WAKATI
wabunge sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakianza
kutumikia adhabu ya kutohudhuria vikao vitano vya Bunge la Bajeti
vinavyoendelea mjini hapa, utata mkubwa umeibuka juu ya kanuni
alizotumia Naibu Spika, Job Ndugai, kutoa adhabu hiyo.
Utata huo
ulibainika jana wakati Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman
Mbowe, alipoomba mwongozo wa Spika Anna Makinda, kutaka kujua kanuni
aliyotumia Ndugai wakati hakuna kanuni iliyomruhusu kutoa adhabu hiyo.
Baadhi ya wabunge pia walihoji kifungu kilichotumika hata kama wabunge hao walikosea.
Miongoni mwa
waliohoji adhabu hiyo, wapo baadhi ya wabunge wa CCM ambao hawakupenda
kutaja majina yao, wakisema kuwa uamuzi wa Naibu Spika ulitawaliwa na
jazba za kibinadamu badala ya kufuata kanuni zinazoliongoza Bunge.
Katika
mwongozo wake jana kwa Spika Makinda, kiongozi huyo wa kambi ya upinzani
alihoji kifungu kilichotumika kuwaadhibu wabunge wake.
Mbowe
alisema juzi wakati Bunge lilipokuwa katika kipindi chake cha jioni,
wabunge sita wa CHADEMA waliotolewa nje kwa maelekezo ya Naibu Spika,
Job Ndugai.
Aliwataja
wabunge waliotolewa kuwa ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Haghness
Kiwia (Ilemela), Ezekia Wenje (Nyamagana), Godbless Lema (Arusha Mjini),
Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Pete Msingwa (Iringa Mjini).
“Na wabunge
hawa walipotolewa, walipewa vile vile adhabu ya kutohudhuria vikao
vitano vya Bunge, adhabu iliyotolewa papo kwa papo na Naibu Spika.
“Kwa mujibu
wa kanuni zetu, kanuni inayompa Naibu Spika au Spika mamlaka ya kumtoa
mbunge kwa siku tano ni kanuni ya 73 ya kanuni ndogo ya tatu ambayo
inahusu mbunge ambaye atashindwa kutoa vielelezo vya aidha kusema uongo
ambayo inasema hivi: “Endapo mbunge yeyote atatakiwa kuthibitisha maneno
aliyoyasema na hadi kufikia mwisho wa muda aliopewa, ameshindwa kutoa
uthibitisho huo, Spika anaweza kumsimamisha mbunge huyo asihudhurie
vikao vya Bunge visivyozidi vitano,” alinukuu.
Mbowe ambaye
pia ni mwenyekiti wa CHADEMA, alisema yaliyotokea bungeni juzi ni
sintofahamu kati ya wabunge na kiti cha Spika ambapo katika mambo ya
msingi CHADEMA ilitegemea kifungu cha nne cha kanuni za Bunge, kifungu
kidogo cha kwanza kingetumika.
Kifungu
kinasema: “Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau mamlaka
ya Spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Haki na Maadili ya
Bunge.
“Ikiwa kwa
maneno au vitendo, mbunge huyo anaonyesha dharau kwa Spika au atafanya
kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au mbunge
yeyote anayeongoza shughuli hiyo.”
Kutokana na
kanuni hiyo, Mbowe aliomba mwongozo wa Spika kutaka kujua wabunge
hao walitolewa kwa kanuni gani na ni lini wataweza kurejeshewa haki yao
ya kurejea ndani ya Bunge.
Vituko vya juzi
Baadhi ya
askari walioamriwa kuingia ndani ya Bunge, walisema hawakuwa tayari
kumtoa Lissu kwa nguvu ndio maana walitumia muda mrefu kutimiza agizo
hilo.
Askari hao
walisema hofu yao ilikuwa ni usalama wa Waziri Mkuu kwani endapo vurugu
zingeibuka, angekuwa katika wakati mgumu kiusalama.
Baada ya
Lissu na wabunge wenzake kutoka nje ya ukumbi chini ya ulinzi, askari
hao walipata wakati mgumu kuwatoa nje ya eneo la Bunge.
“Tulipanda
juu hadi kwenye ofisi ya Lissu, alipofika alikaa chini, akafungua
kompyuta yake, baadaye akaizima wala hakuwa na haraka na sisi wakati huo
tulibaki tumesimama tu.
“Baadaye
aliizima, akachomoa waya na kuziingiza kwenye begi lake, kisha
alisimama taratibu na kuondoka kama vile hakuna jambo lililotokea,”
alisema askari huyo.
Wenyewe wanena
Lema
alisema: “Nimepokea kwa furaha adhabu hii kwa sababu imetokana na
kupigania haki na ukweli ndani ya Bunge. Kwa hiyo adhabu hii kwangu ni
baraka.”
Alisema
uonevu wa wazi uliofanywa na Naibu Spika, Job Ndugai, baada ya muda
kidogo Tanzania itashangilia ushindi mkubwa. Kwamba Watanzania
watafurahia vijana wao na watoto wao walioshinda hofu.
“Ushahidi
nilioombwa kuhusu mwenyekiti wa CCM kuwa mwasisi wa udini ninao, tena wa
uhakika wa nguvu na imara na niko tayari kuutoa mbele ya Bunge kwa kuwa
nilitoa maneno hayo mbele ya Bunge.
“Sitapeleka
tena ushahidi wangu vichochoroni kwa kuwa nilipeleka ushahidi wangu kwa
Spika kuhusu uongo wa Waziri Mkuu, walipiga chenga hadi wakanivua
ubunge,” alisema.
Lema alidai
kuwa ametumiwa meseji za vitisho kwamba wangelimuonyesha tena
mahakamani, lakini akasema wafanye wafanyavyo ila moyo wake una furaha
kuwa amesema yale ambayo wengine wameogopa kuyasema.
Mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, alisema: “Bunge letu lina matatizo, halina
mwelekeo. Job Ndugai anajidai yeye ndiye kiongozi wa serikali.”
Alisema kama Ndugai ana sifa hizo na anajiandaa kuwa Spika wa Bunge lijalo, anamwomba Mungu asiwe mbunge katika Bunge hilo.
“Tusi
lililotolewa na Peter Serukamba wa CCM, lilikuwa kubwa kuliko matusi
yote yaliyowahi kutolewa ndani ya Bunge katika mabunge ya Jumuiya ya
Madola.
“Hili
lilihitaji adhabu, lakini kitendo cha Naibu Spika kumtimua Lissu ambaye
alikuwa anafuata kanuni ni cha kusikitisha sana,” alisema.
Mbilinyi alisema wananchi wa Mbeya Mjini hawakumtuma kushangilia bungeni.
Kwa upande
wake Mchungaji Msigwa alisema: “Adhabu hii ni ya hovyo kwa sababu
haikufuata taratibu; wamegeuza Bunge kama sehemu ya serikali.”
Alifafanua kuwa kama angepata adhabu iliyofuata kanuni asingekuwa na shida, angeipokea kwa furaha.
“Naibu Spika
ana jazba, anapaswa apate mafunzo ya jazba zake. Viongozi wa Bunge
wamejaa u-CCM zaidi kuliko utaifa. Binafsi sitajali kufukuzwa,
ninachotaka haki itendeke,” alisema.
Mbunge wa Ilemela, Kiwia, alisema adhabu waliyopewa ni kinyume cha kanuni.
“Adhabu hiyo
anapaswa apewe mtu aliyesema uongo na kushindwa kuthibitishwa, pamoja
na hayo kanuni zifanye kazi kwa wabunge kwa usawa,” alisema.
Kiwia
aliongeza kuwa kanuni hazipaswi kuwaona wabunge wengine wana haki na
wengine hawana; kwamba hoja za msingi zijibiwe, maamuzi bungeni
yasifanyike kwa mabavu.
Naye Lissu ambaye ni mwanasheria kitaaaluma, alisema hajui ni kanuni gani iliyotumika na kumwadhibu na kwa kosa gani.
Chanzo, mtando wa kijamii wa CHADEMA