Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mh.Celina Kombani |
Ahadi hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani kuwa ajira hizo
zinalenga kupunguza tatizo sugu la watumishi wa kada hiyo ambao wamekuwa
wakilalamikiwa.
Akijibu swali la nyongeza jana lililoulizwa na
Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), Kombani alisema kuwa katika
kipindi cha mwaka huu Serikali inatarajia kutoa ajira kwa waganga 5,000.
“Mwaka huu pekee tunaanza na waganga 5,000 ambao
tayari tumeshapewa kibali cha kuajiri na kipaumbele kikubwa kitaelekezwa
katika zahanaiti za vijijni lakini mwaka tutaajiri waganga 11,000,
wengi wao kwenda vijijini badala ya kuwalundika mijini,” alisisitiza
Kombani.
Awali, katika swali la msingi, Mendrad Kigola
(Mufindi Kusini-CCM) alitaka kujua ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa
vituo vya afya ambavyo wananchi wamejitolea na kufikia hatua nzuri
pamoja na kupelekea waganga.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri alijibu swali hilo akisema kuwa
miradi mingi ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati kwa sehemu kubwa
huibuliwa na wananchi, hivyo gharama za utekelezaji wa miradi hiyo
hutoka kwa wananchi pia.
Mwanri alisema ujenzi wa vituo vya afya vya
Mtwango, Mninga, Mgololo na Bumilayinga katika Jimbo la Mufindi, ni
miradi ambayo iliibuliwa na wananchi wenyewe na kuwa inatekelezwa na
wananchi wenyewe.
Hata hivyo, alisema kuwa Serikali itawaunga mkono
wananchi hao kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa kadri fedha
zinatakavyopatikana.
Hakuna shaka kwamba mpango kama huo utasaidia kupunguza tatizo la ajira ambalo linaonekana kusumbua Watanzania wengi.
Hali kadhalika kuajiriwa kwa watu hao wapatao
16,000 kutasaidia kuimarisha sekta hii muhimu ambayo inaonekana
kuendelea kusuasua nchini hasa maeneo ya vijijini.Chanzo,Mwananchi.