Monday, April 22, 2013

WABUNGE WA CHADEMA WALIOSIMAMISHWA BUNGENI KUWASHITAKI MAKINDA NA NDUGAI KWA WAPIGA KURA WAO.

Wabunge sita wa Chadema waliosimamishwa bungeni wameamua kwenda kuwashtaki Spika Anne Makinda na Naibu wake Job Ndugai kwenye majimbo yao.
Wakitangaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi ya Mbugani, Mwanza jana, walisema pia watakwenda kwenye majimbo ya wabunge wawili wa CCM, Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi) na Livingstone Lusinde (Mtera) ili kueleza jinsi wabunge wa upinzani wanavyokandamizwa bungeni.
Ndugai, ambaye ni Mbunge wa Kongwa (CCM), aliwasimamisha wabunge sita wa Chadema kuhudhuria vikao vitano vya Bunge kutokana na kile alichokiita kufanya vurugu bungeni. Hatua hiyo hatua ya Ndugai aliyoichukua Aprili 17, mwaka huu ilipata baraka za Spika Makinda Ijumaa iliyopita.
Wabunge waliosimamishwa ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Ezekiah Wenje (Nyamagana). Katika mkutano huo ulioanza saa 9.30 alasiri na kumalizika saa 12.00 jioni, ulihudhuriwa na wabunge wanne kati ya hao. Mbilinyi ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhutubia akifuatiwa Mchungaji Msigwa, Kiwia na Wenje. Lissu na Lema hawakuhudhuria.
Akizungumzia ziara yao katika majimbo ya viongozi hao wa Bunge, Mchungaji Msigwa alisema itakuwa ya kuwashtaki kwa kuendesha Bunge kuwapendelea wabunge wa CCM hata wanapofanya makosa ya wazi.
Alidai kuwa wabunge wa CCM ndiyo vinara wa lugha chafu bungeni na kuwatolea mfano Mwigulu na Lusinde. Pia alizungumzia tusi zito lililotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, Aprili 17, mwaka huu.
“Kila mtu alimshuhudia Serukamba alipoporomosha tusi zito, lakini Spika na Naibu wake hawakuchukua hatua zozote.
“Lissu na sisi wengine tumeadhibiwa kwa kosa la kuomba mwongozo wa Spika. Hapa wananchi mnaona kuna haki kweli,?” alihoji Mchungaji Msigwa huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Alisema watapita kwenye majimbo ya wabunge wa chama hicho waliosimamishwa ili kuwaelimisha wapigakura wao.
Alisema wataanza ziara majimboni kesho wakianzia Iramba Magharibi kumshtaki Nchemba. Baada ya hapo watakwenda Singida Mashariki kwa Lissu ili kuwapa ukweli wapigakura wake.
Mchungaji Msigwa alisema baada ya hapo watakwenda Kongwa kwa Ndugai na kisha Mtera kwa Lusinde kabla ya kuelekea Njombe Kusini kwa Makinda. Pia watakwenda Iringa, Mbeya, Kilimanjaro na Arusha.
Hata hivyo, ziara ya wabunge hao kwenda mkoani Mbeya imekwaa kisiki baada ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Athumani Diwani kukataa kutoa kibali.

Kumlipua kigogo CCM
Mchungaji Msigwa ameahidi pia kulipua bomu la kigogo wa ngazi ya juu wa CCM, ambaye alidai kuwa anajihusisha na ujangili wa meno ya tembo atakaporejea bungeni baada ya kumaliza adhabu yake wiki hii.

Wenje ataja safu ya 2015
Wenje aliwaambia wafuasi wa chama chake kuwa kimejipanga kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2015 na CCM wanapaswa kujipanga kuondoka madarakani.
Alitoa kali alimpotaja Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa kuwa Rais na Freeman Mbowe, Waziri Mkuu. Wengine aliowataja na kuwapa vyeo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Waziri wa Fedha), Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Kilimo), Lema (Mambo ya Ndani), John Mnyika (Nishati) na Wenje (Mambo ya Nje).

CHANZO:MWANANCHI.

Sunday, April 21, 2013

KINANA AISASAMBUA CHADEMA MOROGORO


Kinana akihutubia wakazi wa Morogoro leo Jioni.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameisasambua Chadema na kusema ni chama ambacho daima kimekuwa kikiweka mbele maslahi yake binafsi kuliko ya Watanzania.

Amesema viongozi wa chama hicho wamekubuhu kwa udikteta kiasi cha kujiona wao ndio wanajua kila jambo kuliko watu wengine hata mwenzao wa chama cha upinzani ikitokea ana mawazo  au msimamo wasioutaka au ameipongeza serikali kwao huonekana ni msaliti na kibaraka wa CCM.

Akihutubia leo mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika mjini hapa,Kinana, alisema kuwa Chadema ni balaa kwa nchi na watu kwani viongozi wake wamekuwa ni watu wa kuhubiri machafuko badala ya mshikamano uliozoeleka Tanzania.

Alisema kutokana na umangimeza wao sasa CHADEMA kimeanza kuigawa nchi kwa kutumia sera ya ukanda licha ya kwamba sera hiyo ni kinyume cha katiba ya nchi na watu wake.

"Ninapenda leo niwaelezeni ndugu Watanzania CHADEMA ilivyojawa na ubinafsi, wamekuwa wakiwakusanya Watanzania na kuwagawa kwa sera yao ya majimbo. Hili si mara ya kwanza maana katika kipindi cha siku za hivi karubuni walitangaza wazi kuigawa nchi kwa kutaka
kujitenga kanda ya Kaskazini eti ili iwe chini ya utawala wao", alisema Kinana.

Kinana alisema CCM kama chama kilichoingia mkataba na Watanzania haiwezi katu kukaa kimya na kuona hali hii ikitokea, kila mara tumekuwa tukihubiri amani na mshakamano lakini Chadema hili limewashinda jambo ambalo alisema ni dalili kwamba viongozi wa CHADEMA wameingia katika siasa kwa malengo yao binafsi.

"CCM itaendelea kusema ukweli kwa kila jambo na wala haitaficha hata likiwa siyo la kufurahisha wanachama wake ili mradi ni la kweli, tofauti na  hawa CHADEMA, lazima Watanzania muwe makini nao kutokana na aina ya siasa na matendo yao wanayojinasibvu nayo" alisema Kinana.

Vurugu za CHADEMA
Kinana alisema kuwa CHADEMA wamekuwa ni watu wa maajabu na vurugu kubwa nchini, na katika hilo alitoa mfano ya mambo ambayo wanayafanya bungeni.

"CHADEMA kazi yao ni vurugu tu, utadhani wao ndio wamekuwa kambi ya upinzani wa kwanza bungeni katika nchi  hii. Walikuwepo wapinzani  kabla yao kama CUF na Kina Mrema (Augustine Mrema) enzi za NCCR Mageuzi lakini hamkupata kushuhudia vituko kama hawa CHADEMA ambao wanajiona wao ndio kila kitu. Wanatoa vitisho kila siku kwa Serikali hata kumtukana mkuu wa Nchi bila kujali kwamba ni kiongozi ambaye amefika pele kwa kuchaguliwa na idadi kubwa ya Watanzania", alisema.

"Wanabeza wapinzani wengine , wakiona mpinzani anapongeza kazi iliyofanywa na CCM wanaanza kumshambulia.Hakuna anayejua zadi ya Chadema .Wanamtukana Rais, wanaushambulia usalama wa Taifa, wanashambulia vyombo vya usalama,"alisema Kinana

"Hawa jamaa ni watu wa ajabu sana, kila kitu wanajua wao wengine hawajui.Wakigombana katika chama chao utasikia kuna mkono wa CCM. Sijui ni watu wa aina gani , wanafanya mambo ya ajabu sana kiasi cha kushangaza,"alisema.

Kinana alitoa ushauri kwa Chadema kuwa na uwezo wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao kuliko kutumia muda wao mwingi kila jambo ambalo linakwenda kombo kunyoosha vidole kwa CCM.

"CCM tuna changamoto zetu nyingi, lakini tunatatua matatizo yetu wenyewe hatupotayari.Tuna makundi ndani ya chama lakini hayo ndio mambo ya siasa,"alisisitiza.

Mchakato wa Katiba mpya
Kinana alisema pamoja na kazi nzuri ambayo imefanywa katika mchakato wa Katiba mpya, kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni ametoa hotuba yake ambayo inaonesha wazi hakuna ambacho kimefanyika katika mchakato huo.

Alisema kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani Freeman Mbowe akiwa bunge ametumia muda wake mwingi kuzungumzia mchakato wa katiba mpya na kubwa katika hotuba yake kuwa haufai.

"Simsingizii kiongozi wa Kambi ya upinzani bungeni, ndani ya hotuba yake ameeleza wazi kuwa waliopewa dhamana ya kukusanya maoni ya Katiba mpya hawana ujuzi.Hii si kweli, waliopewa dhamana hiyo ni watu ambao wanaifanya kazi hiyo kwa uadilifu,"alisema.

Alisema Chadema ni watu binafsi ambao wao wametawaliwa na uroho mkubwa na wao kazi ni kuangalia maslahi zaidi na ni si maslahi ya nchi.

Ziara yake Morogoro
Kinana alisema kuwa ziara yake amejifunza mamb mengi lakini kubwa na msingi ambalo lipo kwa chama hicho kitahakikisha kinatafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi na hasa migogoro ya ardhi, mipaka na huduma za jamii ambazo nazo ni changamoto kubwa kwa maeneo mbalimbali.

"Ziara yangu na viongozi wengine wa chama chetu ambayo tuimefanya katika wilaya zote za Morogoro tumeona changamoto nyingi.Tumetafuta ufumbuzi wa matatizo lakini mengine yanapatiwa ufumbuzi baada ya kukaa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama na kisha kutoa maagizo kwa Serikali kutekeleza,"alisema.

Agizo kwa wabunge CCM
Katibu Mkuu huyo wa CCM, alitumia nafasi hiyo kwa kuwataka wabunge wa CCM kutembea kifua mbele kwani chama chao kinafanya kazi kubwa lakini aliwataka wawe makini na Chadema na kuwataka kutowasikiliza kwani sasa imetosha.

Alisema Chadema wamekuwa wakisikiliza muda mrefu ndani ya Bunge na kuna wakati wabunge wa CCM walichukia baada ya Rais Jakaya Kikwete kukubali kukutana nao kujadili mchakato wa Katiba Mpya.
Diamond akiburudisha kwenye mkutano wa CCM mjini Morogoro leo

Msanii Lina akiimba leo katika mkutano wa CCM

Chege na Temba wakiburudisha leo katika mkutano wa CCM
 CHANZO:MTANDAO WA KIJAMII WA CCM

KAZI YA UOKOZI KUTOKANA NA TETEMEKO NCHINI CHINA NI NGUMU

Wafanya kazi za uokozi wamekuwa wakipata shida kufika kwenye vijiji vya mbali milimani vilivyoko Kusini-Magharibi mwa China, baada ya tetemeko la ardhi ambalo imelipotiwa kuuwa watu 200 na kujeruhi zaidi ya 11,000.
Wanajeshi 17,000 wametumwa huko kwenda kusaidia.
Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi asubuhi karibu na mji wa Ya'an katika jimbo la Sichuan.
Waokozi wamekuwa wakijaribu kupanda barabara nyembamba zilizozongwa na maporomoko.
Lori moja la jeshi lilobeba wanajeshi 17 lilipinduka mlimani na kumuuwa mwanajeshi mmoja na kujeruhi wengine saba.
Magari ya kubeba wagonjwa yanawapeleka majeruhi katika kituo kwenye hospitali kuu mjini Ya'an.
Majeruhi wengi, baadhi yao wamevunjika viungo, wanatibiwa kwenye mahema yaliyowekwa nje ya hospitali.
Tetemeko hili lilikuwa ni dogo likilinganishwa na lile la mwaka 2008 ambalo liliuwa watu 70,000.
Lakini kwa sababu ya shida za kuwafikia majeruhi na vitetemeko vidogo vinavoendelea wakati wote, idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka.

CHANZO:BBC

CHADEMA WAITEKA MWANZA LEO

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefanya mkutano mkubwa Mwanza na hizi ni baadhi ya picha za mkutano huo:-



CHANZO:CHADEMA

MTUHUMIWA WA BOSTON HAWEZI KUHOJIWA KUTOKANA NA KUUMIA VIBAYA.

Meya wa Boston amesema wakuu wa Marekani pengine hawataweza kabisa kumhoji mshukiwa wa shambulio la bomu katika Boston marathon kwa sababu ya jinsi alivoumia.

Mshukiwa huyo, Dzhokar Tsarnaev, anatibiwa kwenye hospitali moja ya mjini Boston, ambayo ilieleza kuwa hali yake ni mbaya.

Alikamatwa Ijumaa wakati wa msako ambapo kaka ake aliuliwa na polisi.
Meya Tom Menino alipohojiwa na televisheni ya Marekani alisema anafikiri mashambulio hayo yalifanywa na ndugu hao wa kiume peke yao, na pengine hawakupanga kufanya mashambulio mengine.

CHANZO:BBC

Breaking news: HUDUMA ZA USAFIRI WA TRENI DAR KUANZA JUMATATU APRILI 22.

 Huduma za usafiri wa treni katikati ya jiji la dar es salaam zinatarajiwa kuanza tena Jumatatu Aprili 22 kufuatia kukamilika kwa Ukarabati wa reli katika eneo lililokuwa limeharibiwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni na kwamba hakuna badiliko la nauli.
Taarifa kamili tutawaletea baadae.

NJIA YA YANGA KUTWAA UBINGWA WA LIGI KUU YAZIDI KUTAKATA,YAILAZA JKT RUVU 3-0

Fuatana nami ujue nini kilikuwa kinatokea hatu kwa hatua kama ifuatavyo:-
Mpira unamalizika Yanga 3 - 0 JKT

Dk 90+4 Mgosi anachezewa faulo na Yondani nje kidogo ya eneo la hatari la Yanga. Faulo inapigwa na mpira unaokolewa na kuwa kona. Yanga 3-0 JKT

Dk 90+1 Nizar anapiga shuti kali linalopanguliwa na kipa wa JKT, Dihile.

Dk 89 Mwamuzi wa akiba Idd Soud anaonyesha bango kwa mpira umeongezwa dakika 5

Mara yangu ya mwisho kumuona Said Mohamed kwenye uwanja huu ni mwaka jana alipoingia kama sub kuchukua nafasi ya Yaw Berko kwenye mchezo ambao yanga walifungwa mabao 5:0 na Simba

Dk 86 Yanga inafanya mabadiliko ametoka Barthez ameingia Said Mohamed.
Dk 86 Inaonekana Barthez hawezi kuendelea na Said Mohamed anapasha misuli moto kujiandaa kuingia.

Dk 84 Kipa wa Yanga, Barthez anaanguka mwenyewe na mpira unaendelea kusimama ili Barthez atibiwe.

Dk 83 Mpira unasimama kwa muda baada ya Msuva kuchezewa rafu na Zahor Pazi. Yanga 3-0 JKT.

Dk 80 Jerry Tegete anaingia badala ya Hamis Kiiza

Dk 78 JKT wanafanya mabadiliko ametoka Ally Mkanga ameingia Charles Thadei.

Dk 76 JKT wamefanya mabadiliko ametoka Hassan Kikutwa ameingia Sosthenes Manyasi.

Dk 76 JKT wamefanya mabadiliko ametoka Hassan Kikutwa ameingia Sosthenes Manyasi.

Dk 75 Chuji wa Yanga anamchezea faulo Hussein Bunu wa JKT.

Dk 73 Msuva anachezewa faulo na Nashon Naftal nje kidogo ya eneo la hatari la JKT. Faulo inapigwa JKT wanaokoa. Yanga 3-0 JKT

Leo Yanga wametoa burudani kwa mashabiki walioingia uwanjani kwa soka safi

Shuti kali la Chuji linadakwa na kipa wa JKT

Goaaaaaaaaaaaal Nizar Khalfan anaipatia Yanga goli la 3

Dk 62 Mgosi anachezewa faulo na Kelvin Yondani.

JKT wanafanya mabadiliko anatoka Amos Mgisa anaingia Abdallah Bunu

Gooooooooal Free kick iliyopigwa na luhende imeunganishwa na Hamis Kiiza kwa kichwa

Dk 57 yanga wanapata faulo baaada ya Msuva kufanyiwa madhambi

Dk 55 Ally Nkanga analimwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Nizar

Dk 53 Kiiza wa Yanga anashindwa kuunga vizuri pasi ya Domayo kwa shuti lake kutoka nje ya eneo la hatari la JKT.

Dk 49 JKT wanapiga kona na Yanga wanaokoa.

Dk 49 JKT wanapata faulo nje kidogo ya eneo la hatari. Faulo inapigwa lakini Cannavaro anautoa nje mpira na kuwa kona.

Dk 48 Mgosi anapiga shuti hafifu na Barthez anaudaka mpira.

Kipindi cha pili cha mchezo kimeanza, JKT Ruvu 0 - 1 Young Africans

Dk 45 HALF TIME! Yanga 1-0 JKT

Simon Msuva anaipatia yanga bao hapa

Dk 41 Stanley Nkomola anapiga kona lakini kipa Barthez anaokoa.

Dk 39 Mgosi anamchezea faulo Cannavaro.

Dk 36 JKT wanapata faulo nje kidogo ya eneo la hatari la Yanga. Faulo inapigwa na mabeki wa Yanga wanaokoa.

Dk35 Hamis kiiza anakosa bao la wazi

Dk 31 Yanga inapata faulo nje kidogo ya eneo la hatari la JKT. David Luhende anamtengea Haruna Niyonzima lakini shuti lake linawababatiza mabeki wa JKT na mpira unaokolewa.

Dk 30 yanga wanapata kona nyingine Dihile anaokoa

Dk 26 Kwa mara ya tatu ndani ya dakika nne zilizopita mabeki wa Yanga wanamwekea Mgosi mtego wa kuotea naye anashindwa kung'amua hali hiyo na mara nyingi anajikuta akiwa ameotea.

Dk 26 Kwa mara ya tatu ndani ya dakika nne zilizopita mabeki wa Yanga wanamwekea Mgosi mtego wa kuotea naye anashindwa kung'amua hali hiyo na mara nyingi anajikuta akiwa ameotea.

Dk 24 Mussa Mgosi wa JKT anaipangua ngome ya Yanga lakini shuti lake linadakwa na kipa Ally Mustapha 'Barthez'.

Almanusura Nadir aipatie yanga bao kutokana na faulo ya Luhende

Dk 22 yanga wanapata faulo nje kidogo ya eneo la hatari

Dk 19 Athuman Idd Chuji wa Yanga anapiga shuti kali langoni kwa JKT lakini mpira unatoka nje kidogo ya lango.

Dk 18 Zahor Pazi wa JKT anachezewa faulo nje kidogo ya eneo la hatari la Yanga. Faulo inapigwa lakini mpira unatoka nje.

Dk 16 Yanga wanapata kona baada ya Damas Makwaya kuutoa nje mpira. Kona inapigwa na Dihile anaudaka mpira.

Dk 15 Kipa Dihile wa JKT anaudaka mpira wa krosi uliokuwa ukiwaniwa na Kiiza.

Dk 13 JKT wameanza kumiliki mpira na kuisumbua ngome ya Yanga. Yanga 0-0 JKT

Dk 12 Yanga inapata kona lakini kipa wa JKT, Shaaban Dihile anaudaka mpira.

Dk 10 Hamis Kiiza wa Yanga anamiliki mpira vizuri akipokea pasi ya Frank Domayo lakini mwamuzi Oden Mbaga anasema Kiiza ameoteaM

Yanga wanacheza vizuri sana hasa kwenye eneo la kiungo.

Dk 8 Mbuyu Twite wa Yanga anapiga shuti kali langoni kwa JKT lakini mpira unatoka juu kidogo ya mlingoti.

DIHILE AMENYANYUKA ANAPIGA FAULO

Shambulio hilo limesababisha golikipa wa JKT Dihile kuumia yupo chini anatibiwa

Dk ya tatu kona ya Luhende imesababisha kizaazaa kwenye lango la jkt ruvu

Yanga wanapata kona na inapigwa na David Luhende

Musa mgosi anamlazimisha Cannavari kuutoa nje mnamo dk 2

Mpira umeanza hapa taifa Yanga SC 0-0 JKT

Muda wowote kuanzia sasa soka litaanza na yanga ndo wanaanzisha kipute

Makame Rashid alifariki mwanzoni mwa juma hili,alikuwa mdau mkubwa wa soka

Wachezaji wanasimama kuomboleza kifo Makame rashid

JKT Ruvu line up: Shabani Dihile, Hassan Kikutwa, Stanley Mkomola, Madenge Ramadhan, Damas Makwaya, Nashon Naftar, Amos Mgisa, Ally Mkanga, Mussa Mgosi, Zahor Pazi na Haruna Adolph.


Kikosi cha Yanga

1.Ally Mustafa 'Barthez'
2.Mbuyu Twite
3.David Luhende
4.Nadir Haroub 'Cannavaro'
5.Kelvin Yondani
6. Athunman Idd 'Chuji'
7.Saimon Msuva
8.Frank Domayo
9.Hamis Kiiza
10.Nizar Khalfani
11.Haruna Niyonzima


Subs:
1.Said Mohamed
2.Shadrack Nsajigwa
3.Oscar Joshua
4.Salum Telela
5.Nurdin Bakari
6.Said Bahanuzi
7.Jerson Tegete
 
CHANZO,SHAFII DAUDA

AMUUA BABA YAKE KISA USHIRIKINA.

JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamsaka Richard Jecap (30) mkazi wa kitongoji cha Matai A kwa tuhuma za kumuua baba yake kwa kumpiga mpini kichwani  akimtuhumu kuwa ni mshirikina.
Tukio hilo lilitokea Aprili 18 saa 4.50 asubuhi wakati baba huyo akiwa amekaa nyumbani kwake akiota jua.
Akizungumza  mwenyekiti wa kijiji hicho, Emmanuel Mwakibinga alisema kuwa mtuhumiwa alifanya mauaji hayo baada ya watoto wake kufariki ambapo mtoto wa kwanza mwenye umri wa miaka minne alifariki Januari mwaka huu na alikuwa akidai baba yake huyo ndiye aliyemloga.
Alisema kuwa Aprili 16 mtoto wake wa pili mwenye umri wa miaka miwili alifariki na alidai kuwa baba yake ndiye aliyemloga kwani amekuwa akiloga watoto wake hao na siku ya mazishi aliahidi kumfanyia kitu kibaya baba yake huyo licha ya kuwa hakueleza ni kitu gani.

Mwenyekiti huyo alisema siku ya tukio hilo alikuwa akipita karibu na nyumba hiyo akasikia kishindo kikubwa kutoka eneo la nyumba hiyo na kisha kufuatia vilio vya watu na aliposogea alikuta mtuhumiwa huyo amekwishampiga mpini kichwani baba yake huyo na kisha kuanguka na kupoteza fahamu.
Baada ya kuona hivyo, walisaidiana pamoja na wanafamilia wengine kumwahisha hospitali na alitundikiwa maji sambamba na kushonwa katika jeraha kubwa alilolipata kichwani na usoni na kisha kulazwa ili  kuendelea kupata matibabu.
Mwakibinga alisema kuwa wakati akiendelea kupatiwa matibabu alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi na maumivu makali aliyokuwa nayo katika jeraha alilolipata baada ya kupigwa na mpini wa shoka kichwani.

CHANZO: MWANANCHI

BARAZA LA WAFANYAKAZI MORUWASA LATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA MIKUMI.

Baraza la wafanyakazi MORUWASA lilifanya ziara katika hifadhi ya taifa ya Mikumi baada ya kumaliza kikao chake cha siku mbili katika Hoteli ya Chuo Cha VETA MIkumi.Hii ni rasili mali na hazina kwa Taifa letu,wote tushirikane kulinda na kuhifadhi.

Hapa ni bwawa kati ya mabwawa 3 yaliyochimbwa mbuni mikumi.Wanyama wanaopatikana ni Mamba,Kiboko na ndege maji



Eneo la kuingilia mbugani Mikumi
Pundamilia ambao kitu pekee kwao nikwamba wanasimama kila mmoja akiwa ameelekea upande wake kwa ajili ya usalama

Hawa ni Tembo ambao wanapatikana kwa wingi mbugani Mikumi

Hawa ni nyumbu ambao nao wanapatikana kwa wingi Mikumi.

Hawa ni Twiga ambao kitu pekee kwao ni kuwa wakiwa wanatembea miguu ya upande mmoja inaenda pamoja tofauti na wanyama wengine ambao wanapishanisha miguu.

Huyu ni kiboko aliyemo kwenye mabwawa yaliyochimbwa.

Hawa ni nyati ambao wanasemekana kuwa wanya wakorofi hasa wakimuona mwanadamu.
Mikumi kuna hata uwanja wa ndege,unaweza kutua moja kwa moja na ndege.
Watu husema twiga huwa halali ukweli nikwamba analala kama anavyoonekana lakini hawezi kuinamisha kichwa,analala hivo hivo

Hawa ni swala ambao wanapatikana kwa wingi Mikumi.Kitu cha pekee kwao ni kwamba dume moja unakuta linamiliki kundi kubwa la majike hata kuzidi idadi ya 100.



BOSTON YATULIA BAADA YA MSAKO MKUBWA

Wananchi wa Bosto wakionesha furaha yao baada ya msako kukamilika
 Jiji la Boston linarejea katika hali ya kawaida baada ya mojawapo wa msako mkubwa katika historia ya polisi ya Marekani kumalizika kwa kukamatwa kijana mmoja anayeshukiwa kuhusika katika shambulio la mabomu wakati wa mbio za marathon siku ya Jumatatu.
Shughuli zilisimama katika jiji zima mnamo siku ya Ijumaa wakati polisi waliposambazwa kila pembe kumtafuta mshukiwa huyo Dzhokhar Tsarnaev, mwenye umri wa miaka19.
Alipatikana amejificha bustanini mwa nyumba moja katika kitongoji kimoja na alikamatwa baada ya mapambano ya risasi ambapo alijeruhiwa.
Kaka yake , Tamerlan, aliuwawa awali katika mapambano ya risasi na polisi. .
Watu watatu waliuwawa na zaidi ya 170 walijeruhiwa katika mashambulio ya mabomu ya siku ya Jumaatatu na afisa mmoja wa polisi aliuwawa wakati wa msako wa washukiwa..
Dzhokhar Tsarnaev anazuiliwa chini ya ulinzi mkali hospitali ambako pia wanatibiwa wengi wa waliojeruhiwa na mabomu siku ya Jumatatu.
Maafisa wa polisi wanasema wananuia kumhoji bila ya kumsomea haki zake kama mshukiwa --kama haki yake ya kumwita wakili na kutosema chochote kwa sababu za usalama kwa raia.
Uamuzi huo ulishutumiwa na Jumuiya inayotetea haki za raia nchini Marekani ilioyosema kwamba hatua kama hiyo inahusu tu kesi ambazo zinahusika na vitisho vya papo hapo kwa usalama na wala hakuna sababu ya kumnyima mshukiwa haki hizo.
Lakini baadhi ya wabunge wa chama cha Republican wamehoji kwamba Tsarnaev achukuliwe kama ni-mpiganaji adui ikimaanisha hastahili kupewa haki kama anazopewa mshukiwa wa jinai.

CHANZO:BBC

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...