Saturday, September 26, 2015
Tuesday, September 22, 2015
Wednesday, August 26, 2015
Monday, August 24, 2015
Thursday, August 20, 2015
CHADEMA YAZUIWA KUTUMIA UWANJA WA TAIFA.
POSTED THURSDAY, AUGUST 20, 2015 | BY- JULIUS MATHIAS
Serikali imekataa ombi la Chadema la kutumia Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuzindua kampeni zake Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Serikali imekataa ombi la Chadema la kutumia Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuzindua kampeni zake za uchaguzi, ikisema mazingira yaliyopo sasa hayaruhusu eneo hilo kutumika kwa shughuli za kisiasa. Serikali imetangaza uamuzi huo ikiwa ni siku tatu kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani kwa ajili ya Uchaguzi utakaofanyika Oktoba 25. Juzi, kwenye mitandao ya jamii kulienea habari kuwa Chadema, ambayo mgombea wake wa urais, Edward Lowassa amekuwa akivuta maelfu ya watu kwenye mikutano yake, imepanga kutumia uwanja huo unaoweza kuchukua watu 60,000 waliokaa kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni zake Agosti 22. Hata hivyo, Chadema imeshakanusha taarifa kuwa itazindua kampeni zake Agosti 22. Akizungumza na vyombo vya habari jijini jana, Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Assah Mwambene alisema Serikali haijatoa ruhusa kwa chama chochote cha siasa kuutumia Uwanja wa Taifa kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kwamba hakuna chama kitakachoruhusiwa kufanya hivyo. “Tulipata barua ya Chadema kuomba kutumia Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuzindua kampeni zao, tayari tumeshawaandikia kuwaarifu kuwa uwanja ule hauwezi kutumika kwa ajili ya shughuli zozote za kisiasa,” alisema Mwambene. Alieleza kuwa Serikali imeamua kwamba uwanja huo uendelee kutumika kwa shughuli za kimichezo ili kuepuka mihemko na athari yoyote inayoweza kujitokeza kutokana na hamasa za kisiasa. “Uamuzi huu unalenga kuweka uwanja katika mazingira rafiki ya michezo na kuepuka athari zozote zinazoweza kujitokeza,” alisema Mwambene. Akizungumzia uamuzi huo, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema kilichofanywa na Serikali hakijaathiri chochote kwenye maandalizi ya harakati za chama hicho kufanya uzinduzi wa kishindo ili kukidhi matarajio ya Watanzania wanaokiunga mkono. Alisema kilichotangazwa na Mwambene kimetokana na uelewa mdogo wa masuala ya demokrasia na masuala makubwa yenye mvuto wa kitaifa na kufafanua kuwa viwanja hivyo hutumika sehemu nyingi duniani kwa kuwa kampeni ni sehemu pekee ambayo wananchi wanapata nafasi ya kuwahoji wagombea kabla hawajawapa ridhaa ya kuwatumikia. “Mwambene haelewi anachokisema. Anatumika kufunika aibu ya CCM ambayo imeona mvuto wake unaendelea kushuka kila siku. Hivyo hawana uhakika wa kujaza wafuasi kwenye eneo kubwa kama lile,” alisema. “Kwa sasa ni Chadema pekee ndiyo inayoweza kuutumia uwanja ule, ndiyo maana CCM wamekimbilia viwanja vya Jangwani ambavyo kwa sasa ni vidogo kutokana na ujenzi wa vibanda vya biashara uliofanyika,” alisema Makene. Alieleza kuwa CCM inatishwa na wingi wa watu wanaojitokeza kuiunga mkono Chadema baada ya kujionea maelfu ya watu wanaoambatana na mgombea wake wa urais hasa kwa kipindi cha kuomba udhamini mikoani. “Tumekuwa tukiambatana na watu wengi sana ambao wamejitolea kuungana nasi kila tunapokwenda. Tunajipanga kufanya uzinduzi mkubwa eneo jingine na hii inaweza isifanyike Agosti 22, kila chama kinaweza kikaanza siku kinachoona inafaa kwake,” alisema.