MH. ROSE KAMILI SUKUM (MB) |
(Inatolewa Chini ya Kanuni ya 99(9)toleo la mwaka 2013)
A.
DHANA YA
KILIMO KWANZA
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu
wa mpango wa serikali katika utekelezaji wa dhana ya kilimo kwanza, serikali
ilijiwekea nguzo kuu kumi katika utekelezaji wa mpango huo, na pia iliweka
ukomo wa utekelezaji wa mpango huo kuwa ni mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, nguzo kuu
kumi za utekelezaji dhana ya kilimo kwanza zilizopitishwa na serikali zilikuwa kama ifuatavyo ;
i.
Dira ya
taifa ya kilimo kwanza : Hii ililenga kuhakikisha kuwa kilimo
cha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa kiwe cha kisasa na cha kibiashara ifikapo
mwaka 2015
ii.
Kugharamia kilimo
kwanza: Hii ililenga kuongeza bajeti ya serikali kwa ajili ya kilimo, kuanzisha
Benki ya Maendeleo ya Kilimo yenye mtaji wa kuanzia dola za kimarekani milioni
500 Desemba 2009, kuanzisha mfuko maalum wa fedha za kilimo kwanza.
iii.
Muundo mpya
wa Taasisi kwa ajili ya usimamizi: Hii ilikuwa ni pamoja na
kuanzisha utaratibu wa uhusiano na wizara nyingine zinazohusiana na maswala ya
kilimo na kuimarisha vyama vya wakulima.
iv.
Mabadiliko
ya mfumo wa kimkakati : Hii ilikuwa ni pamoja na kubainisha maeneo
ya vipaumbele kwa ajili ya vyakula muhimu ili nchi ijitosheleze kwa chakula.
v.
Ardhi kwa
ajili ya kilimo kwanza: Hii ilikuwa ni pamoja na kurekebisha sheria
ya Ardhi ya Vijiji Na 5 ya 1999 ifikapo 2010 ,kuharakisha mfumo wa upatikanaji
ardhi, kuharakisha utatuzi wa migogoro ya ardhi, kutenga ardhi kwa ajili ya
uwekezaji wa kilimo.
vi.
Vivutio kwa
ajili ya kilimo kwanza : Hii ilikuwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vya
masoko kwa mazao ya kilimo, kuimarisha utumiaji wa vipimo na viwango halali
katika biashara na kuboresha bei ya mazao.
vii.
Viwanda kwa
ajili ya kilimo kwanza : Hii ilikuwa ni pamoja na kuanzisha viwanda
kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya wazalishaji wa kilimo,kuongeza uzalishaji
na matumizi ya mbolea,kuboresha uzalishaji wa mbegu na dawa za kilimo,
uzalishaji wa zana na vifaa vya kilimo
viii.
Sayansi,Teknolojia
na rasilimali watu: Hii ilikuwa ni pamoja na kuanzisha bodi ya usajili ya wataalamu
wa kilimo,kulipia mikopo ya gharama zote za masomo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu
vya kilimo,kuanzisha vituo vya hali ya hewa katika ngazi ya kata.
ix.
Miundombinu
kwa ajili ya kilimo kwanza : Hii ilikuwa ni pamoja na kujenga
miradi ya umwagiliaji ya kutosha, kujenga vituo vya masoko kila kata,kupelekea
umeme vijijini kwa ajili ya kuboresha kilimo
x.
Uhamasishaji
wa watanzania kwa ajili ya kilimo : Hii ilikuwa
ni pamoja na kuhamasisha shule na vyuo kushiriki kwenye kampeni ya kilimo
kwanza, viongozi wa ngazi zote kushiriki katika kilimo binafsi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, inataka kupata majibu ya kina juu ya utekelezaji wa nguzo hizi kumi
za kilimo kwanza na hasa ikizingatiwa kuwa huu ni mwaka 2013 na kwa maana hiyo,
imebaki miaka miwili tu ili utekelezaji
wa nguzo hizi uwe umekamilika.
B : BENKI YA KILIMO
Mheshimiwa Spika, ili
kuwezesha shughuli za Kilimo, Serikali ilikuwa na mpango wa kuanzisha Benki ya
Kilimo, ambapo kulikuwa kunahitajika mtaji wa shilingi bilioni 750 kwa ajili ya
kuanzisha benki hiyo. Hata hivyo, mpango huu umekuwa ukisuasua na matokeo yake
benki hiyo imekuja kuanzishwa na mtaji wa shilingi bilioni 60 kinyume na mpango
wa awali wa mtaji wa shilingi bilioni
750.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa majibu ya kina kama fedha hizi
zitatosha kulingana na mpango wa utekelezaji. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inataka kujua kama mtaji huu wa shilingi bilioni 60 ni sehemu ya
marejesho ya fedha za EPA kama Bunge lilivyokuwa limeelezwa kuwa fedha za EPA
zitaelekezwa kwenye kilimo.
C : MWENENDO WA KILIMO NCHINI
Mheshimiwa Spika, Tangu mwaka 1996 hadi 2012 uchumi wa Tanzania
umekuwa ukikua kati ya asilimia 3.5 hadi 7.8, na kwa kipindi cha
mwaka jana inaonyesha kuwa uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.5[1]
Aidha, Kasi ya ukuaji katika sekta ya kilimo
ambayo inaajiri takribani asilimia 75 ya nguvukazi nchini ilipungua, kutoka
asilimia 4.2 mwaka 2010 hadi 3.6 mwaka 2011. Ni ukweli uliowazi kuwa taarifa hiyo ya ukuaji wa uchumi haiendani na
hali halisi ya maisha ya wananchi. Mafanikio yanayotajwa yameshindwa kuondoa
umasikini kwa wananchi hasa wale wanaoishi vijijini.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
bara ina jumla ya eneo la hekta milioni 29.4 linaloweza kufanya uzalishaji kwa
umwagiliaji, lakini ni karibu eneo la hekta laki 330,000 tu (sawa na 1.1% tu ya
eneo linalofaa kwa umwagiliaji) ndilo kwa sasa linafanya uzalishaji kwa
umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Kilimo ni biashara kama zilivyo biashara nyingine, hivyo ili
kiweze kupiga hatua ni lazima mazingira ya kufanyia biashara hiyo ya kilimo yaboreshwe
ili wakulima wadogo na wale ambao wasiojihusisha na kilimo wavutiwe kufanya biashara
hiyo.
Katika mazingira ya nchi yetu, wakulima wadogo ndio wadau wakubwa wa
kilimo, hivyo basi changamoto za kuongeza tija ndio kikwazo cha kuifanya sekta
hiyo kukua na kuondoa au kupunguza umasikini.
Mheshimiwa
Spika, Mfumuko wa bei unauhusiano
wa moja kwa moja na maisha ya watanzania wengi. Kupanda kwa bei za vyakula kwa
zaidi ya asilimia 50% maana yake ni kushuka kwa uwezo wa manunuzi(Kipato) kwa
wananchi masikini waishio mijini kwa asilimia 25%(Kwa kutilia maanani kuwa
familia hizo hazizalishi chakula).
Sambamba na hilo ni kuwa kipato kikubwa kwa kipindi hicho
kinatakiwa kiende kwa wakulima wazalishaji wa chakula[2].
Mheshimiwa
Spika, changamoto kubwa kwa kilimo ni jinsi ya kuongeza tija kwa eneo dogo la
ardhi inayotumiwa na wakulima wadogo kwa kulinganisha na nguvu kazi
inayojihusisha katika kilimo. Changamoto hii inaweza kuondolewa kirahisi kama
mahitaji muhimu katika kufanikisha kilimo yatapatikana yakiwa na ubora na kwa wakati, mahitaji hayo
ni huduma za ushauri, pembejeo bora (mbegu,madawa) miundombinu ya umwagiliaji,
huduma za kibenki, masoko ya uhakika n.k
Mheshimiwa Spika, Serikali
hii ya CCM inajuua kwamba bila kuwekeza kikamilifu katika Kilimo, umasikini
utaendelea kulitafuna taifa hili, lakini bado sioni dhamira ya dhati ya
Serikali kuwekeza katika Kilimo. Nasema hivi kwa sababu mwezi Agosti, 2010,
aliyekuwa Waziri wa kilimo wakati huo, Mhe. Stephen Masatu Wassira, alisema kwamba; “Msingi wa maudhui ya azma ya KILIMO KWANZA, ni kukiri kwamba, haiwezekani
kukuza uchumi wa Tanzania na kiwango cha kupunguza umaskini kwa Watanzania
walio wengi bila kuwekeza kwa kiwango cha kuridhisha katika Sekta ya Kilimo.”
Mheshimiwa Spika, nikumbushe Bunge hili kuwa
Tanzania iliridhia na kujiunga na mpango wa maendeleo kusini mwa Afrika, CAADP,
tangu ulipoasisiwa mwaka 2003. Pamoja na malengo mengine mpango huu ulilenga
kuongezwa kwa bajeti kwa sekta ya Kilimo hadi 10% ya Pato ghafi la Taifa (GDP).
Hii inajulikana zaidi kama azimio la Maputo-Msumbiji, ambalo lilizitaka nchi zote mwanachama wa African
Union (AU) kutenga asilima 10 ya bajeti zao kila mwaka kwa ajili ya kilimo.
Mheshimiwa
Spika, Tanzania imekuwa na mipango
mingi ya kilimo na kwa sasa tayari kuna mpango mpya uitwao TAFSIP- (Tanzania Agriculture Food Security
Investment Plan) ambao ni
Mpango wa miaka 10 ijayo wenye lengo la kukifanya kilimo kiweze kuchangia
katika ukuaji wa uchumi, kuongeza pato la mkulima na taifa kwa ujumla na
kuhakikisha kwamba taifa linajitosheleza kwa chakula na lishe.
Mheshimiwa Spika, Mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia
yaliyomo katika miongozo na mifumo ya kutekeleza Dira ya Maendeleo yaani Vision
2020 na 2025, Programu za kitaifa yaani MKUKUTA, KILIMO KWANZA, ASDP na Mpango
wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012- 2015/16).
Mheshimiwa Spika, TAFSIP imeainisha maeneo makuu saba (7) ya uwekezaji ili kufikia
lengo la asilimia 6 ya ukuaji wa sekta kila mwaka na kwamba Serikali itaongeza
bajeti yake hadi kufikia asilimia 10 kama Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo
Barani Afrika yaani Comprehensive Africa Agriculture Development Programme
(CAADP) inavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, gharama za kutekeleza mpango kwa
kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2011/2012 – 2015/16 ni shilingi
za kitanzania trilioni 8.7 au dola za kimarekani bilioni 5.3. Wastani wa mahitaji ya fedha kwa mwaka
ni shilingi trilioni 1.7
D : MPANGO WA KUKUZA KILIMO KATIKA
UKANDA WA KUSINI MWA TANZANIA (southern agricultural growth corridor of
tanzania – SAGCOT).
Mheshimiwa Spika, Serikali
imekuwa ikihamasisha na kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi katika kilimo na kujenga dhana ya kibiashara
biashara kama ilivyoainishwa katika nguzo ya pili ya KILIMO KWANZA ambayo pia
umeanza kutekelezwa kupitia Mpango wa Kukuza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa
Tanzania (Southern Agricultural Growth
Corridor of Tanzania – SAGCOT). Mpango huo unalenga zaidi kuvutia uwekezaji
katika kilimo kwa ushirikiano baina ya wakulima wakubwa na wadogo katika maeneo
husika.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji
wowote ambao unalenga kuondoa njaa bila ya kuondoa umasikini kwa wakulima, huo
ni mpango mwingine wa kutuharibia ardhi yetu na unatakiwa ukaribishwe kwa
tahadhari kubwa katika nchi yetu. Hii inatokana na ukweli kwamba uwekezaji
katika kilimo unatakiwa ufanywe kwa wakulima wadogo na wa kati kwani ndio
sehemu kubwa ya jamii inayojihusisha na kilimo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali kuwekeza zaidi kwenye kada hizo mbili za
wakulima. Aidha, tunaitaka Serikali kuchagua aina ya kilimo kitakacho harakisha
kuondoa umasikini kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa
Spika, ujio wa SAGCOT hapa nchini, unapata uhamasishaji mkubwa kutoka
ndani na nje, kwa dhana kuwa ndio mkombozi wa tatizo la njaa hapa nchini. Ujio
huo unakuja pia na washirika wake ambao ni makampuni makubwa Duniani
yanayozalisha Mbolea na Mbegu pamoja na
madawa yakiwa kama washirika katika mpango huo wa uwekezaji mkubwa kwenye
kilimo.
Mheshimiwa
Spika, makampuni hayo washirika katika mpango huo, sio kwamba itakuwa ni
mara ya kwanza hapa Tanzania bali washirika hao wamefanyakazi mataifa mengi
hapa Duniani. Moja ya nchi hizo ni India.
Maandiko na taarifa mbalimbali
kuhusiana na mpango kama huu wa SAGCOT kwenye nchi ya India zinaonyesha kuwa
wakulima wadogo na wakati wamekuwa ni majeruhi wakubwa wa makampuni hayo
yanayozalisha mbegu, madawa na kutoa mbolea. Makampuni ya mbegu hasa za pamba
yamesababisha wakulima kujiua.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na utafiti uliofanywa na Wizara ya Kilimo nchini India
iliishauri Serikali ya nchi hiyo kusitisha uuzwaji wa mbegu za pamba aina ya
Bt-Cotton zilizokuwa zinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Monsanto, ambayo
ilitumia fedha nyingi kuwashawishi wakulima kuachana na mbegu zao za asili na
kutumia mbegu zilizokuwa zinazalishwa na Kampuni hiyo. Mbegu hizo zilionyesha ni ghali sana kwa
asilimia 100 kulinganisha na mbegu za asili za Pamba, mbali ya ughali huo mbegu
hizo zilionekana kuwa hazina uwezo wa kuota katika msimu unaofuata, jambo
ambalo linazidisha kuongeza matatizo kwa wakulima.
Mheshimiwa
Spika,
ukweli uliotolewa na Wizara ya Kilimo ya India ni kwamba zaidi ya wakulima wadogo 1,000
wanajiua kila mwezi kutokana na kukidhiri kwa madeni yanayo limbikizwa
kutokana na mbegu zizalishwazo na Monsanto.
Hilo limepelekea wakulima wadogo
zaidi ya 125,000 kujiua[3].
Mheshimiwa
Spika, kitendo chochote kitakachopelekea wakulima wadogo kununua mbegu
ambazo haziwezi kutunzwa na kuoteshwa zaidi ya msimu mmoja, Kambi Rasmi ya
Upinzani inauweza kukiita kitendo hiki kuwa ni hujuma. Taarifa hiyo inaendelea kusema kuwa uzalishaji mkubwa
ni kwa miaka mitano ya mwanzo tu, na baada ya kipindi hicho maafa yanafuatia.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kufanya tathmini ya kina kuhusu ujio wa makampuni
hayo ya mbegu kwani kwa historia na maandishi niliyoyaweka hapo juu ni janga
lingine linalokuja kwa wakulima wadogo na
kilimo chetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani inataka kujua mpango huo ni maeneo gani ambayo yako wazi kwa ajili
ya uwekezaji zaidi ya kunyang’anya wakulima wadogo mashamba yao (land grabbing) ambayo ndipo
tunapoelekea. Aidha, wizara ya kilimo imekuwa ikihamasisha uwekezaji katika
kilimo kupitia vijarida vyake vikiainisha maeneo yenye fursa ya kilimo (Investment potential and opportunities in
agriculture).
Mheshimiwa Spika, fedha
zilizotengwa na kuidhinishwa mwaka
jana kwa ajili ya SAGCOT ni shilingi
bilioni 6.567 kwa mwaka huu zimetengwa kwa ajili ya uendeshaji wa mradi huo ni
shilingi bilioni 3.827, hizi sio za uwekezaji na ni fedha za ndani. Hoja ni
kwanini fedha hizi za ndani zimetengwa kidogo kwa kulinganisha na mwaka
jana ? Je ni kweli Mradi huo ni kipaumbele cha Taifa kama
inavyodaiwa ? Mwaka wa fedha unaomalizika fedha zilizotolewa na hazina ni shilingi
bilioni 1.75 lakini zilizotumika hadi Machi 2013 ni asilimia 77 tu. Je na hizo
zilitumika katika uendeshaji badala ya uwekezaji? Na wakulima wadogo na wa kati
wamenufaika vipi katika mgawo wa awamu ya kwanza ya fedha hizo za SAGCOT?
Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka kuelewa ni maeneo gani yaliyoanishwa yako wazi na
hayatumiki kwa shughuli nyingine zaidi ya kilimo kwani tumekuwa tukiambiwa
serikali inaandaa land bank. Kambi
inataka kujua ni maeneo gani yaliyoainishwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali
ikiwemeo kilimo, mifugo na makazi kuondokana na migogoro inayoendelea hivi
sasa.
Mheshimiwa Spika, mjumuiko
wa asasi za kiraia ulikaa na kutoa
ushauri kwa Serikali katika bora kutekeleza
mpango wa SAGCOT ili vijiji vinavyotoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa
mpango huo vinufaike na uwekezaji huo katika chapisho lao[4].
Ushauri huo ni kama ifuatavyo :
1) . Kuweka
wazi jinsi gani upatikanaji wa ardhi na mchakato mzima wa uwekezaji na jinsi
wazalishaji wadogo na wa kati wanaozunguka maeneo ya uwekezaji watakavyopata mitaji.
2) Matumizi
bora ya ardhi katika vijiji ambavyo vitatoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa
SAGCOT yawekwe chini ya uangalizi huru ili kuepuka mgongano wa kimaslahi.
3) Eneo la
ardhi ya vijiji litakalotolewa kwa msingi wa uwekezaji wa SAGCOT libaki kama eneo la vijiji kwani baada ya
mradi kumalizika lirudi katika umiliki wa vijiji badala ya eneo hilo kutwaliwa na Serikali kuu.
4) Vijiji
vinavyotoa ardhi ya uwekezaji ni lazima vipatiwe washauri waelekezi ambao ni
huru ili watoe tathmini huru isiyoegemea
upande wowote.
5) Mpango
mkubwa wa uwekezaji wa SAGCOT katika umwagiliaji ni lazima ulazimike kutoa huduma hiyo kwa jamii za wakulima
wanaozunguka mradi huo.
6) Umwagiliaji
ujikite katika kuhakikisha makubaliano ya matumizi bora ya maji na ufuatiliaji
wa mara kwa mara unafanyika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge na watanzania wote utekelezwaji
wa ushauri huo wa ASASI za kiraia hadi sasa umefikia wapi?
E : HALI YA CHAKULA NCHINI
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaonyesha kuwa
kipaumbele cha pili ni kuwekeza katika Sekta ya Kilimo kwa tafsiri pana
ambayo inajumuisha Sekta ya Kilimo cha mazao ya chakula na biashara, Sekta ya Mifugo, Uvuvi, Ufugaji wa Nyuki na
Rasilimali za Misitu. Shabaha Kuu ya kuendeleza Kilimo ni kuleta Mapinduzi ya
haraka ya Kilimo yatakayotuwezesha kuongeza uzalishaji na tija ili
kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada nje.
Mheshimiwa Spika, Kiwango cha ukuaji katika kilimo hakijafikia lengo
lililowekwa na serikali la kufikia ukuaji wa asilimia 10 kwa mwaka kuanzia 2008
– 2015; na ukosefu wa chakula bado ni tatizo kwa watu wengi. Kiasi kikubwa cha
kaya zisizokuwa na chakula cha kutosha zipo vijijini ambapo kilimo kinatagemewa
sana kama chanzo cha kipato
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Bwana Philipe Egger[5] kwenye Jarida la ILO la mwezi Februari,2013
inaonyesha kuwa Africa inaagiza chakula chenye thamani ya karibu dolla za
kimarekani bilioni 50 kwa kila mwaka kwa ajili ya kulisha wakaazi wa miji
inayokuwa kwa haraka sana. Inakisiwa kiasi hiki ni karibu sawa na misaada ya
maendeleo inayotolewa na nchi zilizoendelea.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa Tanzania uingizaji mkubwa wa chakula kutoka nje
hufanywa si kwa sababu Tanzania haina chakula cha kutosha kuweza kukidhi
mahitaji ya wananchi bali ni mkakati unaotumiwa na baadhi ya watendaji
kuhakikisha kuwa nguvu za wakulima hazitoi matunda na wakulima wazidi kuwa
masikini. Mfano mzuri ni uingizaji wa mchele kutoka ‘Thailand’ wakati wakulima
wa mikoa ya Morogoro na Mbeya wakikosa soko la kuuza mchele wao. Kambi ya
Upinzani inaliona hili kuwa ni hujuma kwa wakulima wa Tanzania.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza wakulima ni
kwanini inatoa vibali vya kuingiza nchini mchele wakati mchele upo mwingi kwa
wakulima?
Mheshimiwa
Spika, naomba kunukuu sehemu ya
hotuba ya mhe Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Mipango ya mwaka 2012/2013 aliyoitoa hapa Bungeni ‘Mheshimiwa
Spika, katika kukabiliana na mfumuko wa
bei, Serikali ilichukua hatua zifuatazo: kuhakikisha usambazaji wa chakula
katika maeneo yenye uhaba wa chakula; kuongeza uzalishaji wa mazao ya
chakula; kuendelea kuimarisha hifadhi ya
chakula kwa kuongeza ununuzi wa mazao ya chakula;…….’. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze
watanzania ni wapi inapozalishia
chakula ! Hoja ni kwamba hata chakula kilichonunuliwa kutoka kwa wakulima,
kilinunuliwa kwa mkopo, mfano ni wakulima wa Halmashauri ya Nkasi mkoani Rukwa ambao wanaidai wakala ya Hifadhi ya
chakula ya Taifa zaidi ya shs milioni
500[6].
Mheshimiwa
Spika, huu
ni mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano, kwa
masikitiko makubwa ni kwamba bado tatizo kubwa la ukosefu wa chakula
limeripotiwa kutokea katika wilaya mbalimbali za nchi yetu kutokana na
kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa usambazaji wa chakula kutoka kinapozalishwa kwa
wingi, baadhi ya wilaya hizo ni : Kilindi, Meatu, Iringa, Handeni kati ya August hadi februari
2013 kaya zaidi ya 780 wilayani humo zikakabiliwa na njaa. Kwa kipindi
hicho, wananchi wapatao 81,769 wa kata 12 wilaya ya moshi mkoani Kilimanjaro walihitaji
chakula cha msaada tani 14,634.6 ili kukabiliana na tatizo la njaa
ambalo limeonekana kuathiri shughuli nyingi za kimaendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kwa ujumla
hali ya chakula nchini sio nzuri na
Serikali haionekani kuchukua hatua stahiki kumaliza tatizo hilo, kutokana na
ukweli kwamba mamlaka zilizopewa jukumu la kuhakikisha wahanga wanapewa msaada
wa dharura haraka badala yake mamlaka hizo zinafanyakazi hiyo kwa kuangalia
itikadi za wanasiasa katika maeneo ya wahanga. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kuhakikisha kuwa mamlaka husika zisiingiliwe na watendaji wa kisiasa
jambo linalopelekea mamlaka hiyo kupoteza uhalali wa kuitwa kitengo cha maafa.
F : UHUSIANO KATI YA MGAWO WA BAJETI NA UHABA WA CHAKULA
NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa nchi zilizo makini na mipango yake suala la mgawanyo wa rasilimali za nchi hasa zihusuzo chakula ni lazima ujikite kwenye maeneo ambayo yana athirika mara kwa mara na tatizo la njaa. Utafiti ulioendeshwa na ‘Food Security Information Team (FSIT)’, uligundua kuwa jumla ya mikoa 10 ndiyo inayokumbwa na tatizo la uhaba wa chakula mara kwa mara. Mikoa hiyo ni : Arusha, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mwanza, Mtwara, Shinyanga, Singida, and Tabora.
Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanywa kuona kama mikoa hiyo inapata kipaumbele cha kupata zaidi katika mgawo wa fedha za DADG au la ? Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa, kwa mwaka wa fedha 2009, mikoa hiyo 10 ambayo inaidadi ya watu asilimia 46.2 (karibu 50%) ya watu wote hapa nchini (National Bureau of Statistics (NBS)[7] –Mikoa hiyo ilipatiwa asilimia 30.2% ya fedha zote za bajeti ya DADP kwa 2009/10 (jedwali chini linaonyesha).
Mheshimimiwa Spika, kwa ushahidi huo inaonyesha kuwa mipango ya Serikali mbali na kufanya tafiti haipangwi kutatua matatizo yanayojirudia rudia badala yake inaonyesha kuwa matatizo hayo ni neema kwa watendaji hao wapangaji. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza inakuwaje mikoa yenye idadi karibu nusu ya watanzania wote na inayokabiliwa na uhaba wa chakula mara nyingi, na serikali inaelewa lakini haipewi kipaumbele katika kuhakikisha tatizo la ukosefu wa chakula linaisha ? Au kwa ufupi ni kuwa mgawanyo wa bajeti ya kilimo haiangalii maeneo yenye uhaba wa chakula, Watawala wamechoka kutawala !!!!!!!!!!! hivyo walalahoi hawathaminiwi tena katika mipango yao.
Mheshimiwa
Spika, katika taarifa ya Serikali kwenye kamati ya kudumu ya fedha na
uchumi mwezi Januari 2013, Serikali ilinasema inauza mahindi kwa
wafanyabiashara binafsi toka katika hifadhi ya taifa ya chakula (labda kwa bei
ya chini kuliko ile ya soko). Wafanyabiashara binafsi wanasaga na kuuza kwa
wananchi. Lakini wafanyabiashara hao hao
hulangua wanunuzi wa mahindi au unga kwa kutengeneza vocha mbili na
kuwasainisha wanunuzi bei tofauti.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
iwaeleze watanzania inadhibiti vipi bei
ya unga au mahindi unaouzwa na wafanyabishara walionunua mahindi toka katika
hifadhi ya chakula (kwa bei ya chini) ukilinganisha na bei ya soko ambayo ni
wafanyabishara walionunua unga toka sehemu nyingine? Ni namna gani bei za soko
zitaratibiwa kiasi kwamba wafanyabiashara waliopewa vibali vya kununua mahindi toka
hifadhi ya chakula kuuza unga na mahindi
kwa bei ya chini kuliko bei ilivyo sokoni ?
G: PEMBEJEO ZA KILIMO
Mheshimiwa Spika, kilimo ili
kibebe dhana inayokusudiwa katika sera yake ya mwaka 1997 ya kuwa endelevu,
chenye tija na cha kibiashara ni lazima kubadili zana zilizokuwa zinatumika
hapo kale. Takwimu zinaonyesha kuwa : Maksai wanaotumika katika kilimo wamekuwa wanaongezeka kutoka 320,000
mwaka 1970 hadi kufikia 1,542, 000 mwaka 2010 ambapo majembe yanayokokotwa na
maksai yameongezeka kutoka 140,000 hadi kufikia 620,000 katika kipindi hicho.
Kwa mwaka 1960 kama nchi ilikuwa na Matrekta makubwa 2,580 yaliyotumika katika kilimo na mwaka 2010
yameongezeka hadi 7,825[8]. Aidha kwa mwaka 2010 idadi ya
matrekta ya mkono ilikuwa 4,571[9]
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani kwa kuangalia takwimu hizo za zana za kilimo, inaonyesha wazi
itachukua kipindi kirefu sana kukibadilisha kilimo kwani ongezeko la maksai na
majembe ya kukokotwa na maksai hayaendani na ongezeko la matrekta licha ya
uwepo wa mipango na mikakati mingi ya kuinua kilimo. Hizo zinaonyesha kuwa ni
ngonjera za muda mrefu ambazo zinaendelea hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, Matumizi ya mbegu bora, mbolea, dawa za mimea na
dawa za kuulia wadudu yanakwamishwa na upatikanaji mdogo na bei za juu za
pembejeo. Tatizo la umbali toka kijijini hadi maduka ya pembejeo nalo ni
changamoto. Wananchi husafiri umbali wa takribani kilomita 25 hadi 56 katika
wilaya ya Lindi Vijijini, na kati ya kilomita 25 hadi 70 katika wilaya za
Mtwara Vijijini na Iringa Vijijini na kati ya kilomita 12 hadi 80 katika wilaya
ya Hanang’ kuifuata huduma ya pembejeo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu
matumizi ya pembejeo za kilimo na udhibiti wa ubora wa pembejeo hasa mbegu,
mbolea na viuatilifu. Kambi ya upinzani inapenda kujua serikali imechukua hatua
gani kuhusu malalamiko ya wakulima wengi kuhusu mbegu wanazouziwa kutoota,
mbolea kutokuwa na tija yeyote kwenye mazao na viuatilifu kushindwa kuua
visumbufu vya mimea na mazao. Aidha, pamoja na serikali kuajiri maafisa ugani
wengi, lakini bado wakulima hawapati huduma hiyo hasa kuhusu matumizi bora ya
pembejeo za kilimo na kilimo biashara (farming as business).
Mheshimiwa
Spika, mgawo wa shilingi
bilioni 75 kwa ajili ya vocha za
pembejeo (mbolea), kutokana na hali halisi ilivyo, fedha hizi zinaweza kutumika
kifisadi kama ambavyoimekuwa kwa miaka ya nyuma. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali fedha hizo kupelekwa Idara ya Umwagiliaji ili
kuondoa adha ya ukame ambalo limekuwa kikwazo kikubwa cha uzalishaji. Kilimo
cha kutegemea mvua kumeleta hasara na umasikini kwa wakulima hata wale
wanaopatiwa pembejeo za ruzuku.
H : KILIMO CHA UMWAGILIAJI
Mheshimiwa Spika, katika fursa
ya kujihusisha na kilimo cha umwagiliaji Tanzania ni ya pili katika bara la
Afrika nyuma ya Nchi ya DRC kwa kuwa na hazina kubwa ya maji. Takwimu zilizopo
zinaonyesha kuwa kati ya eneo lote
lifaalo kwa kilimo cha umwagiliaji la hekta millioni 29.4 ni asilimia 1%
inayotumika.
Mheshimiwa Spika, Kwa sasa
nchi yetu ina maeneo makubwa ya ardhi yenye rutuba na mito mikubwa pamoja na maziwa makubwa kama vile Viktoria, Nyasa,
Tanganyika na Rukwa bila ya kusahau mabonde makubwa ya mito, hii asilimia moja
sio kwamba ni ukosefu wa maji ya umwagiliaji ila ni kukosekana kwa utashi wa
kisiasa na jinsi tunavyopanga vipaumbele vyetu katika matumizi ya raslimali
fedha.
Mheshimiwa
Spika, Fursa katika uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji ni kubwa mno
hapa nchini, lakini kuna tatizo kubwa la raslimali watu yenye ujuzi katika
nyanja ya umwagiliaji kwenye ngazi ya Halmashauri kwa ajili utekelezaji kwenye
uwekezaji huo. Nyaraka zinaonyesha kuwa kikundi kazi kilichoundwa mwaka 2010
August na ‘the Basket Fund Steering Committee’ ili kuchunguza chanzo cha fedha
nyingi za miradi ya umwagiliaji kupelekwa mwaka wa fedha unaofuata kiligundua
kuwa, kati ya Halmashauri 132, kuna mainjinia 32 tu, na mafundi mchundo wa
umwagiliaji (irrigation technicians) 107. Katika ngazi ya mkoa, kuna mainjinia
wa umwagiliaji 17 tu. Baya zaidi ni kwamba hata wale mafundi mchundo waliopo ni
kwamba hawana vitendea kazi. La mwisho lakini la umuhimu ni ukiritimba
uliokithiri katika Halmashauri zetu ambao ni kikwazo kikubwa katika uwekezaji
wa miradi kwenye shughuli za kilimo[10].
I : VYAMA VYA USHIRIKA NA BODI ZA MAZAO
Mheshimiwa Spika, Shabaha
kuu ya Vyama vya Ushirika vilipoanzishwa, ilikuwa kuuza mazao ya wanachama kwa bei nzuri na wakati huohuo kuondoa unyonyaji wa wafanyabiashara
ambao walikuwa wakinunua mazao hayo kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu na pia kutayarisha mazao kusudi yawe katika hali bora inayotakiwa na
wanunuzi.
Aidha, kukusanya mazao kutoka kwa wakulima, na kufanya mipango ya kusafirisha mazao hayo toka kwa
wakulima hadi “mikononi” mwa Halmashauri za Mazao au mpaka katika masoko ya
dunia[11]. Pia Vyama vya Ushirika vikiwemo vya Akiba
na Mikopo (SACCOS) na vile vya kilimo na masoko (AMCOS) vimedhihirisha kuwa
nguzo muhimu katika kuwapatia maisha bora Watanzania.
Mheshimiwa Spika, Ushirika unaonyeshwa kuwa ni njia
mojawapo ya kuboresha maisha ya wananchi wa Tanzania walio wanyonge kiuchumi[12]. Hoja ni kuwa kweli maisha bora yaliyokusudiwa
wakati wa uanzishwaji wa vyama hivyo yanaweza kupatikana ? wakati bei kwa
mkulima anaambiwa ni nguvu za ushindani wa soko?
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kutoa tathmini ya utendaji mzima wa AMCOS na imesaidia vipi
hizo AMCOS kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa maendeleo ya wakulima ?
J : BODI YA NAFAKA NA MAZAO MCHANGANYIKO
Mheshimiwa Spika, Nafaka ni mazao makuu ya chakula ambayo hutumiwa na
watanzania wote waishio mijini na vijijini. Nafaka zinaweza kuhifadhiwa kwa
muda mrefu kuliko mazao mengine ya chakula na mara nyingi nafaka huzalishwa
mara moja au mbili kwa mwaka. Kwa hiyo ili iweze kupatikana na kutumika kwa
wakati wote ni lazima kuhifadhi.
Mheshimiwa
Spika, aidha, ili kuweza kuwa
na bidhaa zenye thamani ni lazima kusindika. Jitihada zimekuwa zikifanywa na
serikali kuongeza tija na uzalishaji wa mazao hayo. Uzalishaji wa mazao ya
nafaka unakadiriwa kufikia wastani wa tani 3,897,500 kwa mwaka. Pamoja na
ongezeko la uzalishaji, teknolojia zinazotumika katika uvunaji, utayarishaji na
hifadhi ni duni na husababisha upotevu mkubwa wa mazao hayo. Wastani wa tani
1,559,000 za mazao ya nafaka hupotea kila mwaka[13].
Mheshimiwa
Spika, sheria iliyotungwa na bunge kwa ajili ya kuanzisha chombo hiki
ilikuwa ni kwa ajili ya kuwapatia wakulima huduma muhimu ikiwemo kuwapatia bei
nzuri itakayokidhi gharama za uzalishaji mazao yao ambayo hayana chombo maalum
ya kuyasimamia.
Mheshimiwa
Spika, kwa masikitiko makubwa ni kwamba chombo hiki kimeshindwa kabisa
kuwasaidia wakulima kuwahakikishia ununuzi wa mazao yao kwa bei inayoweza
kurejesha gharama za uzalishaji, mbali na bodi yenyewe kuingia katika mchakato
wa ununuzi wa mazao hayo.
Mheshimiwa
Spika, kwa kadri Serikali inavyochelewa kutimiza wajibu wake kwa mujibu
wa sheria zilizopo, mkulima anazidi kuwa fukara na kilimo kinazidi kukosa tija
kwa mkulima na pale pale mfanyabiashara anazidi kuneemeka na kilimo hicho,
hivyo mnyororo wa biashara isiyoakisi hali halisi baina ya pande mbili husika
inazidi kushamiri, jambo ambalo ni hatari na linapingana na sera yetu ya
kilimo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzania inasema kuwa, muda umefika sasa kwa
mkulima na kilimo kuonekana kuwa sio chaguo la mwisho katika orodha ya kazi za
ajira kwa vijana wa nchi hiii. Jambo hili linaweza kufikiwa sio kwa mikakati
iliyo kwenye makaratasi na kufungiwa makabatini bali kwa kuangalia gharama
halisi ya utoaji ruzuku na gharama halisi kama mkulima akipatiwa bei dira
inayoweza kufuta gharama za uzalishaji. Aidha, ruzuku ikaingizwa kwenye
uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani za mazao.
K: MUHOGO
Mheshimiwa Spika, zao
la muhogo ambalo linalimwa karibu na wakulima wote hapa nchini, linachangia
takriban asilimia 15 kwenye kapu la uzalishaji wa chakula hapa nchini. Ni zao la pili nyuma ya mahindi
abalo ni zao kuu la chakula hapa nchini. Mikoa inayolima muhogo ni Mtwara, Pwani, Mwanza, Kigoma,
Tanga, Morogoro, Mara, Ruvuma, Shinyanga na Lindi. Ila
kiwango cha kilimo cha zao hilo ndicho kinachotofautiana kati ya mkoa na mkoa[14].
Kitendo kilichofanywa na Serikali kwa wakulima wa zao la muhogo wa Mtwara
Mikindani la kuwalipa shilingi 130 kwa shina, ni kitendo cha kudhalilisha
mkulima na kilimo kwa ujumla wake. Wakulima wa Mtwara Mikindani kwa nyakati
tofauti walilamikia kiwango hicho.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani inataka Serikali itoe maelezo, kwa njia hii ya uthamanishaji wa
shina la muhogo kwa shilingi 130, je kilimo kinaweza tumika kama nyenzo ya
kuondoa umasikini ? Au hii ni kiini macho kwa wakulima?
Mheshimiwa Spika, kutokana na
takwimu hizo za uzalishaji wa muhogo hapa nchini na umuhimu za zao hilo katika
uchangiaji kwenye kapu la chakula hapa nchini, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali iwaeleze wananchi ni mkakati gani uliopo wa kuhakikisha kuwa kilimo
cha mihogo hapa nchini kinaleta tija kwa wananchi na Taifa katika kuondoa
umasikini na kukuza uchumi?
L: NGANO
Mheshimiwa Spika, Uzalishaji
wa ngano kwa Tanzania sio kipaumbele kwa maendeleo ya sekta ya kilimo. Hii
inatokana na ukweli kwamba zao la ngano halina sera wala halimo kwenye
vipaumbele vya kuliendeleza (masoko na viwanda vya kuongeza thamani).
Mheshimiwa
Spika, Kwa Tanzania matumizi ya ngano katika orodha ya vyakula ni ya
nne nyuma ya mahindi, muhogo na mchele. Hii inaonyesha ni jinsi gani zao la
ngano lilivyo na umuhimu kwa nchi yetu. Matumizi ya ngano kwa maeneo ya mijini
ni takribani asilimia (83%) na vijijini ni takriban asilimia (17%) (Kilima,
2006).
Mheshimiwa Spika, maendeleo
ya zao hili yameachwa mikononi mwa sekta binafsi iliyonunua mashamba makubwa na
inamiliki viwanda vya usagishaji wa zao hilo. Jambo hili linapelekea wakulima
wadogo ambao wametawanyika sana kumezwa na wafanyabiashara wakubwa. Hata hivyo
Tanzania inauwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 164,000 kwa mwaka kama Serikali
itaweka sera madhubuti ya kuhakikisha hata wakulima wadogo wanauza ngano yao
kwa bei inayoweza kuwa na tija kwao, kama ilivyokuwa hapo awali wakati wakiuza
kwa NMC.
Mheshimiwa
Spika, kwa sasa ngano ya kawaida iliyopetwa kilo moja inauzwa kati ya
shilingi 800/- hadi 900/- Wakati bidhaa zitokanazo na ngano (Mkate, chapati,
Keki, maandazi n.k) bei zake zimekuwa zikipanda kila kukicha. Mkate wa gramu
500 unauzwa kati ya shilingi 1200/- hadi 1700/-. Na kwa upande wa chapati
zinauzwa kati ya shilingi 200/- hadi 500/-.
Mheshimiwa
Spika, bidhaa hizi za ngano ni muhimu sana kwa jamii ya watanzania
waishio mijini, swali la msingi ni namna gani Serikali inahakikisha wakulima
wadogo wa zao hilo na wao wananufaika na umuhimu wa zao hilo kwa jamii ziishizo
mijini?
Mheshimiwa
Spika, bei ya ngano kwa miaka
miwili ya nyuma ilipanda kwa asilimia 65% kutokana na kutokuwepo kwa uhakika wa
uzalishaji toka kwa nchi za Bulgaria, Georgia, Romani, Russia, Turkey na
Ukraine (Black Sea Countries)[15].
Uagizaji wa ngano toka nje umeendelea kupanda na sasa inakadiriwa kuwa ni tani
1milioni wakati uzalishaji wa ngano kwa mwaka ni tani 100,000. Tofauti na uzalishaji
na mahitaji ni kubwa sana na hii inaonyesha ni jinsi gani fursa kwa wakulima
wetu ilivyo kubwa sana.
Mheshimiwa
Spika, mbegu ya ngano kilo moja inauzwa kwa shilingi 5,000/- na gunia la
kilo 100 linauzwa kwa shilingi 500,000/-. Na kwa kawaida kilo 100 za mbegu
zinatosha kupanda hekta 2 tu. Hoja ni kwamba kwa bei hiyo ya mbegu ni kweli
mkulima mdogo ili aweze kunufaika na kilimo cha ngano alime hekta ngapi? Na
bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko inafanya nini kwenye zao hili muhimu
kusudi liongeze tija?
M: ZAO LA KOROSHO
Mheshimiwa Spika, zao hili
kwa muda mrefu limeachwa na wakulima wake wameachwa kana kwamba wao hawazalishi
zao lenye faida kubwa kwa taifa hili na hasa katika kulipatia taifa letu fedha
nyingi za kigeni ambazo badala ya kuelekezwa kwenye kuimarisha viwanda vya
kubangua korosho vimeachwa vife na wakulima waendelee kuuza korosho ghafi nje
ya nchi na hivyo
hawapati faida
kama ilivyotakiwa kuwa, mifano halisi ni kama ifuatavyo hapa chini ya viwanda
vilivyouwawa ;
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya malalamiko au changamoto
zinazotolewa na bodi ya korosho ni kuwa
nanukuu, “ukosefu wa bei ya uhakika ya kuuzia korosho ghafi.
Utegemezi wa soko la nje la korosho ghafi. Zaidi ya asilimia 95 ya korosho
ghafi tunayozalisha nchini inategemewa kununuliwa na nchi za nje. Zaidi ya
asilimia 90 ya korosho ghafi hununuliwa na wamiliki wa makampuni ya ubanguaji
kutoka India, hivyo soko la korosho ghafi kuu kwa ujumla lina wanunuzi kutoka
nchi moja wakati wauzaji ni wengi. Kwa sababu hiyo ni wazi kwamba wanunuzi hao
wana nafasi kubwa ya kukaa pamoja na kupanga bei. Kwa ujumla hakuna ushindani
wa bei”.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa nukuu hiyo ya Bodi ya Korosho
inaonyesha kuwa India imehodhi soko la korosho na hivyo wanapanga bei wao.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tafiti nilizozifanya
zinaonyesha kuwa Vietnam nayo ni nchi inayonunua na kuuza Korosho ndani na nje
kwa msimu wa mwaka 2011 ilinunua korosho ghafi takriban tani 450,000 na hizo
zilitoka Africa ya Mashariki, Afrika ya Magharibi na Indonesia Australia,
Uarabuni, Russia, Uchina na Nchi za Scandnavia[16].
Mheshimiwa Spika, kurudishwa kwa Viwanda vya Korosho
vilivyouzwa na vikashindwa kufanyakazi iliyotarajiwa ndio ufumbuzi wa kudumu
kwa Serikali kuingia kwenye masoko ya nchi wanunuzi nilizozitaja hapo juu.
Mheshimiwa
Spika, mbali ya
matatizo hayo ya soko naomba kunukuu kauli ya Mhe Naibu Waziri kwenye taarifa
rasmi za Bunge ya tarehe 4 February
2013,wakati akijibu swali la Nyongeza la Mhe Mwijage, “Mheshimiwa
Naibu Spika, lakini bado Korosho kwa kiasi kikubwa inabanguliwa India. Sasa
tatizo tulilokuwa nalo ni kwamba Korosho ya Tanzania ndiyo Korosho premium duniani, lakini hatujaifanyia
branding kwa sababu kwenye hali
ya kukandamiza hii hali ya Korosho kuna maslahi kwa watu wengi ambayo
inawakandamiza wakulima”.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kulieleza Bunge hili maslahi ya watu wengi ambayo yanawakandamiza
wakulima na watu hao wengi tunaitaka Serikali iwataje watu hao ili Bunge kwa
liweze kuishauri Serikali vizuri jinsi ya kushughulika na kundi hilo
linalokandamzia maslahi ya wakulima.
Mheshimiwa Spika,
ubinafsishaji wa mashamba, viwanda na mashirika ya umma hapa nchini hasa
vilivyokuwa kwenye sekta ya kilimo vimekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
kuzalisha chini ya kiwango na kutoendelezea kabisa. Kambi ya upinzani inashauri
kuwa mashamba yote hasa yale ya NAFCO BASOTU, KAPUNGA na ya CHAI-TUKUYU
yaendeshwe chini ya ushirika kama ilivyo kwa maeneo mengine ya Mbarali na Mvomero
wananchi kuondokana na umaskini na kupunguza idadi kubwa ya Watanzania
wasiokuwa ajira
Mheshimiwa
Spika, naomba
ninukuu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma KWA MWAKA WA FEDHA UNAOISHIA JUNI 30, 2010 kama ilivyo wasilishwa hapa Bungeni tarehe 17 April 2012 kuhusu tathimini ya
viwanda vya Korosho.
i.
Kiwanda cha Korosho cha Likombe.
Mheshimiwa
Spika, Kiwanda hiki kipo mjini Mtwara na
kilijengwa mwaka 1980 kwa kutumia teknolojia ya Kijapani. Kwa Mwaka
2004,kiwanda kiliuzwa kwa kampuni ya Micronix System Limited kwa
bei ya shilingi milioni 100 ambayo alikwishalipa.
Mheshimiwa Spika,
Kiwanda hakijawahi kuzalisha tangu
kilipobinafsishwa mwaka 2004. Mwekezaji hajafanya ukarabati wowote wa mashine
zilizokuwepo kiwandani ila amenunua mashine nne mpya za upakiaji ambazo ni mixing,
packing, drying na humidifier machines. Aidha ilibainika
kuwa Mwekezaji amekodisha sehemu ya ghala kwa kampuni binafsi ambayo inaendesha
zoezi la kutunza korosho kwa mtindo wa stakabadhi gharani na pia amekodisha
sehemu ya Kiwanda kwa Kampuni ya Olum ambayo inafanya shughuli za Ubanguaji wa
Korosho kwa kiasi kidogo.
ii.
Kiwanda
cha Korosho cha Mtama
Mheshimiwa
Spika, Kiwanda kipo Lindi vijijini na kilijengwa
mwaka 1978 kikiwa na uwezo wa kubangua tani 5,000 za korosho kwa mwaka. Kiwanda
kiliuzwa kwa kampuni ya Lindi Farmers Company Limited mwaka 2005 kwa bei ya
shilingi milioni 30.0 ambayo amekwishalipa. Hadi kinabinafsishwa kiwanda
kilikuwa katika hali nzuri na kwamba yalihitajika matengenezo madogo madogo.
iii.
Kiwanda cha Korosho cha Lindi
Mheshimiwa Spika,
Kiwanda kipo mjini Lindi na kilijengwa
kuanzia mwaka 1977 kwa kutumia teknolojia ya Kitaliano na kilikuwa na uwezo wa
kubangua tani 10,000 za korosho kwa mwaka. Kiwanda kilifanyiwa majaribio mwaka
1978 na kuendelea kufanya kazi hadi mwaka 1996, kiliposimama. Mwaka 2004
kiwanda kiliuzwa kwa kampuni ya Bucco Investment Holdings Limited kwa
bei ya shilingi milioni 50.0.
Mheshimiwa Spika,
Mwekezaji alitakiwa kuwekeza kiasi cha dola
za kimarekani 600,000 kwa ajili ya ukarabati wa kiwanda. Mwekezaji amefanya
ukarabati kwa gharama ya shilingi milioni 250. Maeneo yaliyofanyiwa ukarabati
ni boiler, mashine za kukatia
korosho na grading. Kiwanda kimesima kwa
kukosa mtaji wa uendeshaji. Ni wazi kuwa Mwekezaji amevunja
Mkataba wa Mauzo kwa kushindwa kufufua kiwanda.
iv.
Kiwanda cha Korosho Newala II
Mheshimiwa Spika, Kiwanda
kipo wilaya ya Newala mkoa wa Mtwara. Ujenzi wake ulianza mwaka 1977 na
kukamilika mwaka 1980 kwa kutumia tekinolojia ya kijapani na kilikuwa na uwezo
wa kubangua tani 10,000 za korosho kwa mwaka. Kiwanda kilifanya kazi kwa muda
wa mwaka mmoja na kisha kusimama kutokana na uhaba wa korosho ghafi.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2004 kiwanda kiliuzwa kwa kampuni ya Micronix
Sytems Ltd. kwa bei ya shilingi milioni 75.0. Mwekezaji
alikwishalipa fedha zote na kukabidhiwa kiwanda. Hadi wakati kiwanda hiki
kinabinafsishwa, sehemu kubwa ya kiwanda ilikuwa katika hali nzuri ukiacha
matengenezo ya sehemu kadhaa kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila ya kufanya
kazi.
Mheshimiwa Spika, Kulingana
na Mpango wa uwekezaji, mnunuzi alitakiwa kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani
milioni 3.64 katika ukarabati wa kiwanda kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia
mwaka 2006 mpaka 2010 kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Mauzo. Mwekezaji
alieleza kuwa amewekeza kiasi cha shilingi milioni 150 katika ukarabati wa
kiwanda kwa kununua mashine za kutumia teknolojia ya mkono. Ukarabati huo
ulifanyika mwaka 2009. Mashine za zamani zimekusanywa na kurundikwa sehemu moja
kwa kile mwekezaji anachodai kuwa teknolojia yake imepitwa na wakati.
v.
Kiwanda
cha Korosho Newalla I
Mheshimiwa Spika,Kiwanda
kipo mjini Newala, mkoa wa Mtwara,kilijengwa mwaka 1976 na
kufanyiwa majaribio mwaka 1981 na hakikufanya kazi baada ya majaribio ya awali.
Kiwanda hiki kilijengwa kwa mitambo ya teknolojia ya Kitaliano yenye uwezo wa
kubangua tani 10,000 kwa mwaka. Aidha kwa maelezo ya Uongozi wa Shirika Hodhi
la yaliokuwa Mashirika ya Umma (CHC), Mwaka 2004 kiwanda kiliuzwa kwa kampuni
ya Agrofocus Limited kwa bei ya shilingi milioni 75.0. Mwekezaji alikwisha
kamilisha malipo. Hadi wakati kinabinafsishwa, mitambo na mashine ya kiwanda
vilikuwa katika hali nzuri ukiacha sehemu chache za umeme na mikanda ya
kusafirishia korosho. Aidha, majengo ya kiwanda yalikuwa katika hali nzuri isipokuwa sehemu kadhaa za paa ambazo
zilihitaji ukarabati ili kuzirejesha katika hali ya kawaida.
Mwekezaji
amewekeza kiasi cha shilingi milioni 718.0 katika ukarabati wa kiwanda. Mashine
zote zimekarabatiwa na zinafanya kazi. Kiwanda kipo katika hali nzuri,
mazingira ni safi na majengo yote yamepakwa rangi. Mashine pia zipo katika hali
nzuri.
Mheshimiwa Spika,
baada ya Tathmini, Kamati haijaridhishwa
kabisa na zoezi la ubinafshishaji wa Mashirika ya Umma katika Sekta Ndogo
ya Viwanda vya Korosho (Mamlaka ya
Korosho). Viwanda vyote vya kubangua korosho vilivyojengwa kwa Mkopo wa Benki
ya Dunia vyenye thamani ya Dola milioni 284 havifanyi kazi, wawekezaji
waliovinunua wamevigeuza kuwa maghala ya kuhifadhia korosho na Nchi inaendelea
kupata hasara kubwa kwa kusafirisha korosho ghafi.”
Mheshimiwa
Spika, Baada ya
Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma kutoa tathmini hiyo kama nilivyo inukuu,
ilitoa mapendekezo yake ambayo Bunge hili liliridhia na baadae kuwa ni azimio
rasmi la Bunge, naomba kunukuu azimio hilo la Bunge kama lilivyo kwenye taarifa
ya kamati ya POAC ya 17 April 2012,
“Mheshimiwa Spika, kwa
kuwa katika tathmini yake ya viwanda vilivyobinafsishwa vya ubanguaji Korosho,
imebainika kuwa baadhi ya wawekezaji wamekiuka kwa makusudi mikataba ya
uendeshaji wa Viwanda hivyo, na kwa kuwa kwa kufanya hivyo wamesababisha Taifa
kuendelea kusafirisha korosho ghafi kwenda Nje ya Nchi na hivyo kuondoa fursa
ya wakulima kupata faida ya kutosha na kupunguza ajira Nchini, kwa hiyo Kamati
inapendekeza kuwa Serikali ichukue uamuzi wa kuvirejesha viwanda vyote vya
kubangua Korosho vilivyobinafsishwa na wawekezaji wake kushindwa kuviendeleza
ili kuona namna bora ya kuwekeza kwenye ubanguaji wa korosho ikiwa na pamoja na
Serikali kusisitiza umuhimu wa kuuza Korosho iliyobanguliwa Nje ya Nchi kwa
kuwajengea uwezo wakulima wa kubangua Korosho”.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inataka kupata majibu utekelezaji wa azimio hili umefikia wapi mpaka sasa kwani kutokutekelezwa kwa azimio hili ni kuendelea kuwaumiza wananchi wetu ambao ni wakulima na ambao hawapati pembejeo kwa wakati, dawa na sasa hata bei nzuri hawapati .
N : KAHAWA
Mheshimiwa
Spika, Bodi ya Kahawa
Tanzania (TCB) ni Taasisi ya Umma iliyoundwa kwa sheria ya bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya bodi za mazao namba 23 ya mwaka 2001, pamoja na
majukumu mengine lakini ya msingi yakiwa ni:
• Kusimamia sekta ya kahawa Tanzania
• Kuishauri serikali mambo ya msingi juu ya
mikakati ya kuendeleza
kilimo na biashara ya kahawa
Mheshimiwa
Spika, dira ya bodi
inasema kuwa “Kuwezesha mazingira muafaka kwa maendeleo endelevu ya sekta ya kahawa
nchini Tanzania”. Kwa kadri iwezekekanavyo maendeleo endelevu katika sekta ya kahawa
hayawezi kufikiwa ikiwa bei anayopata mkulima wa Kahawa haiwezi kuzidi gharama
za uzalishaji. Hii ni kudanganyana na kumfanya mkulima aendelee kuwa tegemezi
na maendeleo endelevu kwa sekta hayawezi kupatikana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa bodi hii zao hili la kahawa limeendelea kudidimia
siku hadi siku kutokana na wakulima kukosa pembejeo kama madawa, mbegu bora na
wataalamu wa kutosha .Aidha viwanda vya kubangulia kahawa vilivyojengwa wakati
wa utawala wa Mwl.Nyerere leo hii viko hoi bin taabani.
Kambi ya
Upinzani, inataka kupata majibu kuna mkakati
gani na mpango gani endelevu wa kulifufua zao hili pamoja na viwanda vya
kubangua na kusindika kahawa ili kuliwezesha taifa kupata faida kutokana na
kilimo cha zao hili.
O : PAMBA
Mheshimiwa Spika,
Pamba ni zao kuu la biashara na ni la pili kwa kuingiza fedha za kigeni baada
ya kahawa. Pamba inachangia asilimia 24 ya mauzo yote ya bidhaa za kilimo nje
ya nchi na inachangia asilimia 4 ya mauzo yote nje ya nchi. Takribani
hekta 400,
000 zinatumika kwa ajili ya kilimo cha pamba kwenye wilaya zaidi
ya 40 za mikoa 13 ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa
Spika, Takwimu zinaonyesha kuwa uzalishaji wa zao la
pamba nchini, umeongezeka kutoka kilo milioni 168 msimu wa mwaka 2010/11 hadi
kufikia kilo million 224 katika msimu wa mwaka 2011/12
Mheshimiwa
Spika,
wakati Akiongea
na wawekezaji kutoka Algeria ambao pia ni wafanyabiashara mashuhuri
duniani, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika wakati huo, Mh. Prof. Jumanne Maghembe
alisema “msimu huu uzalishaji wa Pamba umeongezeka kwa kiasi
kikubwa ambacho hakijawahi kutokea kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita”
Kauli hiyo ya waziri
iliongezewa nguvu na Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini, kwa kusema kuwa “ongezeko
hilo limechangiwa na serikali kwa kutoa ruzuku za pembejeo. Aidha alisema pia
kuyumba kwa bei ya pamba ambayo ni kati ya sh 1,100 mpaka sh 800
kwa kilo kunachangia wakulima kutoongeza bidii ya kilimo cha zao hilo”.
Mheshimiwa
Spika, ni ukweli kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha kiasi
kikubwa cha pamba kuliko nchi nyingine zilizopo Kusini na Mashariki mwa Bara la
Afrika. Hivi sasa asilimia 70 ya pamba, inauzwa nje huku viwanda vya ndani
vikitumia asilimia 30. Na matumizi haya ya asilimia 30 siyo kwa ajili ya
kutengeneza nguo bali ni kwa asjili ya kusokota nyuzi kwa ajili ya kupeleka nje
ya nchi. Huu ni uzembe mkubwa au hujuma kwa watanzania jambo linalopelekea
kuendelea kuagiza mitumba toka nje na kuwa nchi ya wachuuzi.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na wakulima wetu kujitahidi kuzalisha kwa wingi kiasi hicho
ambacho kimevunja rekodi ya uzalishaji kwa miaka 50 ila bado bei ya Pamba
imekuwa ni ndogo sana ukilinganisha na uhalisia wa gharama halisi za uzalishaji
kama vile mbegu, madawa na gharama nyingine za uzalishaji wa zao hilo.
PAMBA NA
KILIMO CHA MKATABA
Mheshimiwa
Spika,
kilimo hiki cha mkataba kimekuwa ni sumu kubwa sana kwa wakulima wa Pamba na
hivyo kupelekea wakulima kuona kuwa ni afadhali waachane na kilimo wajihusishe
na shughuli zingine. Ili kilimo hiki kiwe na manufaa kwa mkulima inabidi
uzalishaji kwa hekari uongezeke. Na katika kufikia hilo Ginneries ndizo ziwe na
jukumu la kuhakikisha kuwa matatizo ya mkulima yanatatuliwa, lakini mkataba huo
wa mkulima na hizo Ginneries umwache huru kuuza pamba yake kwa mnunuzi yeyote
atakayetoa bei nzuri, ila imlazimu mkulima kulipa gharama zote zilizotumiwa na
Ginneries katika kumfanya azalishe.
Mheshimiwa
Spika,
katika kuwekeana mikataba inabidi bei dira iwekwe katika mkataba na pia ielezwe kuwa uwepo
uthamanishaji halisi ya nguvu za mkulima katika mchakato mzima wa uzalishaji.
Katika hali hiyo mkataba uwe sawa kwa wakulima walioko kwenye maeneo/ wilaya
moja.
Mheshimiwa
Spika,
wote ni mashuhuda katika mdororo wa uchumi hasara iliyotokea, iliangukia kwa
mkulima na mfanyabiashara alipata fidia toka Serikalini. Hivyo basi Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali pale hasara inapotokea mkulima awe wa kwanza
kupatiwa fidia badala ya mfanyabiashara.
Mheshimiwa
Spika, Hoja sio kuendelea kuongeza ruzuku za PEMBEJEO au bei
za MALIGHAFI Ukifanya marginal analysis (price - unit cost) ya mazao
uliyoorodhesha, utakuta kwamba mkulima anapata kama 12% ya total margin katika
value chain wakati mwenye kiwanda anapata zaidi ya 50%. kwa mazao ambayo
hayaendi viwandani, mkulima hupata kama 30% na mfanyabiashara hupata zaidi ya
60%
Mheshimiwa Spika, Mfano: Leo mkulima wa kule Mwanza anauza
1kg ya pamba kwa Tshs 600/=. Kilo hii inatoa mashati manne na kila shati moja la pamba halisi likiuzwa kwa dolla
50 ni sawa na Tshs 80,000/= Hivyo kwa
kilo moja ni sawa na shilingi 320,000/-. Mwenye kiwanda (mzungu) anatumia Tshs
10,000/= tu kwa kilo kama gharama za ununuzi, usafirishaji (kupeleka pamba
ulaya na kurudisha shati Mwanza) na uchakataji kiwandani. Faida yake ni
Tshs 310,000/= kwa kilo moja. Hata kama angechukua Tshs 10,000/= zingine akatupatia
"msaada" wa kutujengea barabara kutoka Dodoma hadi Mwanza ili
akunyonye vizuri zaidi kwa kupunguza gharama za usafirishaji, bado ana faida ya
Tshs 300,000/[17]=
Mheshimiwa
Spika,
kwa uchambuzi huo, tunaitaka Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Pamba
kujenga kiwanda cha Pamba katika mojawapo ya mikoa inayolima Pamba ambacho
kitakuwa na jukumu la kuongeza thamani ya Pamba yetu.
Kambi ya
Upinzani,
inataka kupata majibu ya kina kuwa serikali ina mpango gani wa kuinua wakulima
wa zao hili muhimu hapa nchini na hasa katika kuwapatia bei nzuri ya Pamba inayoendana
na gharama halisi za uzalishaji wa kilo moja ambayo sasa imekuwa kubwa sana,
wakati inatafakari uanzishwaji wa kiwanda cha Pamba.
P: MIWA
Mheshimiwa Spika, katika uwekezaji
unaotakiwa kufanyika katika mpango wa SAGCOT ni katika sekta ya sukari au
ulimaji wa miwa. Kilimo cha miwa kimetawaliwa na kuhodhiwa kwa kiasi kikubwa na
viwanda vinavyozalisha sukari kwani viwanda hivyo ndivyo vinavyopanga bei na
muda wa kununua miwa toka kwa wakulima wanaozunguka viwanda hivyo. Katika
mchakato huo wa kikiritimba anayeumia ni mkulima. Hoja ni kwa vipi tunamnasua
mkulima katika mtego huo wa wenye viwanda? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali itoe ufumbuzi wa suala hilo.
Mheshimiwa Spika, kanuni zinazowataka
wakulima wanaozunguka kiwanda cha sukari waliondani ya kilometa 40 kutoka
kilipo kiwanda cha sukari wanalazimishwa kuuza miwa yao kwenye kiwanda,
japokuwa kanuni hiyo walidhani wanamsaidia mkulima kusafirisha miwa yake kufika
kiwandani, lakini ukweli ni kwamba ni ujanja wa kuvilinda viwanda na ushindani
unaoweza kujitokeza.
Mheshimiwa Spika, kanuni hii inazidisha
ukiritimba kwa viwanda na kuwanyika haki ya msingi kwa wakulima ambao kwa
kutumia ushirika wao wanauwezo wa kuanzisha kiwanda kikubwa au kidogo cha
kutengeneza sukari. Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuangalia upya kanuni hiyo ili iendane na mazingira
yaliyopo sasa. Aidha, tunaitaka Serikali kupitia SIDO kuanzisha viwanda vidogo
ambavyo vitakuwa na ubia na wazalishaji wadogo wadogo (Cane outgrowers) katika
maeneo mbalimbali yazalishayo miwa hapa nchini. Hii itaondoa tatizo kubwa la
sukari linaloikabili nchi yetu na pia ni njia mojawapo ya kuondoa umasikini wa
kipato kwa wakulima na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Q: MAPITIO YA BAJETI YA KILIMO
Mheshimiwa Spika, Licha ya mabadiliko yaliyotokea katika mfumo wa uchumi katika miaka ya karibuni ambapo sekta za madini, utalii na huduma zimekua kwa kasi Sekta ya Kilimo inatoa mchango mkubwa katika kuwapatia ajira Watanzania zaidi ya asilimia 70 na inachangia wastani wa asilimia 95 ya chakula kinachohitajika nchini. Katika kipindi hicho, Sekta ya Kilimo ilikua kwa wastani wa asilimia 4 na ilichangia asilimia 26 ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa
Spika, toka mwaka 2001/02 bujeti ya kilimo
imekuwa ikiongezeka taratibu mwaka huo mgawo ulikuwa shilingi bilioni 52.1 ,
ambayo ilikuwa sawa na asilimia 3.0 ya bajeti ya mwaka 2001/02, toka hapo
bajeti imekuwa mara dufu hadi kufikia asilimia 7.8 ya bajeti kwa mwaka 2010/11, Lakini kwa mwaka 2011/2012 ilishuka
na kuwa asilimia 6.9.
Mwaka
|
Jumla ya Bajeti ya Kilimo
|
Bajeti ya Serikali
|
% ongezeko/punguzo la bajeti ya kilimo
|
Bajeti ya Kilimo kama % ya Bajeti ya Serikali
|
% ya badiliko la mgawo wa bajeti
|
2001/02
|
52.1
|
1764.7
|
3.0
|
||
2002/03
|
84.5
|
2219.2
|
62.2
|
3.8
|
0.8
|
2003/04
|
148.6
|
2607.2
|
75.9
|
5.7
|
1.9
|
2004/05
|
157.7
|
3347.5
|
6.1
|
4.7
|
-1.0
|
2005/06
|
233.3
|
4035.1
|
48.0
|
5.8
|
1.1
|
2006/07
|
276.6
|
4788.5
|
18.5
|
5.8
|
0.0
|
2007/08
|
372.4
|
6000.0
|
34.6
|
6.2
|
0.4
|
2008/09
|
440.1
|
7216.1
|
18.2
|
6.1
|
-0.1
|
2009/10
|
666.9
|
9500.0
|
34.0
|
7.0
|
0.9
|
2010/11
|
903.8
|
11610.0
|
26.2
|
7.8
|
0.8
|
2011/12
|
926.0
|
13500.0
|
2.7
|
6.9
|
-0.9
|
Chanzo:Idara
ya takwimu ya wizara ya kilimo,chakula na ushirika
Mheshimiwa Spika,Takwimu zinaonyesha kuwa kwa kipindi hicho cha 2001/02 -2012/13
kumekuwa na uhusiano usiorodhisha kati ya bajeti ya maendeleo na bajeti ya
matumizi ya kawaida. Bajeti ya matumizi ya kawaida imekuwa ikiongezeka wakati
ile ya maendeleo imekuwa ikishuka, kwa mfano kwa mwaka 2001/02 bajeti ya
matumizi ya kawaida ilikuwa asilimia 39.5 ya bajeti nzima ya wizara na mwaka
2008/09 ilipanda hadi kufikia asilimia 82.4 na mwaka 2011/12 ilipungua na kuwa
asilimia 59.0.Wakati bajeti ya maendeleo mwaka 2001/02 ilikuwa asilimia 60.5 na
mwaka 2011/12 ilishuka hadi kufikia asilimia41.0.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, kwa tafakuri ya takwimu hizo inaona ni
wazi kuwa Serikali haina nia ya dhati ya
kuwekeza katika kilimo kwani hata bajeti inayokwenda kwenye wizara sehemu kubwa
ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida tu.
Mheshimiwa Spika, mbali na kupanda na kushuka kwa bajeti inayotengwa kwa kilimo hapa
nchini bado kuna tatizo la utoaji wa fedha pungufu kulinganisha na zile
zinazopitishwa na Bunge.
Jedwali lifuatalo linaonyesha Fedha zilizopitishwa na fedha
zilizotolewa
Mwaka
|
Fedha zilizopitishwa
(TSh. Billion)
|
Fedha zilizotolewa
(TSh. Billion)
|
Upungufu
|
% ya Upungufu kwenye zilizopitishwa
|
2000/01
|
26.1
|
13.3
|
-12.8
|
-49
|
2001/02
|
25.5
|
23.4
|
-2.1
|
-8
|
2002/03
|
34.8
|
30.2
|
-4.6
|
-13
|
2003/04
|
73.0
|
60.4
|
-12.6
|
-17
|
2005/06
|
133.5
|
97.4
|
-36.1
|
-27
|
2006/07
|
122.2
|
86.3
|
-35.9
|
-29
|
2007/08
|
131.9
|
124.1
|
-7.8
|
-6
|
Chanzo: Takwimu za Wizara ya Kilimo na Ukokotoaji binafsi
Mheshimiwa Spika, aidha takwimu
zinaonyesha kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 kwa upande fedha
za ASDP. Hazina ilitoa Shilingi bilioni 107.1 kwa wizara zinazojihusisha na
kilimo (Agriculture Sector Lead Ministries) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
ya maendeleo ya sekta ya kilimo. Lakini kati ya fedha hizo, ni kiasi cha
shilingi bilioni 77.9 (72.8%) ndizo zilizotumika hadi mwisho wa mwaka huo wa
fedha.
Mheshimiwa Spika, Hii maana yake nini
kwa nchi ambayo mara zote taarifa zinatolewa kuwa miradi imekwama kutokana na
ukosefu wa fedha, ni dhahiri kuwa inawezekana tatizo la utoaji wa fedha za
miradi nje ya muda bado linaendelea pia uwezo mdogo wa watendaji katika
utumiaji wa fedha. Ujumla wa haya yote ni kukifanya kilimo kuendelea kudumaa na
kushindwa kutoa tija inayokusudiwa.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inasema kama mipango hiyo ipo tayari kwenye
makaratasi tatizo ni utekelezaji. Serikali ya CCM haiwezi kutekeleza mipango
hiyo kwani imekuwa ikifanya hivyo siku zote. Naomba kunukuu kauli
iliyokwishatolewa hapa Bungeni kwamba “insanity
is keeping doing the same thing expecting different results”
Mheshimiwa Spika, ukuaji wa miji kimekuwa ni kichocheo
kikubwa cha mchakato wa maendeleo kutokana na uwepo wa “forward and backward linkages”
kwa bidhaa nyingi za kilimo na viwandani. Njia hii imekuwa na mafanikio makubwa
kwa nchi nyingi hasa zile zilizoendelea ikiwemo China na Korea ya Kusini na
nyingine kama vile India,Thailand zimejikwamua kutoka kwenye umasikini wa
kipato kupitia ukuaji wa miji midogo[18].
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia upya sera ya
kilimo ili iweke mazingira wezeshi kwa wakulima wadogo waweze kunufaika na
kukua na kuwa wakulima wakubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yalikubaliwa na
wakuu wa nchi mbalimbali duniani Septemba mwaka 2000, kwamba Mwaka 2015 ni tarehe ya mwisho ya kufikiwa
kwa malengo nane ambayo pamoja na mambo mengine, yanalenga katika, kuondosha
umasikini wa kipato na njaa lengo linalohusu moja kwa moja sekta hii ya kilimo.
Ukweli ni kwamba hata kipindi cha kukamilika kwa Malengo ya Maendeleo
kingeongezwa, ni dhahiri tusingeweza kuondoa umasikini wa kipato na njaa
kutokana na kushindwa kutambua kiini hasa cha matatizo ya wakulima na kilimo.
Mheshimiwa Spika, Maendeleo
ya Nchi ya Thailand katika kupambana na kuushinda umasikini halikuwa jambo
rahisi na la siku moja, bali ni matokeo ya uwekezaji makini na nia thabiti ya
kisiasa ambayo ilichangiwa na mambo mengi ikiwemo uwekezaji wa nishati
vijijini. Asilimia 97 ya wananchi waishio vijijini Thailand wanapata umeme wa
uhakika, jambo hili linaenda sambamba na uzalishaji kwenye sekta ya kilimo
wenye tija.
Mheshimiwa
Spika, Ni kwa namna
gani Tanzania tunaweza kufanya ulinganisho na wenzetu hao? Takwimu za bajeti ya kazi toleo la mwaka 2007
zinaonyesha kuwa ni asilimia 2.5 tu ya watanzania waishio vijijini ndio
waliounganishwa na gridi ya taifa[19].
Aidha, Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri
wakati alipokuwa anazungumza na watanzania waishio Nchini Uingereza alisema
kuwa “Asilimia 18.4 ndio wanaotumia umeme hapa Tanzania na kati ya hao ni
asilimia 6.6 tu wako vijijini. Sambamba na hilo, kwa mujibu wa mtandao wa
Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuwa “hapa nchini takriban asilimia 14 tu ya
Watanzania ndio wanaotumia nishati ya umeme na kwamba hali ni mbaya zaidi
vijijini wanakoishi takriban asilimia 80 ya Watanzania ambapo ni asilimia 2.5
tu ndio wanaotumia umeme kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa wananchi wakati
upatikanaji wa nishati hizo nao hautoshelezi’.
Mheshimiwa Spika, Akiwakilisha
bajeti ya mwaka wa fedha 2009/2010 yenye kaulimbiu "Kilimo Kwanza",
Waziri wa Fedha wakati huo, Mhe. Mustafa Haidi Mkulo alisema "Misingi
na shabaha ya bajeti hii imezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo
inalenga kuwa Tanzania iwe ni nchi yenye kiwango cha kati cha mapato… na hali
bora ya maisha kwa wananchi, ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka
2005, MKUKUTA, Mpango Maalum wa Maendeleo Tanzania…na Malengo ya Maendeleo ya
Milenia," alisema Waziri Mkulo.
"Hatua zitachukuliwa kuhakikisha kuwa kilimo kinapatiwa rasilimali zaidi ikiwemo pembejeo na zana za kilimo".
"Hatua zitachukuliwa kuhakikisha kuwa kilimo kinapatiwa rasilimali zaidi ikiwemo pembejeo na zana za kilimo".
Mheshimiwa Spika, Kauli mbiu
ya kilimo kwanza ambayo ni mwendelezo wa Sera ya Kilimo ya mwaka 1997
imeonyesha na inaelekea kushindwa kukidhi malengo kutokana na ukweli kama ulivyotolewa
na Mkurugenzi mtendaji wa SAGCOT katika mahojiano yake na Gazeti la Kiingereza
la Business Times kuhusiana na mada ya faida na hasara za Kilimo kwanza alisema na nukuu ‘It is
true the Kilimo Kwanza initiative will bring fundamental changes in Tanzania,
but this cannot happen overnight; there is a need to wait for other
developments to support it, such as infrastructure, rural electrification and
construction of enough warehouses, good market system for agricultural products[20]’. Kwa tafisiri isiyo rasmi kuwa ni ukweli kwamba mpango wa kilimo kwanza
utaleta mabadiliko ya msingi hapa Tanzania, lakini jambo hili halitatokea
ghafla, hivyo ni muhimu kuwa na maendeleo mengine ya kusaidia mpango huu kama
vile miundombinu,nishati ya umeme vijijini,ujenzi wa nyumba za kutosha, mifumo
mizuri ya masoko kwa ajili ya mazao ya kilimo
Mheshimiwa Spika, kwa mtazamo
huo na ukweli huo hadi kupatikane maendeleo kwenye sekta hizo wezeshi
itatuchukua miaka mingine mingapi?
Mheshimiwa Spika, toka wakati
huo hadi sasa watanzania hawaoni tofauti katika kilimo na kuna wanaoona kwamba
kilimo kimeshuka kwa kulinganisha na miaka ya nyuma. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali kuangalia jinsi ya kuendeleza shughuli mbalimbali zisizokuwa
za kilimo (non farm activities)
zinazofanywa na wakazi wa vijijini, ili kusaida kukuza hali ya kibiashara
katika maeneo ya vijijini.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Kwa
unyenyekevu mkubwa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema na
fadhila kwa kunijalia uhai, afya njema na kwa upendo wake anaotujalia kila
mmoja wetu kwa nafasi yake.
Mheshimiwa Spika, kwa namna
ya kipekee napenda kumshukuru Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Mwenyekiti wa
Chama makini cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Makamanda wenzangu wote
kwa mchakato wa mwanzo wa kuifungua nchi yetu kwa kurudisha madaraka ya
kiutendaji kwa wananchi kupitia M4C.
Mheshimiwa Spika, kama
sitowashukuru wananchi wa Wilaya ya Hanang’ nitakuwa sijawatendea haki kwa
ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika kuhakikisha Wilaya yetu inakuwa kiongozi
katika kupambana na ufisadi katika miradi ya maji na ile ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, mwisho
lakini kwa umuhimu mkubwa ni kwa familia yangu hasa wanangu Emiliana na Linus.
Nasema tuendelee kuvumiliana kwa kipindi chote nitakachokuwa kwenye uhamasishaji
wa M4C.
Mheshimiwa
Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya
Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
……………………………….
Rose
K.Sukum(Mb)
Msemaji
Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
22.04.2013
[2]Ibid.
[3]http://savingaplanetatrisk.org/links-farmer-suicides-to-monsanto/
"Climate change and the global food shortage crisis could end civilization as we know it today."
"Climate change and the global food shortage crisis could end civilization as we know it today."
[4] Feedback and
recommendations from Civil Society Organisations for the “Greenprint” strategy
of the Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania Initiative
[5] Philippe
Egger, Director of the ILO Bureau of
Programming and Management
[6] Gazeti la Serikali la
Habari leo la 14 Januari 2013
[8] Wizara ya Kilimo na Ushirika-Maendeleo ya Kilimo na Ushirika kwa
Kipindi cha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara (1961-2011)
[10] Analysis of Agriculture Budget Trends
and Outcomes in Tanzania, by Dr. Damian M. Gabagambi of Sokoine University of Agriculture
and Ms. Magreth Henjewele
[11] USHIRIKA
TANZANIA, kimetungwa na Pius Ngeze
[12]
DR Anaclet Kashuliza, Katibu
Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi,Ufunguzi wa mkutano
wa 19 wa SCCULT, SHINYANGA, 26 FEBRUARI 2012
[13] Teknolojia
za Utayarishaji, Usindikaji na Hifadhi ya Mazao ya Nafaka baada ya Kuvuna. Kitabu namba 1
[14] Agribusiness innovation in six african countries, The
tanzanian experience, report prepared for the world bank institute. By Dr.
J. J. Mpagalile, Prof. R. Ishengoma and Prof. P. Gillah Sokoine University of
Agriculture P. O. Box 3000 Chuo Kikuu, Morogoro, Tanzania
[15] Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania Appendix IV: Value
Chain and Market Analysis
[16] http://www.commodityonline.com/news/vietnam-cashew-nut-export-revenue-soars-37338-3-37339.html
[17] Nganga N. B mtafiti na mchambuzi mshauri masuala ya Pamba
[18] http://www.worldbank.org/tanzania/economicupdate.
[19] Reducing Poverty through Kilimo kwanza : What can we learn from
the East ?y through
CHANZO: MTANDAO WA KIJAMII WA CHADEMA.