|
Mwadhamu Polycarp Kardinali Pengo |
Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kile
alichosema kwamba limeshindwa kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani na
mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Kiongozi huyo akiongelea
upepelezi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Zanzibar aliyepigwa risasi
mwezi uliopita alisema, “Siwezi kusema naridhika au siridhiki
lakini tulitegema kwamba polisi wangetegua kitendawili cha wauaji wa
padri huyo.”
|
Mazishi ya Padre Evarist Mushi. |
Kardinali Pengo alisema Serikali haipaswi
kusema wanaovuruga amani ni wahuni wakati hilo ni jukumu lake
kuhakikisha inadumisha amani. Pengo alikuwa akizungumza na waandishi wa
habari jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za Pasaka.
“Watu wanaharibiwa mali zao, watu wanapoteza
uhai wao, Serikali haiwezi kukaa pembeni na kufikiri ni kauli za
viongozi wa dini peke yao, viongozi wa dini hawana jeshi au hawawezi
kukamata watu, Serikali ndiyo wana jukumu hilo kuhakikisha wanaingilia
kati,” alisema Pengo na kuongeza:
“Wengine wanasema si mapambano ya dini ya
Kikristu na Waislamu ila ni wahuni wachache wanajichukulia madaraka,
lakini lolote liwavyo Serikali haiwezi kukwepa majukumu yake, hatuwezi
kutegemea nchi itawaliwe na wahuni kama vile Serikali haipo.”
Kuhusu Padri Mushi aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kwenda kwenye misa huko Zanzibar, Pengo alisema:
“Watanzania tungeambiwa zimechukuliwa hatua zipi na aliyehusika na mauaji hayo ni nani, lakini hali inayoonekana sasa hatujui.”
Aliongeza:
“Siyo mimi wala Askofu wa Zanzibar (Augostino Shao) au askofu yeyote
anaweza kukwambia kuwa kuna mtu amekamatwa, ila inaonekana kama mambo
yanataka kuisha kimyakimya na kufanya hivyo haiwezi kuwa chimbuko la
amani.”
Kardinali Pengo alisema vyombo vya kulinda amani vinapokuwa
chimbuko la kuharibu amani kwa vyovyote nchi yoyote duniani haiwezi
kuendelea.
Alisema kunahitajika kukutanishwa kwa pande zote mbili za
Wakristu na Waislamu, lakini akatoa angalizo kwa kubainisha mambo mawili
ambayo yanahitajika kuzingatiwa ili kufikia mwafaka.
Alisema pande zote mbili watu wakitaka
kujadiliana ni lazima kila upande uwe tayari kujadiliana na kupokea
ukweli sambamba na kusema ukweli na siyo kupotosha ukweli kwa masilahi
binafsi.
“Pili kila upande uwe na mawazo kwamba upande
wa pili una nia njema, lazima watu wawe tayari kuwasiliana kuwa upande
wa pili una nia njema, lakini kinyume na hapo itakuwa bure na
kudanganyana na mambo yataendelea kuwa mabaya zaidi,” alisema Kardinali
Pengo.
Kuhusu kuwapo kwa taarifa kwamba katika mkesha wa Pasaka kuna
watu watafanya vurugu, alisema haogopi kwani vyombo vya usalama vina
jukumu la kuhakikisha raia wanakuwa salama.
|
IGP Said Mwema |
“Mimi kazi yangu si kujiandaa kushika bunduki kwani Serikali wana jukumu la kulinda amani iwe kanisani au msikitini.
“Wanatakiwa
kuchukulia mazungumzo hayo ‘serious’ (makini) kwani baada ya Padri
Ambrose kujeruhiwa kwa risasi walisema wataendelea na kweli ikatokea
Padri Mushi akauawa. Mimi sitaacha kwenda kanisani hata kama nitaambiwa
nitauawa na kama kufa nife katika kanisa langu,” alisema.
Kauli ya Polisi
|
Advera Senso Msemaji Mkuu wa Polisi
|
Msemaji
Mkuu wa Polisi, Advera Senso alisema upelelezi wa tukio la kifo cha
Padri Mushi unaedelea na kuwaomba wananchi kusubiri kujua
kinachoendelea.
“Kunapotokea tukio la aina yoyote lile polisi ndiyo
jukumu lao kujua chanzo na hatua za kuchukua. Tunaomba watu tuwaachie
wanaohusika ili kuweza kufanya kazi hiyo vizuri na tutawaeleza
kinachoendelea upelelezi utakapokamilika,” alisema Senso.
Kuhusu uvumi wa matukio ya uhalifu wakati wa Pasaka, Senso alisema wanafuatilia taarifa hizo.
“Tunawaomba
wananchi ambao wanajua ni kina nani wanaeneza taarifa hizo, watupe
ushirikiano ili tuwachukulie hatua kutokana na kutoa taarifa za
kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisema Senso.
Pia Novemba
mwaka jana, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhili Soraga alimwagiwa
Tindikali na watu wasiojulika wakati akifanya mazoezi kwenye Viwanja vya
Mwanakwerekwe.
Mapema mwezi ulipita, Mchungaji wa Kanisa la
Pentekoste Assemblies of God (TAG) mkoani Geita, Mathayo Kachila aliuawa
katika ugomvi wa kugombea kuchinja, katika tukio ambalo watu sita
walijeruhiwa vibaya kwa mapanga.
Habari hii ni kwa hisani ya Mwananchi,Alhamisi, Machi 28,2013