Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi (kulia) akizungumza kwenye mdahalo wa Katiba, uliofanyika Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi |
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na wajumbe wa tume hiyo, jana walitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali kuhusu mchakato wa Katiba katika mjadala uliofanyika hapa kiasi cha kuwafanya waliohudhuria siyo tu kumshangilia, bali walimsindikiza hadi alipoingia kwenye gari lake na wakilifuata na kulisukuma.
Jaji Warioba na wajumbe wenzake, Profesa Palamagamba Kabudi, Joseph Butiku, Hamphrey Polepole, Mwantumu Malale na Awadh Ali Said walitoa ufafanuzi huo katika mdahalo la Katiba lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere jana.
Jaji Warioba ndiye alianza kuzungumza kwa kukanusha madai yaliyotolewa juzi katika mdahalo mwingine, kuwa amepeleka maoni mapya serikalini.
Alisema madai hayo hayana ukweli bali maoni aliyowasilisha serikalini yalitokana na maoni ya wananchi waliyokusanya wakati wakiandaa Rasimu ya Kwanza ya Katiba ambayo yataweza kusaidia katika kuandaa Katiba ya Tanganyika.