Sekretarieti ya Ajira inapenda kutoa tahadhari kwa waombaji wote wa nafasi za kazi kupitia chombo hiki kuwa kumezuka kundi la watu wanaojifanya ni watumishi wa Sekretarieti ya Ajira ambao kwa makusudi wamekuwa wakiwapigia simu kwa lengo la kuwalaghai baadhi ya waombaji wa nafasi za kazi Serikali wakidai wapewe fedha ili waweze kuwasaidia kupata kazi Serikalini kwa urahisi mara baada ya kufanya usaili.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amefikia hatua ya kutoa tamko hili kutokana na baadhi ya waombaji wa nafasi za kazi Serikalini kukumbwa na kadhia hiyo na kutoa taarifa. Amesema Ofisi yake haina utaratibu wa kuwapigia simu waombaji wa fursa za ajira Serikalini na kuwadai fedha ili kuweza kuwapatia nafasi ya ajira. Hivyo, endapo kuna msailiwa yeyote atakayepigiwa simu ajue hao watu ni matapeli na ni vyema akawapuuza kw akutokuwapa ushirikiano na badala yake kuwaripoti katika vyombo vya dola ili waweze kuwachukulia hatua stahiki.