Mhe. Dkt Mohammed Gharib Bilali – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano,
Mhe. Mizengo K. P. Pinda (Mb.) - Waziri Mkuu,
Mhe. Seif Sharif Hamad – Makamu wa Kwanza wa Rais – Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar,
Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (Mb.) - Makamo wa Pili wa Rais - Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar,
Mhe. Mathias Chikawe – Waziri wa Katiba na Sheria,
Mhe. Abubakar Khamis Bakary - Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar,
Mhe. Jaji Frederick M Werema - Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,
Mhe. Othman Masoud Othuman - Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume na Wajumbe wa Sekretarieti ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba,
Ndugu Wananchi,
Wageni Waalikwa,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana,
UTANGULIZI
Ndugu Wananchi,
Awali ya yote namshukuru mwenyezi mungu kwa kutuwezesha kufikia hatua hii ya
leo ya kuzindua Rasimu ya Katiba. pia, niwashukuru ninyi nyote mliohudhuria
halfa hii ikiwa ni mwendelezo wa mchakato muhimu wa Mabadiliko ya Katiba ya
nchi yetu.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilipitishwa Bungeni Novemba, 2011 na kufanyiwa
mabadiliko Februari, 2012. Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa mujibu wa
Kifungu 6(1) cha sheria hiyo (Cap.83). Wajumbe 34 wa Tume waliteuliwa na
kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,
mwezi Aprili, 2012. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume imepewa
miezi kumi na minane kukamilisha kazi yake kuanzia siku ilipoanza kazi rasmi
ambayo ilikuwa Mei 2, 2012.
Tume iliandaa ratiba ya utekelezaji wa majukumu yake. Kufuatana na ratiba hiyo
Tume ilijipanga kukusanya maoni ya wananchi katika kipindi cha miezi mitano
kuanzia Mwezi Julai hadi Disemba, 2012. Kazi hiyo ilifanywa kama tulivyopanga.
Tume ilijigawa katika makundi na ilitembelea mkoa yote thelathini.
Tume ilifanya mikutano 1,942 ambayo ilihudhuriwa na
wananchi wapatao 1,365,337 ambao kati ya hao wananchi 333,537
walitoa maoni ama kwa mazungumzo ya ana kwa ana au kwa maandishi. Tume
pia ilipata maoni ya wananchi wengi, wa ndani na nje ya nchi kwa njia mbali
mbali kama vile; Mikutano ya hadhara, Fomu maalum za Tume, barua kupitia
Masanduku ya Barua ya Tume, Mitandao ya Kijamii ya barua pepe; facebook ya
Tume, Tovuti ya Tume; Makala mbalimbali kutoka kwenye magazeti na ujumbe mfupi
wa simu.
Tume ilitumia mwezi Januari, 2013 kukusanya maoni ya makundi mbali mbali katika
jamii, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa, taasisi za Serikali, taasisi za
dini, wakulima, wafugaji, wafanyakazi, asasi za kiraia na kadhalika. Makundi
zaidi ya 160 yalikutana na Tume na kutoa maoni. Tume pia
ilipata maoni ya viongozi wa juu wa Serikali walioko madarakani na
waliostaafu. Kwa jumla viongozi 43walitoa maoni.
Tume ilipanga kutumia miezi mitatu ya Februari, Machi na Aprili kuchambua maoni
ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba. Lakini tuligundua kwamba maoni
tuliyopata yalikuwa mengi sana, na pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa,
tulitambua umuhimu wa kuongeza muda hadi mwisho wa mwezi Mei, Maoni ya wananchi
yaligusa mambo yote yanayohusu Katiba na mengi ya maoni hayo yalikinzana.
Aidha, baadhi ya maoni yaligusia masuala ya Kisera, Kisheria na Kiutendaji.
Tulifanya uchambuzi makini na wa ndani wa maoni hayo na kazi hiyo
tumeikamilisha na rasimu imeandaliwa na Tume na leo tupo hapa kwa ajili ya
kuizindua, ambapo Wananchi watapata nafasi ya kuisoma. Kwa leo, kwa niaba ya
Tume, napenda kutaja maeneo machache tu ambayo tunayapendekeza.
2.0. IBARA ZINAZOPENDEKEZWA KWENYE RASIMU YA KATIBA
Ndugu Wananchi,
Katiba yetu ya sasa ina ibara 152. Tume ilifanya jitihada
kubwa sana kuandaa rasimu ambayo siyo ndefu. Lakini katika hali halisi
haikuwezekana. Rasimu ya Katiba tunayopendekeza ina ibara
240.
3.0. MISINGI MIKUU YA TAIFA
Utangulizi wa Katiba ya sasa ndio unaobeba misingi mikuu ya Taifa ambayo
ni Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Tume inaamini kwamba misingi hii ni
mizito na inastahili kubaki kwenye Katiba mpya. Hata hivyo, Tume imeona ni
busara kuongeza misingi mingine mitatu ya Usawa, Umoja na Mshikamano. Hivyo,
Tume imependekeza Katiba iwe na Misingi Mikuu saba ya Taifa;yaani; Uhuru,
Haki,
Udugu, Usawa, Umoja, Amani na Mshikamano.
4.0. TUNU ZA TAIFA
Katiba yetu ya sasa haina sehemu inayoelezea tunu za Taifa (National Values).
Wananchi wengi walitoa maoni kwamba Katiba itaje Tunu za Taifa. Tume
imependekeza Tunu zifuatazo zitajwe ndani ya Katiba. Tunu hizo ni;-
Utu,
Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na Lugha yetu ya taifa ya
Kiswahili.