|
Mwenyekiti wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni Mh.Freeman Mbowe. |
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitajitoa
katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo muhimu mawili hayatapatiwa
ufumbuzi hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu.
Wakati Chadema wakisema hayo, Jukwaa la Katiba
Tanzania (Jukata), limesema uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
uliomalizika siku tatu zilizopita katika maeneo mbalimbali nchini
haukuwa huru na ni batili, huku likipendekeza urudiwe katika maeneo yote
yaliyokumbwa na kasoro.
Katika hoja zake, Chadema kimesema kinataka
kufutwa kwa uteuzi/uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba
uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata na badala yake wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa
Kata husika bila kuchujwa na Kamati za Maendeleo za Kata (WDC).
Msimamo huo ulitolewa na Msemaji Mkuu wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati akisoma hotuba yake ya
makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/14 huku akiitaka
Serikali kuwasilisha muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ili
maeneo kadhaa yafanyiwe marekebisho.
“Katika Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Katiba tunataka marekebisho ya vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi
katika Bunge Maalumu la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Pia vifungu
vyote vinavyohusu ushiriki wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka
Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya Muungano.”
Jukwaa la Katiba
Kwa upande wake, Jukwaa la
Katiba limesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kubadili
mwenendo wake kuanzia katika utaratibu wa kuwapata wajumbe hao hadi
uundwaji wa Bunge la Katiba na wananchi kupiga kura za maoni. Limesema
isiporekebisha utaratibu huo, litakwenda mahakamani kusitisha mchakato
mzima wa Katiba.
Kumalizika kwa uchaguzi huo kunaashiria kuanza
kwa mabaraza ya Katiba Mei mwaka huu, ambayo yatakuwa yakijadili rasimu
ya Katiba ambayo imetokana na maoni mbalimbali yaliyotolewa na
wananchi.
Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba alisema
uchaguzi huo ulikuwa na kasoro zaidi ya 15, ambazo ni itikadi za vyama
na udini, rushwa, uchakachuaji, upendeleo, ubaguzi wa makundi ya watu
wenye ulemavu na kukosekana kwa mwongozo timilifu wa uchaguzi huo.
Baadhi ya mikoa iliyokumbwa na kasoro hizo ni
Dar es Salaam, Arusha, Mara, Singida na Dodoma. “Pia kulikuwa na vurugu
katika uchaguzi huu, kukataliwa kwa barua za maombi za baadhi ya
waombaji, kutokuwa na tarehe rasmi ya uchaguzi, uandikishaji bandia wa
wapigakura, kukosekana kwa orodha ya majina ya wagombea katika mitaa na
vijiji.”
Habari na Mwananchi