Mgeni Rasmi Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mh.Amir Nondo |
Kila mwaka Wizara ya maji huadhimisha
wiki ya maji nchini kote kuanzia tarehe 16-22, Machi. Katika kipindi hiki cha
maadhimisho haya Mamlaka za maji nchini hufanya kazi mbali mbali ikiwa ni
pamoja na kufanya mikutano na wadau wa maji,kusafisha mazingira, kuhamasisha
wananchi katika kulinda na kutunza vyanzo vya maji, maadhimisho haya pia
hulenga katika kuwaelimisha wananchi kuhusu sera ya taifa ya maji na mikakati yake
ya utekelezaji.
Mkurugenzi mtendaji wa MORUWASA akimueleza Mh.Meya jinsi ya mto Mlali ulivyovamiwa na kuendelea kulima mdani ya mto. |
Kwa kipindi cha miaka 25 sasa
Tanzania imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Maji kila mwaka. Chimbuko la Maadhimisho
ya Wiki ya Maji Kitaifa ni Azimio la Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wahandisi wa Maji
uliofanyika Mkoani Shinyanga Mwaka 1987. Aidha, mwaka 1992 Mkutano Mkuu wa
Umoja wa Mataifa ulipitisha Azimio Na. 47/193 kuwa tarehe 22 Machi ya kila
mwaka, nchi wanachama waadhimishe Siku ya Maji Duniani, ambayo ni Kilele cha
Wiki ya Maji.
Msitahiki Meya wa manispaa ya Morogoro akiongea na wakazi wa Mlali pamoja na watumishi wa MORUWASA na Bonde la Wami/Ruvu. |
KAULIMBIU YA MAADHIMISHO
Maadhimisho haya huwa na kaulimbiu tofauti
mwaka hadi mwaka. Kaulimbiu ya Wiki ya Maji kwa mwaka huu ni “Uhakika
wa Maji na Nishati”. Kaulimbiu hii imetokana na kaulimbiu ya Siku ya Maji
Duniani ambayo ni “Water and Energy”.
Ujumbe huu unaweka mkazo ili kuona umuhimu wa Maji na Nishati kwa pamoja. Maji
na Nishati ni rasilimali zenye umuhimu sana kwa maisha ya binadamu, huduma za
Maji na Nishati zinategemeana sana, kutokana na uhusiano uliopo kati ya
rasilimali maji na uzalishaji wa nishati, kwa upande mmoja maji yanategemea
nishati ili yasafirishwe kwenda maeneo mbalimbali katika mfumo kuanzia kwenye
chanzo, kupitia mitambo ya kusukuma na kusafirisha hadi hapo yanapomfikia
mtumiaji. Katika upande mwingine upatikanaji wa Nishati unategemea kuwapo kwa
maji ya uhakika katika uzalishaji.
Ili kwenda sambamba na kaulimbiu
katika kuadhimisha wiki ya maji , MORUWASA imeamua kwa kushirikiana na Ofisi ya
Bonde la Wami/Ruvu kuweka mipaka katika vyanzo vya maji hasa mito inayoingiza
maji katika bwawa la Mindu kwa kupanda Mikatani kuanzia kwenye chanzo cha mito
hiyo huko milimani hadi bwawa la Mindu.
Aidha, MORUWASA itatembelea wateja
wake katika Manispaa ya Morogoro ili kuwahamasisha na kuwaelimisha kuhusu Hali
halisi ya upatikanaji wa huduma ya majisafi katika maeneo yao na majitaka kwa
ujumla.
Wananchi wa Mlali waliokutwa wakifua nguo katika mto Mlali.
UMUHIMU WA UTUNZAJI WA MAZINGIRA KATIKA VYANZO VYA MAJI
|
Kama tunavyofahamu kuwa MAJI NI
UHAI, ni jambo la muhimu kusisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuifanya
huduma ya maji kuwa endelevu. MORUWASA inawaomba na kuwashauri wananchi wote
kuachana na vitendo vya kuharibu mazingira kwa kuchoma moto, kulima kwenye
miteremko mikali bila ya kuzingatia utaalam wa kilimo cha miinuko na kuacha
kabisa uchimbaji wa dhahabu na kokoto kandokando ya mito.
No comments:
Post a Comment