YALIYOJILI KATIKA ZIARA YA ZITTO KABWE IGUNGA,NI PAMOJA NA KUTAJA KIPATO CHA RAIS.
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe ameendelea na ziara yako Mkoani Tabora katika jimbo la Igunga Wilayani Igunga na haya ndiyo maelezo yake Zitto Kabwe juu ya kilichojili:-
"Siku ya 9 ya Ziara ya
CHADEMA kanda ya Magharibi imetufikisha Jimbo la Igunga, Wilaya ya
Igunga.
Tumefanya mikutano 6 katika kata sita tofauti,
tumefungua matawi ya chama na kuhutubia wananchi. Pia tumepokea kero za
wananchi zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Tukiwa
Katika kata ya Choma tumeshuhudia kiwanda cha kuchambua Pamba kilicho
binafsishwa kikiwa kimetelekezwa na mwekezaji toka mwaka 1998. Ginnery
hii iliyokuwa mali ya umma na kuajiri wafanyakazi 500 kwa shifti 3 kila
siku (jumla 1500) nyakati za msimu imekufa na baadhi ya Mashine kuuzwa
kama chuma chakavu. Kijiji cha Choma kimedorora kiuchumi kutokana na
ubinafsishaji huu. Nimewaeleza wananchi kuwa nitafuatilia suala hili la
Ginnery ya Manonga, katani Choma na kuwajulisha hatua mwafaka za
kuchukua.
Nimependekeza pia kwamba iwe marufuku kuuza nje
mazao ghafi kwani tunakuwa tunauza ajira za watu wetu. Suala hili
nimekuwa nikilisema Bungeni mara kwa mara kwamba ni lazima kusafirisha
mazao yaliyoongezwa thamani kwa kupiga marufuku kuuza korosho ghafi,
Pamba ghafi, kahawa ghafi na Katani ghafi. Viwanda vya kilimo vinaongeza
ajira sana kwa wananchi na ni suluhisho endelevu kwa tatizo la ajira na
kuondoa umasikini.
Niliwapa mfano wa kiwanda kilichouzwa huko
mtwara na kugeuzwa godown la kuhifadhi korosho na godown liligeuzwa
kuwa kiwanda cha kubangua korosho! Niliwaeleza namna viongozi wa
Serikali wanavyochanganya dhana ya uhuru wa biashara (liberalisation) na
ubinafsishaji (privatisation). Dhana mbili zinazochanganya watawala
wengi wa Afrika na kujikuta wakiuza mali za umma kiholela. Unaweza kuwa
na Mashirika ya Umma yakishindana katika soko na makampuni binafsi.
Ubinafsishaji holela unatengeneza 'private monopolies' na kuathiri sana
ukuaji wa uchumi kutokana na ufanisi mdogo ie efficiency.
Nimerejea wito wangu wa kutaka sera ya hifadhi ya jamii kwa wakulima
kupitia vikundi vyao na ushirika. Nimesisitiza umuhimu wa kuweka akiba
ili kuongeza uwekezaji wa ndani na hasa uwekezaji wa miundombinu ya
kilimo. Nimeonya tabia ya wananchi kukimbilia kulipwa fidia badala ya
kutaka kushiriki katika miradi mikubwa ya kilimo. Kilimo endelevu ni
kilimo cha wakulima wadogo wanapata huduma pamoja (integrated production
schemes) badala ya wakulima wakubwa wenye kuhitaji manamba.
'outgrower's schemes' ndio mwelekeo sahihi kuwafanya wananchi wamiliki
ardhi, wawe na ushirika imara, wawe na hifadhi ya jamii na waondokane na
umasikini.
Leo (jana) nikiwa kijijini Choma na mjini Igunga
nimewaambia wananchi umuhimu uwazi wa mapato ya viongozi wa umma.
Nimewaambia kuwa mishahara ya viongozi wa umma haipaswi kuwa siri na
inapaswa kukatwa kodi. Kama nilivyoahidi niliokuwa mjini Mpanda,
nimewaambia kuwa mshahara wa Rais wa Tanzania ni Tshs 384m kwa mwaka.
Kipato hiki hakikatwi kodi na Rais hupata huduma mbalimbali bure.
Niliahidi kwamba kwa kuwa gazeti la Mwananchi lilifungiwa kwa sababu ya
kutaja mishahara ya watumishi wa Serikali, basi ni vema kuonyesha
Serikali kuwa lile sio kosa na wananchi wana haki ya kujua. Ndio maana
nikachukua hatua ya kutaja kipato cha Waziri Mkuu na Rais.
Nimemaliza awamu ya kwanza ya ziara ya kanda ya Magharibi. Nimetembelea
jumla ya kata 53 katika majimbo 10 ya uchaguzi ya mikoa ya Katavi na
Tabora. Siku si nyingi nitamalizia majimbo ya Urambo na Kaliua kisha
Mkoa wa Kigoma. Nimefarijika sana na mwitikio wa wananchi wanaotaka
mabadiliko. Wazee kwa Vijana, kina mama kwa kina baba, wanataka
mabadiliko.
Nimesononeshwa na kiwango cha umasikini wa
wananchi na huduma mbovu za kijamii kama Maji, Elimu na Afya.
Nimeumizwa sana na unyonyaji mkubwa dhidi ya wakulima wa Pamba na
Tumbaku.
Nimekasirishwa sana na ufisadi mkubwa wa fedha za umma
kupitia mbolea ya ruzuku.
Nina Hofu kubwa ya wanasiasa wengi
kutojua changamoto hizi za wananchi lakini wakitaka kupewa dhamana.
Nina Hofu na wanasiasa 'manipulative' lakini nina matumaini kuwa
viongozi 'inspirational' watasimama kidete kushika usukani wa jahazi
letu na kulifikisha salama. Tanzania ina kila sababu ya kuendelea,
hatuna cha kupoteza isipokuwa minyororo ya umasikini.
Chukua
hatua!"
Chanzo: Zitto SocialMedia a/c.
No comments:
Post a Comment