Jamali Malinzi - Rais mpya wa TFF |
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) anayemaliza muda
wake, Leodegar Tenga usiku wa kuamkia leo amemtangaza rasmi Jamal
Malinzi kuwa rais mpya wa Shirikisho hilo baada ya kushinda uchaguzi wa
rais wa TFF kwenye Ukumbi wa NSSF Waterfront, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa, Malinzi alipata kura
73, huku mpinzani wake pekee Athuman Nyamlani akiambulia kura 52. Hii ni
tofauti ya kura 21 kati ya mshindi Malinzi na Nyamlani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ndiye
aliyetangaza matokeo hayo na kuamsha shangwe ukumbini hapo huku wapambe
wa wagombe wengine wakitoka vichwa chini.
Awali kabla ya uchaguzi huo, Nyamlani ndiye aliyekuwa Makamu
wa rais wa TFF.
Kwa upande wa
makamu wa rais wa TFF, aliyeshinda ni Wallace Karia aliyepata kura 67,
akifuatiwa na Ramadhan Nasib aliyepata kura 52 na Iman Madega aliyepata
kura 6 tu.
Kabla ya
uchaguzi huo, Karia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi inayoendesha
Ligi Kuu ya Bara na Ligi Daraja la Kwanza.
KIDAU,
MGOYI, KABURU, NYENZI WASHINDA UJUMBE
Katika uchaguzi
wa wajumbe wa kamati ya utendaji, Wilfred Kidau alishinda kwa upande wa
kanda ya Dar es Salaam akiwabwaga Alex Crispine Kamuzelya, Muhsin Said
Balhabou na Omary Isack Abdulkadir. Aliyeshinda kanda ya Pwani na
Morogoro ni Geofrey Nyange ‘Kaburu’ aliyewabwaga Farid Nahdi, Juma Abbas
Pinto, Riziki Juma Majala na Twahil Twaha Njoki.
Khalid Mohamed ameshinda ujumbe kanda ya Tanga, Kilimanjaro
akimshinda Davis Elisa Mosha. Naye Msafiri Mgoyi ameshinda kanda ya
Tabora na Kigoma akimshinda Yusuf Hamis Kitumbo. Ayoub Nyenzi ameshinda
kwa upande wa Iringa na Mbeya akiwashinda David Lugenge, John Exavery
Kiteve, na Elias Mwanjala.
Kwa upande wa
Ruvuma na Njombe aliyeshinda ni James Mhagama aliyemshinda Stanley
William Lugenge. Naye Athuman Kambi ameshinda kanda ya Lindi na Mtwara
akiwashinda Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder. Na Blassy
Kiondo ameshinda kanda ya Katavi, Rukwa akimbwaga Ayubu Nyaulingo.
No comments:
Post a Comment