Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakionesha eneo lililoainishwa na kufanyiwa tathmini kwa ajili ya kazi ya utanuzi wa Kiwanja hicho. |
Na Saidi Mkabakuli, Kigoma
Serikali imeazimia kuanza kufanya utanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kigoma ili kuweza kukidhi mahitaji yanaongeza siku baada ya siku ya kiwanja hicho.
Azma imetolewa na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma.
Bibi Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini ipo kwenye mkakati wa kuuendeleza uwanja huo ili uwe wa kiwango kizuri kwa kuhudumia watumiaji wa wa kiwanja hicho.
“Kama munavyokumbuka Serikali katika mwaka ujao wa fedha imepanga kuendeleza na kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi; na kuendelea na kazi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege katika maeneo ya kimkakati ikiwamo Kiwanja cha Ndege cha Kigoma,” alisema.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya uwanja huo, Meneja Mradi wa Utanuzi wa Kiwanja cha Kigoma, Mhandisi Neema Mwasha alisema kuwa mpaka sasaMamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini imekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa usalama na eneo la maegesho ya ndege.
“Kwa sasa tunaendelea na kazi ya utayarishaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kazi za ujenzi wa barabara ya kuingia kiwanjani, maegesho ya magari, na usanifu wa kina kwa ajili ya upanuzi wa maegesho ya ndege pamoja na usimikaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege,” alisema.
Mhandisi Neema aliongeza kuwa wapo kwenye mchakato wa kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya usanifu wa jengo la abiria uwanjani hapo.
Naye Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege Kigoma, Bw. Joseph Nyahende alisema kuwa katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa wakati, Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini kwa kushirikiana na Mkoa wa Kigoma vimeainisha na kufanyia tathmini eneo litakalotumika kwa ajili ya kazi hiyo.
Sehemu ya Kiwanja cha Ndege Kigoma ikiwa imekamilika kwa kiwango cha lami. |
Meneja Mradi wa Utanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kigoma, Mhandisi Neema Mwasha (Wapili kulia) akionesha eneo likaloboreshwa katika Mradi wa Utanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma. |
PICHA ZOTE NA SAIDI MKABAKULI
No comments:
Post a Comment