Na
Saidi Mkabakuli
Maendeleo ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara
hadi Dar es Salaam unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu
kufuatia kuendelea vyema kasi ya kundaza bomba hilo.
Wakizungumza na wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Wahandisi wa Ujenzi kutoka Shirika la Mafuta
Tanzania (TPDC), Mhandisi Mwita Yagela na Mhandisi Omary Kitiku wamesema kuwa kasi ya sasa ya
ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo kijiji cha Madimba, mkoani
Mtwara inatia moyo na hivyo kuashiria kukamilika kwa mchakato huo kwa wakati.
“Mpaka sasa jumla ya kilomita 350 kati ya kilomita 492 za bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam zimeshatandazwa hali inayokwenda sambamba na mpangokazi wa ujenzi wa kiwanda hiki,” alisema Mhandisi Yagela.
Kwa mujibu wa Mpangokazi wa ujenzi wa kiwanda hiko
hadi kufikia mwisho wa Julai kiwanda kinatakiwa kukamilika, na mpaka sasa,
makazi ya wafanyakazi imekamilika.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mmoja wa
viongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya
Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri alisema
kwamba kukamilika kwa bomba hilo kunatoa mwanya wa kukamilika kwa wakati
uzalishaji wa umeme katika vituo vya Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.
“Kukamilika kwa bomba hili kunatoa fursa ya kwa
Mradi wa kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 150 na Megawati 240 kwa kutumia gesi asilia vilivyopo Kinyerezi,
jijini Dar es Salaam,” alisema Bibi Mwanri.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16), Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa
uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya nishati ambapo nguvu kubwa imewekwa
katika uwekezaji wa miundombinu ya nishati ambapo utekelezaji wa ujenzi wa
bomba la gesi Mtwara hadi Dar es Salaam unafanywa sambamba na ujenzi wa mitambo
miwili ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi katika eneo la Kinyerezi Dar es
Salaam.
Serikali imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2011/12 -2015/16) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo
kuu la Mpango huu ni kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka
misingi ya ukuaji mpana wa uchumi na unaolenga watu walio masikini zaidi.
Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja wa
mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa utekelezaji na
kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya
maendeleo kitaifa.
Lengo la Dira ni kuibadili
Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais ikijionea maendeleo
ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba, mkoani Mtwara.
|
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa makazi ya wafanyakazi katika kiwanda
cha kuchakata gesi kilichopo Madimba, mkoani Mtwara.
|
No comments:
Post a Comment