Wakati nauli mpya zikianza kutumika leo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu
(Sumatra) imekamata magari ya kubeba abiria (daladala) 75 katika
operesheni maalum iliyoanza mwanzoni mwa wiki hii katika mikoa ya Dar es Salaam
na Pwani.
Uamuzi wa kukamata magari hayo umekuja baada
ya kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya abiria ya kutozwa nauli
kubwa kuliko iliyotangazwa na Serikali kuwa zianze kutumika leo.
Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe alisema
jana mjini Dodoma kuwa ongezeko la viwango vipya vya nauli si tatizo,
la muhimu ni wahusika kufuata vigezo.
Akizungumza jijini Dar
es Salaam jana, Ofisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki wa Sumatra, Conrad
Shio alisema kuwa,daladala zilizokamatwa zilikuwa na makosa mbalimbali
yakiwemo kukatisha ruti, kutoza nauli, kuiba ruti na kufanya biashara ya
kusafirisha abiria bila ya kuwa na kibali.
Alisema kutokana na hali hiyo wamiliki wa
daladala zilizokamatwa wametakiwa kwenda na mikataba ya madereva wapya,
ili wale wa zamani waweze kukaguliwa na Jeshi la Polisi Tanzania juu ya
uhalali wa leseni zao.
“Tumepata malalamiko ya daladala 105 ambazo
zimekuwa zikivunja sheria ya usafiri barabarani, ambapo daladala 75
tayari tumezikamata,” alisema Shio.
Aliongeza kati ya hizo, daladala
36 zilikatisha ruti, wakati 18 ziliiba ruti na 21 zilitoza nauli kubwa,
jambo ambalo limewafanya wazichukulie hatua.
Alisema kuna nyingine zimebeba abiria bila ya kuwa na kibali, ambapo wamiliki wake wamechukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kutokana na hali hiyo, wamiliki wa
daladala hizo wametakiwa kulipa faini na kwenda na mikataba ya madereva
wapya ili madereva waliofanya makosa wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa
ni pamoja na kuwafikisha mahakamani. Alisema daladala ambazo zilikuwa
zinafanya kazi bila ya kibali hasa nyakati za usiku katika baadhi ya
maeneo zimepelekwa kwenye yadi ya Serikali ili wamiliki wake waweze
kuchukuliwa hatua za kisheria kwa sababu ni kosa kubeba abiria wakati
huna kibali cha usafirishaji.
Alisema kuwa, ili kupunguza ukubwa wa tatizo,
wamelifanya zoezi hilo kuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kuwataka
madereva wa vyombo vya usafiri kufuata sheria na taratibu zilizowekwa
ili kupunguza malalamiko. Alisema kutokana na hali hiyo Sumatra
itaendelea kukamata magari ambayo yataonekana yanaendelea kuvunja sheria
kwa makusudi.
Habari hii ni kwa mujibu wa Mwananchi