Wednesday, March 6, 2013

WATAALAMU WA AFYA NCHINI SASA KUWASILIANA BURE

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika juhudi zake za kuboresha afya za wananchi imeanzisha mfumo mpya wa mawasilano kama taarifa ilivyotolewa kwenye vyombo vya habari.
 


Madaktari na wataalamu wengine wa afya kuanzia sasa wataanza kupata huduma ya kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi bila malipo yoyote kwa wataalamu wenzao popote nchini na kupokea taarifa, maelekezo na ushauri unaohitajika kupitia mtandao wa mawasiliano ya simu za mkononi wa Vodacom pekee.


Health Network Programme hii imeanzishwa mahsusi kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wa madaktari na kuboresha kiwango cha mawasiliano ya wao kwa wao, na kwamba usajili wa mtandao huo kuanzia sasa unatarajia kuhusisha wataalamu wa afya wapatao 9,000 nchi nzima, wakiwemo madaktari, madaktari wa meno, madaktari wasaidizi, madaktari wasaidizi wa meno, tabibu na tabibu wasaidizi kukote waliko, serikalini na wale wa binafsi.

Aidha ili daktari aweze kujiunga kwenye programu hiyo atahitajika kutumia simu yake ambayo itakuwa na kadi ya simu (simcard) ya Vodacom na kisha kupiga *149*24# na baadaye kupata maelekezo ya namna ya kujisajili.

Mbali ya kupiga simu bure wanachama wa mtandao huo kwa kushiriki katika programu hiyo watakuwa na uwezo wa kutuma ujumbe mfupi ‘sms’ 50 bure kila mwezi kuwasiliana na wenzao waliojisajili ndani ya programu.

Mpango huo utakwenda mbali zaidi na kupanua wigo wa fursa kwa sekta hiyo katika kukabiliana na changamoto zake kwa haraka ili kukidhi matakwa ya Watanzania walio wengi.

Switchboard kwa utaratibu kama huu pia imefaulu kuwaunganisha karibu madaktari wote wa nchi za Ghana na Liberia, na kwamba zaidi ya simu milioni 4 zimepigwa kutoka mwaka 2008 hadi sasa ambapo madaktari wamekuwa wakisaidiana katika kuboresha huduma stahiki anazohitaji mgonjwa.

Kwa sasa madaktari karibu wote wa nchi hizo ni sehemu ya Mtandao wa Afya unaowawezesha kupata huduma za bure za mawasiliano sambamba na wao kwa wao kushirikiana na kusaidiana kitaalamu katika kila pembe ya nchi hizo kwa manufaa yao na wagonjwa.

Programu hiyo inadhaminiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Switchboard na Kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom.

Kwa wale watakaojisajili wanaombwa kutoa kibali kwa Timu ya Tafiti ya Mpango huu ya Switchboard yaani Programme Research Team (PRT) na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuweza kutathmini matumizi ya simu zao za mkononi ili kujua imeleta mabadilko kiasi gani katika sekta ya afya kupitia programu hiyo.

PRT na Vodacom hawatavujisha wala kujihusisha na taarifa zako zozote binafsi za mawasiliano kupitia simcard yako na kwamba kushiriki ni hiari yako, na unaweza kujitoa kwenye programu wakati wowote ukihitaji na hautatozwa wala kulipishwa gharama yoyote,”

Kupitia programu hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeiomba Switchboard kuratibu na kuweka mpangilio mzuri wa mchakato wote wa programu husika kwa manufaa ya wataalamu wa afya na ustawi wa tiba nchini.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...