HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI
NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI
JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO
YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
(Inatolewa chini ya kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013)
A:
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Waziri wa Nishati na Madini ilianzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 21 cha
Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya
Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la
Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment
of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17
Desemba 2010.
Mheshimiwa Spika, Katika
kujadili Mapitio ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2013/2014
naomba tuyatafakari maandiko ya katika muktadha wa uongozi wetu wa leo na hatma
ya sekta hizi mbili muhimu za nishati na madini.
Mheshimiwa Spika,
Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE katika ukurasa wa pili tutafakari kwamba, naomba kumnukuu ‘ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali
mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki. Kwake wote ni sawa. Pia ukweli
unayo tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa.Ukiniona nataka kulipiga teke
jiwe kwa kuwa nafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini
nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi,
nitalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi
kupuuzwapuuzwa.
Mheshimiwa Spika,
Tuendelee kutafakari maandiko ya Nyerere kwamba
‘Wakati mwingine, mtu tunayempinga huwa anamakosa kweli, lakini hoja
tunazozitoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake.Nikisema mbili na
tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine nifikiri
tunazidisha kumbe tunajumlisha.Ni kweli mbili mara tatu ni sita;lakini mbili na
tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo
yangu na kukubali yako kwa kusema kuwa meno yangu ni machafu ,au natoa kamasi
daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana, Huu ni mfano wa upuuzi;
lakini mara nyingi hoja tunazozitumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale
tusiowapenda,au kukubali mawazo yetu, huwa haziuhusiani kabisa na mambo
tunayojadili’.
Mheshimiwa Spika, Tutafakari
maandiko ya Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA uk. 50, nanukuu “Rais
Mwinyi ni mtu mwema na mpole, lakini ni kiongozi dhaifu; au upole wake na
udhaifu wake unatumiwa na watu ambao wala si wema wala wapole kuhatarisha umoja
na amani ya nchi yetu, Kipindi chake cha pili kinakaribia kwisha”.
Mheshimiwa Spika, Tutafakari
maandiko mengine ya Mwalimu Nyerere kwamba “lakini
hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa chama na Serikali. Wala tukiendelea
na hali hii, bila kubadili uongozi wa Chama na Serikali, sina hakika kama
tutafika huko salama.Masuala muhimu ya nchi yetu hayatashughulikiwa.Viongozi
wetu wataendelea na matendo yao ya kuvuruga muungano. Matatizo ya kweli ya
muungano hayatashughulikiwa, maana hatuna serikali ya kuyashughulikia.Na
masuala mengine muhimu ya uchumi, huduma za umma, rushwa,chuki za uzawa na
ukabilana udini yataachwa yajitatue yenyewe.Nasema , katika hili kama hiyo sina
hakika kama tutafika salama;na tukifika “salama”,tukiwa na uongozi huu huu wa
chama na serikali , mbele yetu kutakuwa ni giza tupu.Majuto ni mjukuu, huja
baadaye.Tunaweza tukafikishwa mahali tukilinganisha uongozi wa rais Mwinyi na
wa rais wa kesho tukaona kuwa chini ya Ndugu Mwinyi, Pamoja na udhaifu wake
wote, tulikuwa peponi”!
Mheshimiwa Spika,
Mwalimu Nyerere anaendelea kuandika kwamba “Waingereza wana msemo “Nature abhors vacuum”, “hulka huchukia ombwe” . Hata siasa huchukia
ombwe. Kama uongozi ni mbovu, upo kama haupo au upo kwa masilahi ya wenyewe,
watatokea watu waujaze uwazi uliopo;hauwezi kuachwa wazi hivi hivi.Lakini
uongozi mbovu ni kama mzoga, unatabia ya kukaribisha mafisi na mainzi.
Tusidhani kuwa hulka ya siasa yetu ni tofauti na hulka ya siasa ya watu
wengine; kwamba sisi tunaweza kuvumilia uongozi mbovu na tusivune matunda ya
hulka ya uongozi mbovu”.
Mheshimiwa Spika,
Mwalimu Nyerere alikuwa akiandika wakati wa awamu ya Rais Mwinyi kuhusu masuala
yanayohusu Muungano; sisi tutafakari maandiko haya katika muktadha wa uongozi
wa sasa wa taifa letu na mustakabali wa sekta nyeti kwa uchumi wa nchi na
maisha ya wananchi za nishati na madini.