Wasailiwa waliofanya usaili kuanzia tarehe 4 hadi 15 Machi, 2014 kwa kada za Kilimo, Mifugo na Uvuvi wametakiwa kuangalia majina yao katika Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira kwa watakaokuwa wamefaulu usaili huo kuanzia tarehe 28 Aprili, 2014.
Naibu Katibu wa Idara ya Ajira katika Sekretarieti ya Ajira Bw. Lucas Mrumapili amesema hayo leo wakati akiongea na baadhi ya wasailiwa waliomtembelea ofisini kwake ili kujua matokeo ya usaili wa kada za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Sasa hivi kuwapa matokeo yenu hapa siwezi maana kuna taratibu zake ila ninachoweza kuwaeleza ni kwamba mchakato mzima wa usaili huo uko katika hatua za mwisho ambapo hivi sasa tunaandika barua za kuwapangia vituo vya kazi wale waliofaulu usaili kulingana mahitaji ya Waajiri. Hivyo ni vyema nyote mkatembelea tovuti yetu mwishoni mwa mwezi huu tutakuwa tumeshatoa matokeo” alisema Mrumapili.
Alifafanua kuwa ambao hawataona majina yao pindi tangazo litakapowekwa hewani watambue kuwa hawakufaulu usaili husika kwa kiwango kinachotakiwa, hivyo pindi watakapoona matangazo mengine ambayo wanasifa zinazotakiwa wasisite kuwasilisha maombi yao kwa mara nyingine.
Wakati huo huo, Mrumapili amewataka waombaji wa tangazo la kazi la tarehe 22 Januari, 2014 ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 5 Februari, 2014 kuwa usaili wake umeshaanza kwa baadhi ya kada na kwa kada zilizobakia mchakato wa kuwaita waombaji wenye sifa kwa ajili ya usaili unaendela.
Pia amefafanua kuwa kwa waombaji wa tangazo la tarehe 17 Februari, 2014 ambalo mwisho wa kupokea maombi ilikuwa tarehe 3 Machi, 2014 mchakato wake nao uko katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuitwa kwenye usaili.
Naibu Katibu amesema kuwa ofisi yake imefunga kupokea maombi ya kazi kwa tangazo la tarehe 18 Machi, 2014 kwa kuwa mwisho wa kupokea maombi hayo ilikuwa tarehe 3 Aprili, 2014. Aliongeza kuwa kwa tangazo la tarehe 1 Aprili, 2014 ofisi yake bado inaendelea kupokea maombi ya kazi kwa tangazo husika hadi tarehe 15 Aprili, 2014.
Mwisho amewataka waombaji wote wa fursa za ajira Serikalini pindi wanapotuma maombi yao kuzingatia masharti na maelekezo yaliyotolewa katika tangazo husika ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuitwa kwenye usaili.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Ofisi ya Rais-Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
Kwa maelezo zaidi; wasiliana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Kwa barua pepe;
gcu@ajira.go.tz na Facebook-page ya “Sekretarieti Ajira”
au simu 255-687624975
11 Aprili, 2014.