MADIWANI
wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Kagera waliofukuzwa
uanachama wiki iliyopita wamekaribishwa kujiunga na Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA).
Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe, ndiye aliyewakaribisha madiwani hao wanaosubiri
kufukuzwa rasmi na vikao vya Kamati Kuu ya CCM, vinavyotarajiwa
kufanyika wiki hii mkoani Dodoma.
Madiwani
waliofukuzwa na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar (Miembeni),
Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni
naibu meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa
wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi
(Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna
(Ijuganyondo).
Akihutubia
katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Uhuru wa Bukoba Mjini, Mbowe
alisema CCM imewachakachua madiwani hao wanane na hata wakibaki huko
chama chao hakitawaona wa maana, kwa sababu chama hicho kinalea ufisadi.
Mbowe alisema
CHADEMA wako tayari kuwapokea madiwani hao waliofukuzwa na kuwafundisha
siasa za mageuzi.
“Tutasimama
nao katika kujenga Bukoba mpya isiyo na ufisadi kama unaofanywa na Meya
wa manispaa hiyo iwapo wataamua kuja kwetu, milango ipo wazi
nawakaribisha,” alisema.
Mbowe alisema
CHADEMA kinamuunga mkono Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Hamis Kagasheki
(CCM), anayepinga ufisadi unaofanywa na meya kutoka chama chake, Anatory
Amani.
Alisema
CHADEMA itashirikiana na kiongozi yeyote kutoka CCM atakayekuwa tayari
kupambana na ufisadi ulioshamiri kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.
“CHADEMA
katika mambo ya ufisadi ina msimamno unaoeleweka na kwamba katika
kupinga ufisadi kipo tayari kumuunga mkono yeyote bila kujali itikadi,”
alisema Mbowe na kusisitiza kwamba hata kama meya angekuwa mwanachama wa
CHADEMA kingeunga mkono afukuzwe.
“Hatuna
masilahi ya kisiasa na Kagasheki lakini katika suala hili tunamuunga
mkono. Nawapongeza madiwani wetu wa CHADEMA walioungana na mbunge huyo
kupinga ufisadi wa meya na kusimamia masilahi ya wananchi wa Bukoba
Mjini,” alisema Mbowe.
Mbowe
aliikejeli CCM kuwa haiwezi kuwafukuza madiwani hao kwa sababu itakuwa
imejimaliza na hawana uhakika wa kuzirejesha kata hizo ukiitishwa
uchaguzi.
Alisema
kutokana na hofu hiyo Makao Makuu ya CCM yaliamua kuwarejesha madiwani
hao wanane waliofukuzwa na CCM Mkoa wa Kagera.