Ndugu
Wananchi,
Serikali
ya Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye
dhamana ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika utakaofanyika tarehe 18 – 21 Februari, 2020, Zanzibar. Mgeni
Rasmi, atakayefungua
mkutano huo ni Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe Dk. Ally Mohamed Shein.
Itakumbukwa
kuwa Tanzania ilichukua rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa jumuiya kuanzia mwezi
Agosti, 2019 kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi mwezi Agosti, 2020. Hatua hii inatokana na utaratibu wa kawaida
wa mzunguko wa kushika nafasi hiyo kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa
jumuiya hiyo.
Mkutano huu unafanyika kwa mara ya kwanza visiwani
Zanzibar tangu Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akabidhiwe uenyekiti wa jumuiya. Kufanyika kwa mkutano huu
ni fursa kubwa kwa wananchi wa Tanzania kwani utasaidia kukuza biashara na
utalii katika nchi yetu hasa visiwa vya Zanzibar na kuendelea kujitangaza
kimataifa.
Ndugu
Wananchi,
Kamati
ya Mawaziri wenye dhamana ya menejimenti ya Maafa imeanzishwa kwa lengo la kulishauri Baraza la
Mawaziri wa nchi za jumuiya ya SADC kuhusu masuala ya upunguzaji wa madhara ya
maafa kikanda. Lengo mahususi pia ni, kuwa jukwaa la kubadilishana taarifa na uzoefu
wa kiutendaji miongoni mwa nchi wanachama ili kutekeleza kwa ufanisi shughuli za
usimamizi wa maafa.
Ndugu
Wananchi,
Mkutano
huu unakuja kipindi ambacho nchi nyingi wanachama katika ukanda huu zimekuwa
zikiathiriwa na majanga ya asili mara kwa mara na kusababisha madhara makubwa. Sote
tunakumbuka ukame wa mwaka 2016 ambao uliathiri
takribani watu milioni 40 katika ukanda huu na kusababisha ukosefu wa chakula.
Idadi hii iliongezeka hadi watu milioni 41.6 katika nchi 13 Wanachama kipindi
cha msimu wa 2018/2019.
Ndugu
Wananchi,
Baadhi
ya nchi wanachama ikiwemo; (Komoro, Malawi, Msumbiji na Zimbabwe) kwa mwaka
2019 zilipata mafuriko yaliyosababishwa na Vimbunga Idai na
Kenneth. Kutokana madhara ya mafuriko hayo, Gharama za
misaada kukabilia na madhara zilikadiriwa kuwa dola milioni 323, wakati gharama
za kurejesha hali zilikadiriwa kuwa dola bilioni 10.
Ili
kuweza kupunguza gharama kubwa katika urejesahi wa hali ndio maana katika
mkutano wa SADC kujadiliana namna ya kuwekeza katika punguza madhara ya maafa,
kwa kuwa Gharama za usimamizi wa maafa kama ya ukamae na mafuriko huzilazimu
Nchi Wanachama kuelekeza rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za za
maendeleo na badala yake kuelekezwa katika shughuli kurejesha hali.
Sote
tunakumbuka, matukio ya Vimbunga vya Idai na Keneth, katika nchi za Msumbiji,
Malawi na Zimbabwe, zilizoathirika
zaidi. Kutokana na madhara ya Vimbunga
hivyo, Nchi yetu ilishiriki
katika hatua za kurejesha hali, kwa
kutoa misaada ya kibinadamu: ikiwemo tani 24
za dawa za binadamu na mahindi tani 200 kwa nchi hizi 3 (Msumbiji, Malawi na Zimbabwe).
Ndugu Wananchi,
Kwa
uzoefu wa aina ya majanga ambayo hutokea katika nchi za SADC, yanadhihirisha umuhimu
wa ushirikiano wa kikanda ulio thabiti katika kukabiliana nayo. Majanga haya
kwa kiasi kikubwa yanatokana na mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa, Pia yamekuwa yakitokea magonjwa ya milipuko ya wanyama
na mazao, katika ukanda huu ambao asilimia kubwa ya wananchi wake hutegemea
sana shughuli za kilimo kwa ustawi wa uchumi.
Hali
hii imekuwa ikichangia kudumaza ukuaji wa uchumi wa kikanda, hivyo
hatuna budi kuchukua hatua kwa pamoja za kupunguza madhara, kuimarisha utayari
wa kikanda na uwezo wa kukabiliana na maafa.
Aidha,
katika kuchukua hatua za kuimarisha ustahimilivu wa kikanda dhidi ya maafa, Sekretarieti
ya Jumuiya kwa kushirikiana na nchi wanachama imekuwa ikifanya juhudi
mbalimbali za kuimarisha ustahimilivu kwa kuandaa Mpango wa Dharura wa Kujiandaa
na Kukabiliana na Maafa, kushirikiana kuandaa
taarifa za utabiri wa msimu na kutoa tahadhari ya awali kuhusu hatari
zitokanazo hali ya hewa pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalam wa nchi wanachama
katika fani mbalimbali ikiwemo tathmini, utafutaji na uokoaji.
Aidha,
baadhi ya nchi wanachama ikiwemo Tanzania zimefaidika kwa kupata vifaa na
mifumo ya kufuatilia majanga ya mafuriko, ukame na moto wa misituni kwa ajili
ya kutoa tahadhari ya awali.
Ndugu Wananchi,
Ili
kwenda sambamba na juhudi za kikanda na kimataifa, serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, itaendelea kuimarisha uwezo wake wa usimamizi
wa maafa katika nyanja zote. Tayari serikali ya awamu ya Tano imetunga Sheria
ya Usimamizi wa Maafa ya Kitaifa Na. 7 ya 2015 na kanuni zake, Tunao Wasifu wa Janga
la Mafuriko na Ukame wa Kitaifa na Mkakati wa Taifa Kupunguza Madhara ya Maafa;
Serikali
imefanikiwa kuandaa Mpango wa Dhamira ya Taifa wa Utekelezaji wa Makubaliano ya
Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi, pia Mfumo wa Taifa wa Ufuatiliaji na Taarifa za
Gesi Joto umeandaliwa pamoja na Mipango
ya Kukabiliana na Dharura za afya ya binadamu, mifugo na wanyama pia na kuandaa
Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao baada ya Kuvuna.
Lengo
kubwa la serikali ni kuhakikisha kila sekta inazingatia hatua za upunguzaji wa
madhara ya maafa katika mipango ya maendeleo na uandaaji wa bajeti ili
kupunguza madhara kwa jamii na hasara za kiuchumi.
Ndugu Wananchi,
Mkutano
wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Menejimenti ya Maafa kwa Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika utakaofanyika mwezi
Februari, 2020 visiwani Zanzibar unakusudia kuchochea juhudi zilizopo katika kupunguza
madhara ya maafa kwa kuteleleza yafuatayo:
i.
Kujadili na kupitisha Mkakati
wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa Kikanda 2016 – 2030;
ii.
Kujadili na kuridhia Mfumo Mkakati
wa Ustahimilivu wa Kikanda 2020 – 2025;
iii.
Kupitia maombi ya nchi
wanachama kuunga mkono Sekretarieti ya Jumuiya kupata idhini ya matumizi ya
Mfuko wa Fedha za Ufadhili wa Mabadiliko ya Tabianchi.
iv.
Kupokea taarifa za maendeleo
juu ya utekelezaji wa Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mpango Kazi;
v.
Kupokea taarifa ya hatua za
utekelezaji wa maazimio mbalimbali ikiwemo kuanzisha Mfuko wa Kujiandaa na
Kukabiliana na Maafa wa Kikanda; kuanzisha Kituo cha Kikanda cha Operesheni ya
Maafa; Mpango wa Mazoezi ya Nadharia ya Kukabiliana na Dharura; pendekezo la
Mfumo wa Ushirikiano wa Rasilimali ikiwemo wataalam, fedha na vifaa wakati wa
dharura; na Utafiti wa Njia Mbadala za Ufadhili wa Majanga katika huduma za
kibinadamu na urejeshaji wa miundombinu kutokana na majanga ya asili.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Uratibu, Bunge, Uwekezaji, Ajira,
Vijana na Wenye Walemavu
No comments:
Post a Comment