizika siku tatu zilizopita katika maeneo mbalimbali nchini haukuwa huru na ni batili, huku likipendekeza urudiwe katika maeneo yote yaliyokumbwa na kasoro.

Katika hoja zake, Chadema kimesema kinataka kufutwa kwa uteuzi/uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata na badala yake wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na Kamati za Maendeleo za Kata (WDC).
Msimamo huo ulitolewa na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati akisoma hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/14 huku akiitaka Serikali kuwasilisha muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ili maeneo kadhaa yafanyiwe marekebisho.

“Katika Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba tunataka marekebisho ya vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalumu la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Pia vifungu vyote vinavyohusu ushiriki wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya Muungano.”

Jukwaa la Katiba
Kwa upande wake, Jukwaa la Katiba limesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kubadili mwenendo wake kuanzia katika utaratibu wa kuwapata wajumbe hao hadi uundwaji wa Bunge la Katiba na wananchi kupiga kura za maoni. Limesema isiporekebisha utaratibu huo, litakwenda mahakamani kusitisha mchakato mzima wa Katiba.

Kumalizika kwa uchaguzi huo kunaashiria kuanza kwa mabaraza ya Katiba Mei mwaka huu, ambayo yatakuwa yakijadili rasimu ya Katiba ambayo imetokana na maoni mbalimbali yaliyotolewa na wananchi.

Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba alisema uchaguzi huo ulikuwa na kasoro zaidi ya 15, ambazo ni itikadi za vyama na udini, rushwa, uchakachuaji, upendeleo, ubaguzi wa makundi ya watu wenye ulemavu na kukosekana kwa mwongozo timilifu wa uchaguzi huo.

Baadhi ya mikoa iliyokumbwa na kasoro hizo ni Dar es Salaam, Arusha, Mara, Singida na Dodoma. “Pia kulikuwa na vurugu katika uchaguzi huu, kukataliwa kwa barua za maombi za baadhi ya waombaji, kutokuwa na tarehe rasmi ya uchaguzi, uandikishaji bandia wa wapigakura, kukosekana kwa orodha ya majina ya wagombea katika mitaa na vijiji.”

Habari na Mwananchi

NAULI MPYA KUANZA KUTUMIKA RASMI KESHO.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolea na Mamlaka ya kudhibiti usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA),nauli mpya zitaanza kutumika kesho (Ijumaa) tarehe 12.04.2013.
Katika mabadiliko hayo,wanafunzi watakuwa wanasafirishwa kwa Tsh.200/= huko sehemu iliyokuwa inatozwa Tsh.300/= kwa watu wazima itakuwa Ts. 400/=
Katika mabadiliko hayo hata  nauli za kwenda Mikoani zitabadilika kama ifuatavyo:-


AZAM MWENDO MDUNDO,YAWANYUKA AFRICAN LION 3-1


Ligi kuu ya Vodacom imeendelea tena leo kwa mechi moja katika uwanja wa Azam Complex kati ya Azam na african Lion na mpaka dakika 90 zinakamilika Azam 3- Af. Lion 1.
Azam anazidi kumsogelea kinala wa ligi Yanga.

KUNDI LA BOKO HARAM LAKATAA MSAMAHA NIGERIA



Kundi la wapiganaji wa kiisilamu nchini Nigeria, Boko Haram , limekataa pendekezo la kukubali msamaha.
Wiki jana Rais Goodluck Jonathan, aliuomba mkutano wa maafisa wakuu wa usalama kutafakari swala la kuwapa msamaha wapiganaji hao ili kuwashawishi kusitisha harakati zao.
Tangazo na mtu anayeaminika kuwa kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau.
Katika miaka ya hivi karibuni, Boko Haram imekuwa ikiendesha kampeini ya ghasia na vurugu katika eneo la Kaskazini mwa nchi, na kuwaua takriban watu 2,000.
Kundi hilo linasema kuwa wapiganaji wake wanapigania kile wanachosema ni taifa la kiisilamu katika eneo la Kaskazini ambalo lina idadi kubwa ya waisilamu.
Bwana Shekau alisema kuwa kundi lake halijakosa hata kidogo, na kwa hivyo msamaha kwao sio jambo la kuzungumzia.
Aidha Shekau aliongeza kuwa ni jeshi la Nigeria ambalo linakiuka haki za waisilamu.
"nashangazwa kwa kuwa serikali ya Nigeria inazungumzia kuhusu msahama. Sisi tumefanya makosa gani? Ni sisi ambao tunapaswa kuwasamehe.'' alinukuliwa akisema Shekau
Mwandishi wa BBC nchini Nigeria,Will Ross, anasema kuwa viongozi wa kisiasa na kidini Kaskazini mwa nchi, wamekuwa wakimtaka rais Jonathan kuwasamehe wapiganaji hao, wakisema kuwa hatua za kijeshi dhidi ya wapiganaji hao hazisaidii kuleta amani.
Jopo la kutoa msahama liliundwa na serikali wiki jana na linajumuisha waakilishi wa jeshi.

Habari hii kwa hisani ya BBC

KUKITHILI KWA UCHAFU SOKO LA JIJI LA ARUSHA

Soko Kuu la jijini Arusha, limekithiri kwa takataka zinazotoa harufu mbaya  ambayo inalalamikiwa na baadhi ya wafanyabiashara kuwa inahatarisha usalama wa afya zao.

Wafanyabiashara hao wakiwemo wanaomiliki maduka yanayolizunguka soko hilo, waliliambia gazeti hili kwamba takataka hizo zinatupwa nje ya soko.

Hata hivyo walalamikaji hao hawakutaka majina yao yatajwe lakini walisema takataka  hizo zimerundikwa kwa  muda mrefu  bila ya kuzolewa na mamlaka zinazohusika.
Wafanyabiashara hao walisema katika kipindi hiki ambacho mvua zimekuwa zikinyesha mfululizo mkoani humo,  wamekuwa wakizishuhudia taka hizo zikioza na hatimaye kutoa harufu mbaya.
Mkuu wa soko hilo, John Lugiza alikiri kuhusu kuwapo kwa taka hizo na kwamba ni  kero hata kwa uongozi wa soko hilo.

Alisema kutokuzolewa kwa takataka hizo kunasababishwa na  gari kushindwa kuingia ndani ya soko na kwamba dampo la Muriet nalo  limejaa maji.


Habari hii kwa hisani ya Mwananchi.

SAFARI YA TANZANIA NA KIPANYA

Kwa vikwazo hivi kweli tanzania tutafika?????? Tafakari,Chukua hatua.

MAWAZIRI SASA HAWARUHUSIWI KUTOA SHUKRANI NA POLE BUNGENI

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge na Naibu Spika, Job Ndugai
KUANZIA sasa Bunge limepitisha kanuni za kuwabana mawaziri kutoa salamu za pongezi, shukrani na pole pindi wanapokuwa wakizungumza bungeni. Pia Mawaziri hao wamezuiwa kutaja majina ya wabunge waliochangia bajeti zao kwa kuwa kufanya hivyo ni kutumia vibaya muda wa Bunge.
Kauli hiyo, ilitolewa bungeni jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge ambaye pia ni Naibu Spika, Job Ndugai, alipokuwa akiwasilisha Azimio la Marekebisho ya Kanuni za Bunge.

Pamoja na mambo mengine, Naibu Spika alitoa kauli hiyo alipokuwa akifafanua kauli ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), aliyeonyesha kutoridhishwa na jinsi Spika wa Bunge anavyotumia Kanuni za Bunge juu ya matumizi ya muda.

Katika mazungumzo yake alipokuwa akichangia marekebisho ya kanuni hizo za Bunge, Lissu alimshutumu Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwamba anachangia kwa wabunge na mawaziri kupoteza muda kwa sababu wanapokuwa wanazungumza bungeni, husema maneno ambayo hayana msingi wowote bungeni.

Kwa mujibu wa Lissu, kitendo cha mawaziri na wabunge kutoa pole, kutoa pongezi na kushukuru bungeni, ni maneno yasiyokuwa na maana na kwamba kitendo cha Spika kuyaruhusu kinakiuka Kanuni ya 154 ya Bunge.

“Mheshimiwa Spika, pamoja na kusema hayo, naomba niseme jambo hili na nalielekeza kwako moja kwa moja na hili linahusu matumizi ya muda.

“Kiti chako kina nguvu sana na baadhi yetu tunaona kama kiti chako kitatumia vizuri Kanuni za Bunge, tunaweza kuokoa muda mwingi unaopotea bila sababu.

“Huu utaratibu wa mheshimiwa kusimama na kutoa pole, kutoa pongezi unapoteza muda bure na unakiuka kanuni za Bunge. Kwa hiyo, naomba tuweke utaratibu ili ikiwezekana Spika ashukuru au apongeze kwa niaba ya Bunge na Waziri Mkuu apongeze kwa niaba ya Serikali.

“Naamini kama tukifanya hivyo, wabunge watapata muda wa kuchangia badala ya huu utaratibu wa sasa ambapo muda unapotea bila sababu,” alisema Lissu.

Akitoa ufafanuzi wa kauli hiyo, Naibu Spika aliungana na Lissu na kusema kuwa japokuwa siyo busara Spika kumkatisha mbunge asizungumze, wabunge na mawaziri wanatakiwa kutumia muda vizuri kwa kujielekeza kwenye hoja moja kwa moja.

“Marekebisho haya ninayowasilisha hapa, yanalenga kuitendea haki bajeti ya Serikali, kwani wabunge sasa wanapata muda wa kujadili bajeti za wizara kabla ya ile bajeti kuu.

“Kuhusu suala la muda wa kuchangia, marekebisho haya mapya yanasema mbunge atakuwa akichangia kwa dakika 10, wakati wa Bunge la Bajeti na atakuwa akitumia dakika 15 wakati wa Bunge la kawaida.

“Lakini, chama kinaweza kuomba zile dakika kumi zigawanywe kwa wabunge wawili ili kila mmoja achangie kwa dakika tano. Juu ya hili suala la wabunge na mawaziri kutoa pongezi, shukrani na kutoa pole na mawaziri kutaja majina ya waliochangia bajeti zao, kuanzia sasa halitaruhusiwa na nawashauri wabunge kila mnaposimama mwende kwenye hoja na kama unajijua huna hoja, tafadhali usisimame kuzungumza,” alisema Naibu Spika.

Awali katika mazungumzo yake, mbali na kutoridhishwa na jinsi muda unavyotumiwa bungeni, Lissu alilisisitiza Bunge, kwamba kilichokuwa kimewasilishwa na Naibu Spika kilihusu sehemu ya tisa ya Kanuni za Bunge, inayohusu masuala ya fedha na kwamba isije ikatafsiriwa kwamba marekebisho hayo yamegusa na maeneo mengine.

Kuhusu muda wa wabunge kuchangia, aliunga mkono kila mbunge atumie dakika kumi badala ya 15 zilizokuwa zikiruhusiwa kikanuni kwa kile alichosema kuwa, mabadiliko hayo yatawafanya wabunge wengi wazungumze.

Pamoja na hayo, alisema kuna haja Bunge kuangalia upya kanuni ya 96, kifungu cha pili, cha tatu na cha nne kinachompa waziri mamlaka ya kuweka ukomo wa bajeti yake.

Naye, Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), waliunga mkono kwa nyakati tofauti marekebisho hayo na kusema yanalenga kulipa nguvu Bunge. Pamoja na mjadala huo, Bunge lilipitisha marekebisho hayo.

Tuesday, April 2, 2013

UKOSEFU WA MAJI NA KIBONZO CHA MASOUD KIPANYA LEO

Hii ni habari iliyokatika mfumo wa kibonzo,lakini kutokana na hali halisi ilivyo huko mitaani maeneo mengi ya Tanzania kibonzo hiki kinaweza kuwa kweli.

RAIS KIKWETE AKUTANA NA NAIBU RAIS WA KENYA WILLIAM RUTO.

Rais kikwete akiongea na Naibu Rais Mteule wa Kenya Mh.William Ruto
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete leo (jana) Aprili 1, 2013 amekutana na Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto  ambaye alikuwa nchini kwa mapumziko ya Pasaka.
Akiongea na mgeni huyo katika hoteli ya Seronera iliyoko katika mbuga ya wanyama ya Serengeti  mkoani  Mara, Rais Kikwete  amempongeza Mhe Ruto na Rais mteule wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta, kwa ushindi wao kwenye uchaguzi mkuu nchini Kenya.
Mhe Rais pia alimueleza Mhe Rutto furaha yake pamoja na kuridhishwa  na jinsi  uchaguzi ulivyofanyika kwa amani katika nchi hiyo.
Alielelezea  matumaini yake ya kuwa  urafiki uliopo kati ya Tanzania na Kenya  utadumishwa  pamoja na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mhe Rutto, ambaye aliwasili Mkoani  Mara wiki  iliyopita akiwa na mke wake na watoto, ameondoka  leo baada ya chakula cha mchana alichoandaliwa na mwenyeji wake.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

AMUUA MKEWE BAADA YA KUMFUMANIA

 Antony Lutta - Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora
Mkazi mmoja wa Kijiji cha Idubula, katika Kata ya Karitu ,wilayani Nzega, Tabora, amemuua mkewe kwa kumkatakata kwa mapanga baada ya kumfumania.

Akiongelea tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Antony Lutta, alisema tukio hilo lilitokea usiku wa mkesha wa Sikukuu ya Pasaka.

Lutta alisema mtuhumiwa alimfumania mke wake Veronica Maganga (20) akiwa chumbani kwake na mwanamume mwingine .

Kwa mujibu wa kamanda huyo, mwanamume huyo alifanikiwa kukimbia.
Alisema  hasira za mtuhumiwa katika tukio hilo  ziliishia kwa kumtakata mke kwa panga hadi alipokufa.

Kamanda Lutta aliwataka wananchi kutojichukulia sheria mikononi mwao na badala yake, waviachie vyombo vya dola kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa.
“Watu wamekuwa na tabia ya kujichukulia sheria mikononi kwa kuwahukumu watuhumiwa, huo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi na tunawasihi waache,” alisema kamanda huyo.

Alisema mtuhumiwa wa tukio hilo atafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa upelelezi.

Habari hii ni kwa hisani ya Mwananchi.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...