HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE . EZEKIAH
DIBOGO WENJE (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA
2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA AFRIKA
MASHARIKI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Jumuiya ya Afrika Mashariki imeundwa na Ibara ya 2(1) ya Mkataba
wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kufuatia makubaliano ya wakuu
wa nchi
wanachama wa jumuiya hiyo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na
Burundi.
Aidha Ibara ya 8(3) (a) ya Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki imezipa mamlaka
nchi wanachama kuanzisha Wizara mahsusi, itakayoshughulikia masuala ya
Afrika
Mashariki. Kwa mujibu wa ibara hiyo, Tanzania, ilianzisha Wizara ya
Afrika Mashariki ambayo majukumu yake ni pamoja utekelezaji wa Mkataba
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mikataba Midogo (Protocols) Umoja wa
Forodha, Soko la Pamoja la Afrika
Mashariki na Mazungumzo ya uundwaji wa
Shirikisho la kisiasa la Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika, ni mategemeo ya Watanzania kwamba, Wizara hii ya Afrika Mashariki
italitendea haki taifa hili, kwa kuwashirikisha wananchi kwenye kila hatua na kwa
kusimamia kwa dhati na kikamilifu michakato yote ya mtangamano wa Afrika
Mashariki, kwa maslahi ya nchi yetu, ili kuhakikisha kwamba Tanzania inanufaika
vilivyo na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kipindi hiki itajielekeza kwenye mambo
machache ambayo tunaamini yakizingatiwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa
imara, na nchi zote wanachama watafurahia matunda ya jumuiya hiyo.
2.0 MADAI YA MAFAO
YA WASTAAFU WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI ILIYOVUNJIKA 1977
Mheshimiwa Spika, madai ya mafao ya wazee wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki sasa ni aibu kwa Taifa. Wastaafu hawa wameyumbishwa kiasi cha
kutosha, wamepuuzwa kiasi cha kutosha, wamedhalilishwa kiasi cha kutosha na
wameonewa kiasi cha kutosha na serikali hii ya CCM inayojiita sikivu. Hakika
laana ya wastaafu hawa wanaodhulumiwa haki yao wazi wazi namna hii itaendelea kulitafuna taifa hili kwa kwa miaka
mingi ijayo kama Serikali haitawatendea haki.
Mheshimiwa Spika, Baada ya Jumuiya hiyo kuvunjika ghafla tarehe 30 Juni, 1977
ulizuka mgogoro wa mgawanyo wa mali na madeni yake. Ili kuumaliza mgogoro huo,
Umoja wa Mataifa uliiteua Benki ya Dunia kusuluhisha mgogoro huo. Benki ya
dunia ilimteua mtaalamu wake, mwanadiplomasia, Dkt. Umbricht (sasa marehemu) ambaye alifanikisha kuwanzishwa kwa
Mkataba wa Kimataifa uliojulikana kama “East African Community Mediation Agreement
1984” kuhusu mgawanyo wa mali na madeni ya Jumuiya yakiwemo mafao ya
wafanyakazi wa Jumuiya hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, kazi kubwa aliyofanya
msuluhishi, Dkt. Umbritch ilikuwa ni kuzigawanya fedha za pensheni na provident
funds za Jumuiya kwa nchi tatu wanachama yaani Kenya, Uganda na Tanzania
kulingana na idadi ya raia wake katika Jumuiya, kwa madhumuni ya kuwalipa mafao
raia wake. Katika mgawo huo, Tanzania ilikabidhiwa paundi za Uingereza milioni
14 kwa ajili ya kulipa mafao ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza bunge hili na
wananchi wote fedha hizo zilitumika kufanyia nini kama walengwa hawakulipwa
mafao yao?
Mheshimiwa Spika, nchi za Kenya na Uganda tayari zilishawalipa wastaafu wa Afrika
ya Mashariki stahili zao na hali huko ni shwari, lakini kwa Tanzania jambo hili
limegubikwa na wingu zito la ufisadi kwa kuwa fedha ya kuwalipa wastaafu hao
ilishatolewa. Kwanini wastaafu hao hawakulipwa, na wale waliolipwa, walipewa
cheki za silingi 10 na shilingi 130 za kitanzania jambo ambalo ni aibu na
fedheha kwa Serikali hii ya CCM inayojiita sikivu kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali hii ya CCM inayojiita
sikivu, kutoa tamko leo, mbele ya bunge
hili kuhusu mafao ya wastaafu hao ili wajue moja: kama wanalipwa au hawalipwi. Kama Serikali haitatoa tamko leo, kuhusu unyanyasaji wanaofanyiwa wastaafu wa
Afrika Mashariki, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuleta hoja
binafsi bungeni kwa hatua za kibunge kuhusu mafao ya wastaafu wa iliyokuwa
Afrika Mashariki.