Thursday, September 25, 2014

Wafuasi wa Boko Haram wajisalimisha.

Jeshi nchini Nigeria limesema zaidi ya wafuasi 260 wa Boko Haram wamejisalimisha Kaskazini mwa nchi hiyo.
Jeshi hilo limesema katika mapambano limemuua mtu mmoja ambaye huwa anaonekana kwenye picha za video za propaganda za Boko haram akijidai kuwa Kiongozi wa wa kundi hilo, Abubakar Shekau.
Jeshi lilisema kuwa wapiganaji 135 walijisalimisha wakiwa na silaha zao katika eneo la Biu , jimbo la Borno siku ya Jumanne. Liliongeza kuwa wengine 133 walijisalimisha Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Hata hivyo mwandishi wa BBC mjini Lagos Will Ross anasema kuwa ni vigumu kuthibitisha madai hayo ya jeshi.
Mwaka jana jeshi lilisema kuwa Shekau huenda aliuawa , lakini halikutoa thibitisho lolote.
Hata hivyo ikiwa ni kweli kuwa wapiganaji hao wamejisalisha basi huenda ni ushindi kwa jeshi la Nigeria katika vita vyake dhidi ya Boko Haram.
Mwandishi wa BBC nchini Nigeria amesema kuwa majuma ya hivi karibuni Boko Haram imeshindwa kwa kiasi kikubwa wakati walipokuwa wakipambana kudhibiti eneo karibu na mji wa Maiduguri ambalo ni ngome yake.
Jeshi limesema wafuasi 135 wa Boko Haram wamejisalimisha wakiwa na silaha zao katika majimbo ya Biu na Borno,halikadhalika wafuasi wengine 133 wanahojiwa.
Kwingineko , Rais wa Nigeria,Goodluck Jonathan amesema kuwa zaidi ya watu 13,000 waliuawa katika miaka mitano ya kwanza ya harakati za Boko Haram nchini humo.
Rais Jonathan alisema hayo katika hotuba yake katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Jumatano.
Rais Jonathan pia alisisitiza kuwa juhudi zinafanywa kuwaokoa wasichana wa Chibok.
CHANZO: BBC

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...