Wednesday, April 24, 2013

CHADEMA WAFUNIKA IRINGA,WAFANYA MKUTANO MKUBWA UKIONGOZWA NA DR.SLAA


Dr.Slaa akiwahutubia wakazi wa Iringa.
Jana CHADEMA walifanya mkutano mkubwa katika Manispaa ya Iringa kwa kutekeleza ahadi ya wabunge wa chama hicho waliyoitoa wakati wakiwahutubia wakazi wa Jiji la Mwanza kuwa watatembelea majimbo kadhaa ili kuwaeleza wananchi nini kilichotokea bungeni mpaka wabunge 6 wa chama hicho wakasimamishwa kuhudhulia vikao 5 vya Bunge.
Hapa ni picha mbali mbali kuhusiana na ziara hiyo ya Mkoani Iringa.
Msafara ukielekea Iringa.

Msafara ukiwa Mkoani Iringa.

Sugu akiwahutubia wakazi wa Iringa.
Dr.Slaa akiwa na Mbunge wa Ubungo Mh.John Mnyika.




RAIS UHURU KENYATTA AANZA KUTANGAZA BARAZA LA MAWAZIRI.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameanza mchakato wa kuunda serikali mpya ambapo ametangaza majina ya mawaziri wanne. Mawaziri hao ni pamoja na Dkt. Fred Okeng'o Matiangi ambaye ni waziri mteule wa Teknolojia na Mawasiliano, Henery Rotich ameteuliwa wizara ya Fedha, James Wanaina Macharia ndiye Waziri mteule wa Afya na Balozi Amina Mohammed ametangazwa Waziri wa mambo ya kigeni.
Ilitarajiwa kwamba Rais Kenyatta angewataja mawaziri wote 18, lakini amesema wengine watatangazwa baadaye na kuomba taifa kuwa na subira. Huku haya yakiarifiwa Bunge la Kenya limeidhinisha kamati maalum ambayo itawachuja mawaziri watakaoteuliwa na Rais.Kamati hiyo inaoongozwa na Spika wa Bunge Justin Muturi.
Chini ya katiba ya Kenya sharti bunge lipitishe majina ya maafisa wakuu wa serikali, wakiwemo Mawaziri, Mabalozi na wakuu wa tume za kikatiba.

Chanzo:BBC

Tuesday, April 23, 2013

DIAMOND KUFANYA SHOO KUBWA UINGEREZA...!!

Diamond anatarajia kufanya shoo kubwa nchini Uingereza kuanzia tarehe 27 mwezi 4.Hii ni kwa mujibu wa habari alizozitoa Diamond katika mtandao wake wa kijamii na Diamondi ameandika hivi:-
 

"Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru mwenyezi mungu kwa wingi wa rehema zake na mapenzi yake kwangu mpaka nuda na saa hii nipo hapa nilipo.....
Napenda kuchukua nafasi hii kuwataharifu mashabiki zangu wote...Hususani Mashabiki zangu wa Nchini Uingereza kuwa bado siku 6 tu toto la kimanyema.....kutoka Tandale .Ntakuwa nchini Uingereza Nikianza na show ya tarehe 27 mwezi wa 4....
Ntakuwa na Silaha zangu mbili za maangamizi.Nikizungumzia Dancers wangu wawili machachari na wazawa kutoka wasafi...Dumi Utamu na Mose Iyobo....!!
Nakuja kuweka Historia Mpya Uingereza....Ntahakikisha kuwa naididimiza ardhi ya Malkia kwa Michezo ya kuringa ringa na Mashetani ya Kimanyema yatakapopanda....Ts Gona Be Crayz Usikose....Asikudanganye mtu tarehe London ntakuwepo
tarehe 27 april na reading ntakuwepo Tarehe 5may.....!! 

Thats official me....
Njoo tulewe kwa pamoja kisha kesho muone ntampeleka nani kwa Bi Sandrah Nchini Tanzania.....Hii si yakukosa....!!

WASAAAAAAFIIIIIIII"


 Kila la heri Diamond, keep it up!!!!!

LEO NI LEO,BARCELONA vs BAYERN MUNICH


Vita kusaka tiketi ya kusafiri kwenda jijini London kwenye mchezo wa fainali wa klabu bingwa barani Ulaya inaanza usiku huu kati ya Mabingwa wa soka nchini Ujerumani dhidi ya inayotajwa kuwa timu bora kwa vilabu vya soka duniani kwa wakati huu FC Barcelona.
Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes amesema haogopeshwi na urejeo wa nyota wa Barcelona, Lionel Messi kuelekea mchezo huo wa kwanza wa nusu fainali ya klabu bingwa barani Ulaya.
Messi hajacheza mchezo wowote wa Barcelona toka alipoingia kama mchezaji wa akiba na kuisaidia timu yake kufuzu nusu fainal katika mchezo robo fainali dhidi ya Paris St-Germain ya Ufaransa. Lakini kuna kila dalili Muanjetina huyo mwenye umri wa miaka 25 ambaye ndiye mchezaji bora wa dunia kwa sasa,akajumuishwa kwenye kikosi cha Barcelona kwenye mchezo wa usiku wa leo.
Mwezi uliopita Messi aliweka rekodi kwenye ligi ya Hispania kwa kuwa mchezaji aliyezifunga timu zote zinazoshiriki ligi kuu nchini humo maarufu kama La Liga kwa misimu miwili mfululizo.
Barcelona inapambana kutaka kutwaa taji la tatu la klabu bingwa barani Ulaya ndani ya miaka mitano,Huku Bayern Munich ambao msimu ujao watakuwa chini ya aliyekuwa kocha wa Barcelona, Pep Guardiola, wao wanapambana kutafuta nafasi ya kucheza fainali yao ya tatu ndani ya miaka minne.
Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes ambaye aliwahi kuwafundisha mahasimu wa Barcelona, Real Madrid amesema licha ya kumheshimu mrithi wake wa kiti cha ukocha kwenye timu hiyo lakini hajaomba ushauri wowote kutoka kwa Guardiola na amejiandaa kwa kila namna kuhakikisha anaifunga Barcelona usiku huu. Aliongeza kwa kusema anaijua vizuri sana timu yake kuliko mtu yeyote na anafahamu soka ya Hispania na Barcelona wenyewe kwa undani mkubwa.
Wakati Barca wakiwa hawajaweka wazi kama watamuanzisha Messi au la, Baadhi ya wachezaji wa Barcelona akiwemo Xavi Hernandez alinukuliwa siku ya jumatatu akisema, kombe la ligi kuu nchini Hispania, La Liga lina umuhimu mkubwa kuliko klabu bingwa barani Ulaya.
Mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja wa Allianz Arena mjini Munich nchini Ujerumani,majira ya saa nne kasorobo usiku kwa saa Afrika Mashariki.

UBALOZI WA UFARANSA NCHINI LIBYA WASHAMBULIWA.

Bomu limelipuka nje ya ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli na kuwajeruhi walinzi wawili huku ikisababisha uharibifu mkubwa.
Mlipuko huo ulisababisha uharibifu katika sehemu moja ya ofisi hizo na pia kuharibu nyumba jirani.
Mwandishi wa BBC mjini Tripoli, Rana Jawad anasema kuwa inaaminika kuwa mlipuko huo ulisababishwa na gari lililokuwa na mabomu.
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, aliitaka serikali ya Libya kuchukua hatua za haraka kukabiliana na waliosababisha shambulio hilo.
Aliongeza kwamba shambulizi hilo lililenga nchi za kigeni zinazopambana dhidi ya ugaidi.
Balozi za kigeni nchini Libya zimewahi kushambuliwa katika siku za nyuma, lakini hili ndilo shambulizi la kwanza kubwa dhidi ya ubalozi wa kigeni mjini Tripoli.
Shambulizi liliwahi kufanywa dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi mwezi Septemba mwaka jana na kusababisha kifo cha balozi Christopher Stevens pamoja na maafisa wengine wamarekani .
Shambulio la leo lilifanyika muda wa saa kumi na moja alfajiri katika mtaa wa kifarahari mjini Tripoli.
Wakazi wa eneo hilo walighadhabishwa sana na shambulizi hilo na kulalamikia ukosefu wa ulinzi mzuri wa sehemu hiyo.
Waziri wa mambo ya nje wa Libya, Mohammed Abdel Aziz alilaani vikali shambulizi hilo, ingawa hawajaeleza ni nani wanayemshuku kulifanya shambulizi hilo.

CHANZO: BBC

KIKWETE:AFRIKA TUNAWEZA KUJISIMAMIA,TUMESHAKUA

Rais Jakaya Kikwete, amesema Bara la Afrika limepitia kwenye kipindi kigumu cha kukabiliana na utawala wa kikoloni ulioendesha mambo kwa kuzikandamiza nchi za Kiafrika, lakini sasa bara hilo limepiga hatua na linaweza kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kiusalama pasipo kutegemea msaada wa nje.

Rais Kikwete ambaye alikuwa akizungumza wakati akifungua kikao cha siku moja kilichowajumuisha mawaziri wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika (AU), alisema kuwa, Afrika imefanikiwa kujitambulisha kwenye duru la kimataifa kuwa ni bara linaloweza kujiamulia mambo yake bila kuingiliwa.

Alisema Umoja wa Afrika utaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea masilahi ya wananchi wa Kiafrika hasa katika kipindi hiki ambacho alisema kuwa kiwango cha migogoro kimeanza kupungua.

“ Kwa kweli hadi kufikia hapa Afrika imepiga hatua, tumeweza kuishughulikia na kuitatua migogo mingi iliyolikumba bara letu,tutaendelea kufanya hivyo katika siku za usoni na kwa kweli sasa tumedhamiria kupambana na viongozi wanaoingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi” alisema Rais Kikwete.

Alisema yale yanayoendelea kushuhudiwa sasa katika nchi za Mali, Jamhuri ya Kati ni matukio yasiyovumilika na kwamba suala la kutumia nguvu za kijeshi kwa ajili ya kurejesha utulivu na amani ni suala lisiloepukika.

“Nataka niwakumbushe pia wakati nikiwa mwenyekiti wa AU, tulifanikiwa kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini Comoro baada ya Kanali Bacar kujaribu kutaka kuteka moja ya kisiwa,na sasa haya tunayoyashuhudia Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati hayawezi kufumbiwa macho pindi itapolazimika sisi kwa umoja wetu tutalazimika kufanya hivyo hivyo “alisema.

Mbali ya kupigana kijeshi kisiwani Comoro, Tanzania inatazamia kushiriki operesheni ya kivita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa ajili ya kuwafurusha wanamgambo wa kundi la M23 ambao wamedhibiti eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.

Tanzania imeitikia wito wa Umoja wa Mataifa ambao hivi karibuni ulipitisha azimio lilitoa fursa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kushiriki operesheni ya kivita kama moja ya hatua ya kukabiliana na waasi hao.

Kuhusu hali ya kisiasa nchini Madagascar, Rais Kikwete alisema nchi za Sadc zitaendelea kufuatilia jinsi wanasiasa wa taifa hilo wanavyotekeleza makubaliano yaliyofikiwa baada ya upatanishi wa muda mrefu ulioongozwa na aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Joachim Chissano.

Mkutano huo wa mawaziri wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ulikuwa na agenda ya kujadili hali ya kisiasa nchini Madagascar kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Julai mwaka huu.

CHANZO:MWANANCHI

Monday, April 22, 2013

HATRICK YA ROBIN VAN PERSIE YATOSHA KUWAPA UBINGWA MAN UNITED.

Robin van persie akifunga goli la 3 (Hatrick)
Ilikuwa ni dakika ya kwanza RVP alipoipatia timu ya Man United goli la kwanza dhidi ya timu ya Aston Villa katika mchezo wa ligi kuu ya Uingereza mchezo uliopigwa katika uwanja wa Old trafford.
Ni dakika ya 12 Van Persie tena akaipatia timu yake goli la pili.Goli la tatu lilifungwa na Van persie tena ikiwa ni dakika ya 32.Magoli yote yalipatikana katika kipindi cha kwanza.Kutokana na kufunga magoli hayo matatu,Van Persie alitoka uwanjani na mpira baada ya kupiga Hatrick.
RVP akishangilia goli.
Van Persie alionekana kuwa mwimba katika ngome ya Aston  Villa baada ya kuwasumbua vyakutosha mabeki wa timu hiyo.
Na huu ndo msimamo baada ya matokeo hayo hapo juu:-

Club Pld Pts
Man Utd 34 84
Man City 33 68
Arsenal 34 63
Chelsea 33 62
Tottenham 33 61
Everton 34 56
Liverpool 34 51
West Brom 33 45
Swansea 33 42
West Ham 34 42
Fulham 34 40
Southampton 34 39
Norwich 34 38
Sunderland 34 37
Stoke 34 37
Newcastle 34 37
Aston Villa 34 34
Wigan 33 31
QPR 34 24
Reading 34 24

SERIKALI YAFUNGA VIWANDA VYA NONDO

Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limevifungia viwanda viwili vya kuzalisha nondo kwa muda usiojulikana.

Viwanda vilivyofungiwa ni vya Metro Steel Mills kilichoko Vingunguti Dar es Salaam na Quaim Steel Milis kilichopo Chang’ombe wilayani Temeke.

Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kwamba vimekuwa vikizalisha na kuuza nondo zisizo na ubora wa viwango vinavyokubalika na hivyo kuwa tishio kwa watumiaji wa bidhaa hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Quaim, Hassan Amir, alisema kiwanda chake kilianza kuzalisha nondo tangu mwaka 2006.

Katika maelezo yake, , alipinga hatua hiyo ya TBS akidai kwamba inafanywa kinyume cha sheria, kwa madai kuwa hakupewa barua kabla ya amri ya kukifunga kiwanda chake.
Hata hivyo Mwanasheria wa TBS Baptista Bitao alisisitiza uhalali wa hatua hiyo, akieleza kuwa inafanywa kwa kuzingatia sheria inayompa mamlaka Inspekta wa shirika hilo kukifungia kiwanda kinachokiuka sheria ya viwango ya mwaka 2009.

“Hatua ya kusimamisha uzalishaji wa bidhaa ni ya kwanza kisha barua inatakiwa ifuate katika kipindi cha siku tatu, hawa wamefungiwa ili waweze kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kuzalisha bidhaa zenye ubora, wakikiuka watawafikisha mahakamani,” alisema.

Meneja wa Kiwanda cha Metro, Onesmo Ngondo, alitoa lawama kwa TBS akidai kuwa haitoi elimu kwa wananchi na hasa wawekezaji, ili waweze kutambua umuhimu wa kupeleka bidhaa zao kuchunguzwa na kuthibitishwa kabla ya kuuzwa.

Akizungumzia kuhusu hatua hiyo, Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile alisema imetekelezwa baada ya TBS kuchukua sampuli ya vipande kadhaa vya nondo na kuvipima kwenye maabara yake.

Alisema katika uchunguzi huo, ilibainika kuwa nondo hazikuwa na ubora unaotakiwa.
Alisema hatua hiyo ya TBS ni mwendelezo wa kusaka bidhaa zinazozalishwa zikiwa chini ya kiwango.
Wiki iliyopita TBS ilianza kuzisaka nondo feki kwenye baadhi ya kampuni za usambazaji wa bidhaa hizo na kusimamisha uuzaji wa zaidi ya tani 1,350.
Hatua hiyo inafanywa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

CHANZO:MWANANCHI

RAIS TENGA ATOA MIPIRA YENYE THAMANI YA DOLA 30,000


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa mipira zaidi ya 1,200 yenye thamani ya dola 30,000 za Marekani kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na vituo 21 vilivyo hai vya kuendeleza vijana (academies).

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) lilimpa Rais Tenga fedha hizo ikiwa ni shukrani kwake kwa kushughulikia mgogoro wa uongozi wa mpira wa miguu nchini Kenya uliodumu kwa miaka miwili; ambapo nchi hiyo kutokana na mgogoro huo ilikuwa na vyama viwili (KFF na FKL).
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mipira hiyo kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Aprili 22 mwaka huu), Rais Tenga amesema amefanya hivyo kwa vile anaamini kuwa mipira ndiyo kitu muhimu katika kuinua mchezo huo mahali popote.

“Dhamira yangi si kushukuru kwa hafla hii, bali kutoa sababu kwa nini nimefanya hivi. Ninaamini kwa kuanzia mipira ndiyo muhimu, pili kwa kufanya hivi itaonekana kweli mipira imegawiwa,” amesema Rais Tenga.

Amesema amesema mpira wa miguu kwa Tanzania unahitaji sana watu wa kujitolea, na yeye amefanya hivyo kwa kujitolea kutokana na ukweli shughuli anazotumwa na FIFA ni za kujitolea.
Rais Tenga ambaye pia alitumwa na FIFA kutatua matatizo ya uongozi wa mpira wa miguu katika nchi za Uganda, Zambia na Sudan Kusini amesema anaamini anapata fursa hizo kutokana na kuwa kiongozi wa TFF, na kwa kuwakumbuka waliomchagua ndiyo maana hakusita kupeleka fedha hizo kwenye mipira.

Amesema moja ya ndoto zake wakati anaingia kuongoza TFF mwaka 2004 ameshindwa kutimiza ni kusaidia mipira, kwani uwezo wa kununua mipira kwa wanaocheza katika ngazi ya chini hasa watoto haupo.

“Hizi kelele zote za maendeleo ya mpira wa miguu ni kwa sababu shuleni hakuna vifaa. Nia yangu ilikuwa shule zote zipate mipira, lakini hiyo ni moja ya ndoto nilizoshindwa kutekeleza. Vipaji haziwezi kupatikana kama watoto hawachezi.

“Tunashukuru sana kwa Serikali kurejesha mpira shuleni. Hata nitakapoondoka madarakani nikipata nafasi nitaendelea kuomba mipira kwa ajili ya shule,” amesema Rais Tenga.

Vyama vya mikoa ambavyo jumla ni 32 (Tanzania Bara na Zanzibar) kila kimoja kimekabidhiwa mipira 25 (kumi saizi namba tano, 15 saizi namba nne kwa ajili ya vijana). Kwa academies ambazo ni 21 kila moja imepewa mipira 25 (minane saizi namba tano, na 15 saizi namba nne).

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Almasi Kasongo, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) Nassib Mabrouk na Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Riziki Majala.

Kwa upande wa shule alikuwa Kanali mstaafu Idd Kipingu ambaye ni mmiliki wa shule ya Lord Baden ya Bagamoyo mkoani Pwani. 

CHANZO:TFF

UPINZANI SYRIA WAIONYA HEZBOLLAH

Upinzani nchini Syria umelitaka kundi la wanamgambo nchini Lebanon la Hezbollah kuwaondoa wapiganaji wake kutoka Syria. Wanaharakati wamesema kuwa majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na watu wenye silaha wenye mafungamano na kundi hilo la Hezbollah, jana Jumapili walipambana na waasi wakitaka kuvidhibiti vijiji kadhaa karibu na mpaka wa Lebanon na Syria. Muungano wa upinzani wa Syria, umeonya kuwa kujihusisha kwa Hezbollah katika vita vya Syria kunaweza kusababisha hatari kubwa katika eneo hilo. Wakati huo huo, kiongozi wa muungano huo, Mouaz al-Khatib, jana amewasilisha barua ya kujiuzulu. Taarifa hizo zimetolewa kwenye ukurasa wa kijamii wa muungano huo, katika mtandao wake wa Facebook. Ama kwa upande mwingine, wanaharakati wameorodhesha majina ya watu 80 waliouawa katika mashambulizi yaliyofanywa na majeshi ya serikali kwa siku tano zilizopita.

CHANZO:IDHAA YA KISWAHILI YA UJERUMANI

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...