HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/14
I. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, hakuna
ubishi kwamba ardhi ndio msingi mkuu wa uchumu wa taifa lolote, na kwa maana
hiyo ardhi ni msingi maisha ya mwanadamu.
Ardhi ni miongoni mwa vitu vikuu vine vinavyohitajika ili taifa
liendelee. Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere aliwashi kusema “Ili taifa
liendelee linahitaji watu, ardhi, siasa
safi na uongozi bora”
Mheshimiwa Spika,
nimekuwa nikijiuliza kuhusu chimbuko la umasikini uliokithiri Tanzania kwa
kuzingatia vigezo vya maendeleo alivyotoa Hayati Mwalimu Nyerere. Baada ya kufanya marejeo ya machapisho
mbalimbali lakini pia baada yakupata uzoefu wa uongozi kama Mbunge wa Wananchi
na hasa kama Waziri Kivuli kwa Arhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na kwa
kuzingatia mwenendo halisi wa watawala hapa Tanzania nimegundua kuwa kiwazo
kikubwa kwa maendeleo ya nchi yetu sio watu (watu wapo wengi sana takribani
milioni 45), tatizo sio ardhi (hiyo ipo ya kutosha na ziada takribani hekta
milioni 94.3[1]).
Mheshimiwa Spika,
tatizo ni “siasa safi na uongozi bora”. Tofauti na Kauli Mbiu
mkakati za kisiasa enzi za Mwalimu, kwamba Sisa ni kilimo, Uhuru na Kazi, Kilimo cha Kufa na Kupona,
sasa hivi tunashuhudia siasa za watawala za kuongeza umasikini wan chi hii “kwa
ari na kasi zaidi, tunashuhudia watawala wakijigamba kwamba “wamethubutu
na wameweza” kuwa mafisadi wa rasilimali za nchi hii.
Mheshimiwa Spika,
maneno niliyoyatumia hivi punde hayanifurahishi hata kidogo, lakini
nimelazimika kuyasema kwa kuwa sioni watawala wa nchi hii wakifikiri namna ya
kumkomboa mtanzania kutoka kwenye wimbi la umasikini, bali kila mmoja
anajitahidi kujilimbikizia mali hasa kwa hofu ya kuondolewa madarakani (akakosa
namna ya kuishi) kutokana na kuenea kwa kasi na kuungwa mkono kwa wingi na
wananchi kwa chama kikuu cha upinzani nchini cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA).
Mheshimiwa Spika,
nasikitika sana kwamba badala ya Serikali ya CCM kutumia muda na rasilimali
ilizo nazo kutatua matatizo sugu ya kiuchumi ya taifa hili (hususan uporaji wa
ardhi ya wananchi), inatumia fedha nyingi za umma kupambana na CHADEMA ambayo
inatetea maslahi ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Nchii hii ina rasilimali nyingi sana ikiwemo
ardhi ambazo zingeweza kuifanya Tanzania
kuwa miongoni mwa nchi za ulimwengu wa pili kiuchumi, lakini tuna tatizo la uhaba wa viongozi wenye “ufahamu, maadili na busara” ya kutumia rasilimali
hizi kwa maslahi ya taifa.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na ombwe la uongozi katika taifa hili, na kutokana na “ubinafsi,
ulafi na ufisadi” wa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali
za nchi yetu, leo taifa hili ni masikini, miaka hamsini na mbili baada ya
uhuru.
Mhshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA imekuwa ikibainisha mapungufu
na kasoro nyingi katika masuala ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tangu
mwaka 2011 hadi leo, lakini Serikali hii ya CCM imeendelea kuwa na shingo ngumu
kuyafanyia kazi mapendekezo ya Kambi ya Upinzani jambo ambalo linaendelea
kusababisha migogoro mingi na ufisadi katika umiliki na matumizi ya ardhi hapa
nchini
Mheshimiwa Spika,
katika hotuba ya msemaji mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika bajeti ya
wizara hii kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilianisha matatizo makubwa ya ardhi
nyumba na maendeleo ya makazi na kuitaka Serikali kutafuta ufumbuzi kwa kuchukua
hatua za haraka. Matatizo hayo yalikuwa kama ifuatavyo:-
1.
Uporaji wa ardhi ya Tanzania unaofanywa chini ya
usimamizi wa Serikali kwa mbinu au hila ya uwekezaji,
2.
Ufisadi wa ardhi unaofanywa na viongozi wa Serikali na
Chama cha Mapinduzi kwa kuuziana ardhi
kwa bei ya kutupwa,
3.
Ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka
1999 na Sheria namba 5 ya ardhi ya vijiji ambapo viongozi wa Serikali walikuwa
wakigawa ardhiki holela bila kuzingatia matakwa ya sheria hizo,
4.
Migogoro mikubwa ya ardhi baina ya wakulima na
wafugaji ambayo kwa nyakati tofauti imepelekea umwagaji wa damu miongoni mwa
wananchi,
5.
Matatizo makubwa katika tathmini ya malipo ya fidia
kwa wananchi wanaotakiwa kuondoka katika maeneo yao kupisha matumizi mapya ya
ardhi,
6.
Kuendelea kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi jambo
ambalo limesababisha wananchi kuendelea kuishi katika makazi duni na hivyo
kuhatarisha usalama wao na kutweza utu wao,
7.
Serikali na
taasisi zake kutolipa kodi za pango kwa wakati kwa Shrika la Nyumba la Taifa na
hivyo kulirudhisha nyuma kimaendeleo, na
8.
Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba bora na Vifaa vya
Ujenzi kushindwa kuleta mabadiliko
kutokana na kuongezeka kwa nyumba zisizo bora ( kama vile nyumba za tembe, tope
na nyasi) na kuongezeka kwa bei ya vifaa vya ujenzi