Na Saidi Mkabakuli
Katika kutekeleza mkakati wa kutembelea na kukagua utendaji kazi wa vitengo vya mawasiliano serikalini, Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Bw. Assah Mwambene leo ametembelea Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, pia kuzungumza na Mtendaji Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Philip Mpango.
Akiwa katika ziara hiyo, Bw. Mwambene ambaye ndiye Msimamizi Mkuu masuala ya Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Serikali amesema kuwa vitengo vya mawasiliano serikali vina jukumu kubwa ya kuuelimisha umma wa Watanzania juu ya masuala mbalimbali yanayojiri kwenye ofisi zao.
“Tumieni utaalamu wenu kwa kuwapatia taarifa sahihi na kwa wakati Watanzania ili kuweza kutoa suluhu ya masuala mbalimbali ambayo munaweza kuyajibu,” alisema.
Akizungumza wakati alipokutana na Msemaji Mkuu wa Serikali, Katibu Mtendaji wa Ofisi hiyo, Dkt. Philip Mpango, alimpongeza na kumshukuru Bw. Mwambene kwa kutenga muda na kutembelea Tume ya Mipango, ambayo ndiyo Washauri Wakuu wa Serikali katika menejimenti ya uchumi na masuala ya maendeleo.
Dkt. Mpango aliweka bayana mkakati wa Ofisi yake wa kuwafikia Watanzania wote bila kujali maeneo yao ya kijiografia kwa kuwaelimisha juu ya mipango mbalimbali ya serikali yenye dhamira ya dhati katika kuwavusha katika umaskini miongoni mwao.
“Tuna mkakati wa kuwafikia na kuwaelimisha Watanzania juu ya masuala ya mipango na maendeleo, na naomba kuchukua fursa hii kuiomba Ofisi yako kutuunga mkono katika hili ili kuweza kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo (TDV) 2025,” alisema Dkt. Mpango.
Kwa mujibu wa TDV 2025 ni kuivusha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment