MWENDESHA
Mashitaka wa Serikali (DPP) jana asubuhi aliambulia patupu baada ya
Hakimu wa Mahamaka ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Dodoma, kumwachia huru
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, (CHADEMA) ambaye alimfikisha
kizimbani kujibu tuhuma za kumkashifu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kupitia
mitandao ya kijamii.
Wakili wa Mbilinyi ambaye ni Mwanasheria na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Mb, CHADEMA), aliitaka mahakama ifutilie mbali shitaka alilofunguliwa mteja wake kwa kudai kuwa halina msingi wowote wa kisheria.Baada ya mabishano ya kisheria baina ya Lissu na Mwanasheria wa Serikali kushindwa kuthibitisha kuwa neno, “mpumbavu” ni lugha ya matusi, ndipo Hakimu alipoamua kulifuta shitaka lililowasilishwa kwake na kumwambia DPP akatengeneze upya mashitaka yake kwani aliyoyapeleka yalikuwa na hitilafu kubwa.

Naye Lissu ametaka kesi mpya itakayoletwa mahakamani iwe na maelezo ya Waziri Mkuu na awe tayari kusimama mahakamani kuthibitisha shitaka hilo.
Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Elinaza Luvanda.
Awali akimsomea mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Harriet Lopa alidai kuwa Juni 24, mwaka huu, Mbilinyi akiwa Dodoma alituma ujumbe wenye lugha ya matusi kwa kutumia mtandao wa kijamii wa Facebook kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Mshtakiwa alikana shitaka hilo na Wakili wa Mshtakiwa, Lissu aliomba kutoa hoja na kusema hati ya mashtaka ni mbovu na kuomba Mahakama itupilie mbali kwa sababu ina makosa.
“Lugha ya matusi haikutajwa, lugha gani hiyo ya matusi na hati ya mashtaka iko kimya, mshtakiwa atajitetea vipi,ataandaa utetezi namna gani kwani hata kinachodaiwa kuwekwa kwenye facebook hakijasemwa,” alidai Lissu.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali alisema kesi hiyo bado iko kwenye upelelezi na kutaka mshtakiwa aendelee na mashtaka yake mpaka itakapothibitishwa vinginevyo.
Kutokana na kauli hiyo ya wakili wa Serikali, Lissu alizidi kusisitiza hati ya mashtaka haina maelezo ya kutosha na inatakiwa kukidhi matakwa ya sheria.
“Hati ya mashtaka iliyoletwa si halali kinyume na kifungu cha 132 cha mwenendo wa makosa ya jinai na itakuwa makosa kama Mahakama ikikubali hati hiyo,” alisema.
Alitoa uamuzi wa Mahakama, Hakimu Luvanda alisema anakubaliana na maelezo ya Wakili upande wa utetezi Lissu kuwa hati hiyo ina mapungufu.
Alisema Mahakama inamuachia huru mshtakiwa na upande wa mashtaka unaweza kumshtaki tena mshtakiwa kama itaona umuhimu wa kufanya hivyo.
Akizungumza nje ya Mahakama Lissu alisema hati ya mashtaka dhidi ya Mbilinyi kuwa alitoa lugha ya matusi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda haijaeleza anachodaiwa kusema Mbilinyi.
Alisema Mahakama imetenda sawasawa kuifuta hati hiyo ilitakiwa ifafanue lugha ya matusi iliyotumika ni ipi. ”Hakimu hajasema Sugu hana makosa, lakini upande wa mashtaka ukajipange kutengeneza hati mpya,” alisema.