|
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge na Naibu Spika, Job Ndugai |
KUANZIA sasa Bunge limepitisha kanuni za kuwabana mawaziri kutoa
salamu za pongezi, shukrani na pole pindi wanapokuwa wakizungumza
bungeni. Pia Mawaziri hao wamezuiwa kutaja majina ya wabunge
waliochangia bajeti zao kwa kuwa kufanya hivyo ni kutumia vibaya muda wa
Bunge.
Kauli hiyo, ilitolewa bungeni jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Kanuni za Bunge ambaye pia ni Naibu Spika, Job Ndugai, alipokuwa
akiwasilisha Azimio la Marekebisho ya Kanuni za Bunge.
Pamoja na
mambo mengine, Naibu Spika alitoa kauli hiyo alipokuwa akifafanua kauli
ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), aliyeonyesha
kutoridhishwa na jinsi Spika wa Bunge anavyotumia Kanuni za Bunge juu ya
matumizi ya muda.
Katika mazungumzo yake alipokuwa akichangia marekebisho ya kanuni
hizo za Bunge, Lissu alimshutumu Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwamba
anachangia kwa wabunge na mawaziri kupoteza muda kwa sababu wanapokuwa
wanazungumza bungeni, husema maneno ambayo hayana msingi wowote bungeni.
Kwa
mujibu wa Lissu, kitendo cha mawaziri na wabunge kutoa pole, kutoa
pongezi na kushukuru bungeni, ni maneno yasiyokuwa na maana na kwamba
kitendo cha Spika kuyaruhusu kinakiuka Kanuni ya 154 ya Bunge.
“Mheshimiwa
Spika, pamoja na kusema hayo, naomba niseme jambo hili na nalielekeza
kwako moja kwa moja na hili linahusu matumizi ya muda.
“Kiti
chako kina nguvu sana na baadhi yetu tunaona kama kiti chako kitatumia
vizuri Kanuni za Bunge, tunaweza kuokoa muda mwingi unaopotea bila
sababu.
“Huu utaratibu wa mheshimiwa kusimama na kutoa pole,
kutoa pongezi unapoteza muda bure na unakiuka kanuni za Bunge. Kwa hiyo,
naomba tuweke utaratibu ili ikiwezekana Spika ashukuru au apongeze kwa
niaba ya Bunge na Waziri Mkuu apongeze kwa niaba ya Serikali.
“Naamini
kama tukifanya hivyo, wabunge watapata muda wa kuchangia badala ya huu
utaratibu wa sasa ambapo muda unapotea bila sababu,” alisema Lissu.
Akitoa
ufafanuzi wa kauli hiyo, Naibu Spika aliungana na Lissu na kusema kuwa
japokuwa siyo busara Spika kumkatisha mbunge asizungumze, wabunge na
mawaziri wanatakiwa kutumia muda vizuri kwa kujielekeza kwenye hoja moja
kwa moja.
“Marekebisho haya ninayowasilisha hapa, yanalenga
kuitendea haki bajeti ya Serikali, kwani wabunge sasa wanapata muda wa
kujadili bajeti za wizara kabla ya ile bajeti kuu.
“Kuhusu suala
la muda wa kuchangia, marekebisho haya mapya yanasema mbunge atakuwa
akichangia kwa dakika 10, wakati wa Bunge la Bajeti na atakuwa akitumia
dakika 15 wakati wa Bunge la kawaida.
“Lakini, chama kinaweza
kuomba zile dakika kumi zigawanywe kwa wabunge wawili ili kila mmoja
achangie kwa dakika tano. Juu ya hili suala la wabunge na mawaziri kutoa
pongezi, shukrani na kutoa pole na mawaziri kutaja majina ya
waliochangia bajeti zao, kuanzia sasa halitaruhusiwa na nawashauri
wabunge kila mnaposimama mwende kwenye hoja na kama unajijua huna hoja,
tafadhali usisimame kuzungumza,” alisema Naibu Spika.
Awali
katika mazungumzo yake, mbali na kutoridhishwa na jinsi muda
unavyotumiwa bungeni, Lissu alilisisitiza Bunge, kwamba kilichokuwa
kimewasilishwa na Naibu Spika kilihusu sehemu ya tisa ya Kanuni za
Bunge, inayohusu masuala ya fedha na kwamba isije ikatafsiriwa kwamba
marekebisho hayo yamegusa na maeneo mengine.
Kuhusu muda wa
wabunge kuchangia, aliunga mkono kila mbunge atumie dakika kumi badala
ya 15 zilizokuwa zikiruhusiwa kikanuni kwa kile alichosema kuwa,
mabadiliko hayo yatawafanya wabunge wengi wazungumze.
Pamoja na
hayo, alisema kuna haja Bunge kuangalia upya kanuni ya 96, kifungu cha
pili, cha tatu na cha nne kinachompa waziri mamlaka ya kuweka ukomo wa
bajeti yake.
Naye, Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM) na
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), waliunga mkono kwa nyakati
tofauti marekebisho hayo na kusema yanalenga kulipa nguvu Bunge. Pamoja
na mjadala huo, Bunge lilipitisha marekebisho hayo.