Friday, December 12, 2014

MIKOA IHAMASISHE UWEKEZAJI WA VIWANDA.

Kaimu Meneja Utawala Bw. Atanas William  wa Kiwanda Cha Mafuta (Jielong Holdings) akitoa maelezo kwa timu ya ukaguzi jinsi mafuta yanavyofungashwa katika ndoo tayari kwa kwenda sokoni. Kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha lita za mafuta milioni 2.4 kwa mwezi.

Na Oyuke Phostine - Shinyanga
Serikali imetoa wito kwa Ofisi za wakuu wa mikoa kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda kwenye mikoa yao ili kuweza kukuza uchumi wa mikoa husika na taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Bw. Paul Sangawe, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, anayeshughulikia Biashara za Kimataifa wakati akiongoza timu ya wataalam kutoka ofisi hiyo iliyokuwa  ikifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali na sekta binafsi katika mikoa ya Shinyanga, Mara, Simiyu, na Mwanza.

Bw. Sangawe, alisema kuwa Wajibu wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza.  Alifafanua kuwa, moja ya vipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao utekelezaji wake unaishia 2015/16, ni miundombinu ili kufungulia fursa za ukuaji wa uchumi.

Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaofuata kuanzia 2016/17 utalenga katika kuendeleza viwanda.  Hivyo, alitoa rai kwa viongozi katika ngazi za mikoa kuratibu masuala ya uwekezaji hususan katika viwanda ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa uwekezaji huo unawanufaisha wananchi wa maeneo husika kwa kuongeza fursa za ajira na masoko ya bidhaa za kilimo.

“Uwepo wa viwanda hivi unaonyesha mwenendo na mwelekeo mzuri wa taifa katika kufungua fursa za maendeleo na kiuchumi kupitia sekta ya viwanda, hivyo basi iwapo jitihada za kuhamasisha uwekezaji wa viwanda katika kila mkoa zitatiliwa maanani ni dhahiri kuwa fursa za ajira zitaongezeka na kasi ya ukuaji uchumi itaongezeka” alisema Bw. Sangawe.

Akizungumza na timu hiyo ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ilipotembelea na kukagua kiwanda cha kusindika mafuta kwa kutumia alizeti na mbegu za pamba cha Jielong Holdings Mkoani Shinyanga, Kaimu Meneja Utawala Bw. Atanas William alisema kuwa mpaka sasa kiwanda hicho kinaweza kusindika na kuhifadhi lita milioni 2.4 kwa mwezi.  

“Kwa sasa upatikanaji wa mali ghafi ni wakuridhisha kwa sababu bado tunanunua alizeti kutoka kwa wakulima, na mbegu za pamba katika vinu vya kuchambua pamba (Ginneries). Tuna mpango wa kuhamasisha na kuwafundisha wakulima njia bora za kilimo na utunzaji wa mazao ili kujihakikishia upatikanaji wa mali ghafi yenye ubora zaidi” alisema Bw. Atanas.

Viwanda vingine vilivyotembelewa ni kiwanda cha Dahong kinachotengeneza nyuzi za pamba na kiwanda cha Xinghua cha kusindika ngozi mkoani Shinyanga na kiwanda cha nguo cha Mwatex Mkoani Mwanza. Kiwanda cha Dahong kina uwezo wa kununua tani 12,000 za pamba kwa mwaka na kuzalisha tani 7 za nyuzi za pamba kwa siku. Kiwanda hiki kimeanza uzalishaji mwezi Septemba 2014, na nyuzi zote zinazozalishwa zitauzwa nchini China.

Kwa mujibu wa bwana Luke Li, ambaye ni afisa fedha wa kiwanda hicho, mipango ya baadae ya kiwanda hicho ni kutengeneza nguo.  Bwana Li pia alisema kuwa kuna mpango wa kujenga kinu cha kuchambua pamba na kutoa mafunzo kwa wakulima ili kuwezesha upatikanaji wa pamba yenye ubora unaotakiwa.

Kwa upande wake, Meneja wa kiwanda cha Xinghua, Bw. Wang, alisema kuwa usindikaji wa ngozi  unasuasua kutokana na upatikanaji hafifu wa malighafi. Wafugaji wanapowekea alama mifugo na kutoboa ngozi wakati wa kuchinja, wanaathiri sana ubora wa ngozi alisema meneja huyo. Katika kukabiliana na changamoto hii, mwekezaji huyo ana mpango wa kujenga machinjio ya kisasa ambayo pia itahusisha usindikaji wa nyama. 

Aidha Bw. Sangawe alitoa rai kwa viongozi wa mikoa inayotoa ngozi kwa wingi kuongeza jitihada za kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa ubora wa ngozi ili kuhakikisha ngozi inayopatikana Tanzania inakuwa na thamani ya hali ya juu.

Afisa fedha wa Kiwanda cha nguo Dahong Bw. Luke Li  akiwaonyesha  Bw. Erasmus Masumbuko na Bi. Angela Shayo (wachumi kutoka Tume ya Mipango) ubora wa nyuzi za pamba zinazotengenezwa na kiwanda chake.

Kaimu Meneja Utawala Bw. Atanas William  wa Kiwanda Cha Mafuta (Jielong Holdings) akimwonyesha Bw. Paul Sangawe, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, shehena ya mbegu za pamba zinazotumika na kiwanda katika usindikaji wa mafuta.

Wakaguzi wa Miradi kutoka Ofisi ya Raisi, Tume ya Mipango wakiwa na Kaimu Meneja Utawala Bw. Atanas William  wa Kiwanda Cha Mafuta (Jielong Holdings) wakiangalia jinsi mitambo inavyomimina mafuta katika ndoo tayari kwa kwenda sokoni.

Meneja wa Kiwanda Cha Ngozi Bw. Wang (aliyeinama) akiwaonyesha wakaguzi wa miradi kutoka Ofisi ya Rais Tume ya Mipango ngozi za mbuzi zilizochakatwa . Kiwanda hiki kina uwezo wa kuchakata ngozi 10,000 za mbuzi na 2,000 za ng’ombe kwa siku.

Meneja wa Kiwanda Cha Ngozi Bw. Wang (Kulia) akitoa maelezo kuhusu uandaaji ngozi kabla ya kwenda sokoni.  Kiwanda hiki kina uwezo wa kuchakata ngozi 10,000 za mbuzi na 2,000 za ng’ombe kwa siku. Wengine katika picha kutoka kulia ni Bw. Paul Sangawe, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia Biashara za Kimataifa na Bw. Erasmus Masumbuko, Mchumi Tume ya Mipango.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...