|
Mh.Faith Mitambo Mbunge wa Liwale (CCM) |
Takriban nyumba 20 zimeteketezwa katika maandamano
yaliyofanywa na wakulima wa Korosho pamoja na waandamanaji wengine
Kusini mwa Tanzania.Hii ni kwa mujibu wa mbunge mmoja wa eneo hilo.
Mbunge huyo, Faith Mitambo alisema
kuwa majengo mawili nyumbani kwake mjini Liwale, yalichomwa na kuwa
nyumba zingine mali ya baadhi ya wanachama wa chama tawala CCM
ziliteketezwa.
Uharibifu huo ulianza baada ya wakulima kulipwa
kiasi kidogo cha pesa ikilinganishwa na zile walizokuwa wamekubaliana
kulipwa na serikali baada ya kuiuzia mazao yao mwaka jana.
Polisi zaidi wamepelekwa katika eneo hilo kuzuia ghasia zaidi.
Bi Mitambo, aliyekuwa mjini, Dodoma, wakati huo aliambia BBC kuwa alikuwa anazuru eneo bunge lake kudadisi hali ilivyo.
Alipokea habari kuwa waandamanaji waliokuwa
wanajumuisha vijana , walianza kufanya fujo vijijini mnamo Jumanne
asubuhi hadi walipofika mjini Liwale saa za jioni.
Mkaazi mmoja wa mji huo aliambia BBC kuwa mnamo
Jumatano kulikuwa na hali ya wasiwasi mjini humo na kwamba polisi
walikuwa wamewarushia gesi ya kutoa machozi wandamanaji ili kuwatawanya.
Maelfu ya wakulima wadogo wadogo wanaopanda
Korosho nchini Tanzania na ambao huvuna mazao yao mwezi Oktoba, huyauza
kwa mashirika mbali mbali kwa bei waliyokubaliana.
Mwandishi wa BBC mjini Dar es Salaam, Erick
Nampesya anasema kuwa wakulima walikubaliana kulipwa shilingi 1,200 pesa
za Tanzania kwa kila kilo ya korosho hizo.
Mwishoni mwa mwaka jana, wakulima walilipwa sehemu ya deni lao.
Lakini pale waakilishi kutoka kwa mashirika
walipokwenda katika wilaya ya Liwale, kuwalipa sehemu ya mwisho ya deni
lao, wakawa wamebadilisha makubaliano waliyokuwa wameafikiana.
Wakulima walilipwa nusu au chini ya nusu ya deni
lililokuwa limesalia, baada ya kuambiwa kuwa bei ya Korosho ilikuwa
imeshuka sana katika soko la kimataifa.
Wanasiasa wakuu ambao wakulima hao wanawalaumu kwa kukosa kuwasaidia ndio walikuwa wamewaelekezea ghadbabu zao
Wakulima wamekuwa wakilalamika kuhusu msukosuko wa bei za Korosho ambayo huathiriwa zaidi kulingana na msimu.
CHANZO : BBC