LOUIS van Gaal amefanikiwa kuchukua kombe la mashindano ya kimataifa ya Guinness nchini Marekani kufuatia Manchester United kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya mahasimu wao wakubwa, Liverpool katika mchezo wa fainali uliomalizika usiku wa jana mjini Miami.
Japokuwa kombe hilo sio kubwa kwasababu ni kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, lakini ni heshima kwa Van Gaal na sasa itamuongezea imani kuelekea msimu mpya wa ligi kuu soka nchini England inayotarajia kuanza Agosti 16 mwaka huu.
Katika mchezo wa jana, Liverpool walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza katika dakika ya 14 kwa mkwaju wa penalti uliofungwa na Steven Gerrard.
Bao hilo lilidumu mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakatika, lakini kipindi cha pili katika dakika ya 55, mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney alisawazisha bao hilo.