Wednesday, June 11, 2014

TAARIFA KWA UMMA - KUTOKA UTUMISHI.

Sekretarieti ya Ajira inapenda kutoa tahadhari kwa waombaji wote wa nafasi za kazi kupitia chombo hiki kuwa kumezuka kundi la watu wanaojifanya ni watumishi wa Sekretarieti ya Ajira ambao kwa makusudi wamekuwa wakiwapigia simu kwa lengo la kuwalaghai baadhi ya waombaji wa nafasi za kazi Serikali wakidai wapewe fedha  ili waweze kuwasaidia kupata kazi Serikalini kwa urahisi  mara baada ya kufanya usaili.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amefikia hatua ya kutoa tamko hili kutokana na baadhi ya waombaji wa nafasi za kazi Serikalini kukumbwa na kadhia hiyo na kutoa taarifa. Amesema Ofisi yake haina utaratibu wa kuwapigia simu waombaji wa fursa za ajira Serikalini na kuwadai fedha ili kuweza kuwapatia nafasi ya ajira. Hivyo, endapo kuna msailiwa yeyote atakayepigiwa simu ajue hao watu ni matapeli na ni vyema akawapuuza kw akutokuwapa ushirikiano na badala yake kuwaripoti katika vyombo vya dola ili waweze kuwachukulia hatua stahiki.

Daudi amesema kuwa ni vyema kila mwombaji wa nafasi za kazi Serikalini kutambua kuwa Sekretarieti ya Ajira inaendesha mchakato wa ajira kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu na si vinginevyo. Aidha, ni kosa kosa kwa mtu au Taasisi yeyote ile kutoa ama kupokea rushwa ili katika kutoa huduma au kutekeleza jambo lingine lolote. 

Katibu  anawataka watu wote wanaowapigia waombaji wa fursa za ajira simu na kuwalaghai kuacha kufanya hivyo mara moja na Serikali inaendelea kuyafanyia kazi malalamiko ambayo yamewasilishwa katika ofisi yake na pindi inatakapowabaini wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria za nchi. 

Aliongeza kuwa mtu yeyote anayepata kazi kupitia chombo hiki ajue ameipata kutokana na kuwa na sifa na kutimiza vigezo vyote baada ya kupitia mchakato mzima hadi kupangiwa kituo cha kazi lakini sio kwamba amepata kazi kutokana na rushwa au kumjua mtu, hivyo, hakuna sababu yoyote ya kuhadaika na watu wasiopenda kufanya kazi za halali na badala yake kutumia njia za mkato kujipatia fedha kirahisi bila hata ya kujali madhara anayomsababishia mwingine au yanayoweza kumkuta pindi atakapobainika kufanya hivyo.

Ni vyema wananchi wote wakafahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ndio chombo pekee kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu 29 (1), pamoja na marekebisho yaliyofanyika katika Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 toleo Na. 2 la mwaka 2008 ambapo katika Vifungu Na. 4.6 na 6.6. vya Sera hiyo vimetamka kuwepo kwa chombo maalum cha kushughulikia mchakato wa masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma na si mtu au kikundi cha watu kinachotaka kupotosha uma kwa kujua au kutokujua wanaweza kumpa mwombaji kazi ajira Serikalini kwa njia za mkato. 

Aidha, amewasisitizia wadau wote wa Sekretarieti ya Ajira wanaotafuta kazi pindi wanapopigiwa simu au kuona matangazo yanayohusu ajira Serikalini katika Vyombo mbalimbali vya Habari ambavyo wanamashaka navyo, ikiwemo mitandao ya kijamii wajaribu kujiridhisha kwa kuthibitisha taarifa hizo kama ni za kweli kwa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz kwa taarifa sahihi zihusianazo na ajira katika Utumishi wa Umma au kupiga simu namba 255-687624975 kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 9:30 jioni kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa ili kupata ufafanuzi zaidi.
Amesema, Sekretarieti ya Ajira haiwajibiki na wala haitawajibika kwa mtu au watu watakaopigiwa simu na kutoa fedha kwa matapeli hao kwani ni kosa kutoa au kupokea rushwa kwa mujibu wa Sheria za nchi.

Imetolewa 11 Juni, 2014 na

     Katibu,

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma

Maktaba Kuu ya Taifa/Barabara ya Bibi Titi Mohammedi,
S. L. P 63100, Dar Es Salaam.
Simu; +255 22 2153517, Nukushi; +255 22 2153518
Barua pepe: katibu@ajira.go.tz,  Tovuti; www.ajira.go.tz

Aidha, kwa maelezo zaidi; wasiliana na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
kwa Barua pepe; gcu@ajira.go.tz  au  Simu; 255-687624975

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...