Friday, October 24, 2014

Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda wakamilika

Timu ya ukaguzi ikitazama barabara ya kutua na kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa Mpanda.
Na Mwandishi wetu, Mpanda
Serikali imekamilisha ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mpanda, mkoa wa Katavi na hivyo kuufanya uwe wa kiwango kizuri tayari kwa kutumika kwa ndege za binafsi na biashara.
Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Bw Seneti Lyatuu alisema uwanja huo umeboreshwa na hivyo, unaweza kutumika kutua na kuruka ndege za kiwango cha kati na hata zile ndege kubwa zinaweza kutua kwa dharura.
Aliiambia timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango iliyotembelea uwanja huo mwishoni mwa wiki kuwa uwanja huo umeongeza idadi ya wasafiri mara dufu kutokana na ukarabati na upanuzi uliofanyika.
Meneja wa Uwanja huo alisema idadi ya abiria imeongezeka kutoka abiria 285 mwaka 2009 hadi 2,390 mwaka 2013/14.
Bw. Lyatuu alisema kuwa uwanja huo umekarabatiwa na barabara ya kuruka na kutua ndege imerefushwa kwa kiwango cha lami kutoka urefu wa mita 1,500 na upana wa mita 30 hadi kufikia urefu wa mita 1,820 na upana wa mita 30.
Alisema maeneo mengine yaliyokarabatiwa ni pamoja na kujenga uzio na mifereji ya kupitishia maji ya mvua.
“Kwa sasa kiwanja kipo vizuri na ndege za aina zote zinaweza kutua hapa uwanjani hivyo, tunawakaribishwa wadau wote kuutumia uwanja huu” alisema Bw Lyatuu.
Eng. Caroline Mntambo kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Makao Makuu Dar es Salaam alisema kuwa tayari wamealika mashirika ya ndege yanayofanya biashara hapa nchini kuanzisha safari katika uwanja huo. Mashirika hayo ni pamoja na ATC, Precision Air, Fast jet   nk.
Eng Mntambo alisema kwa sasa shirika la ndege la Auric Air tayari limeanzisha safari za kwenda Mpanda ambapo linasafirisha abiria kutoka Dar- Mpanda – Mwanza mara tatu kwa wiki.
Alisema ndege zingine zinazotua uwanjani hapo kwa sasa ni pamoja na za UNHCR, ndege za kukodi na ndege za serikali.

PICHA NA JOYCE MKINGA




No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...