1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika bajeti
ya wizara hii mwaka 2012/13, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na
CHADEMA ilibaini mapungufu mengi ya kiutendaji na kiuwajibikaji katika wizara
hii, na hivyo kuitaka Serikali kufanya
mambo yafuatayo ili kuboresha utendaji na ufanisi:
1. Kuziwezesha
balozi zetu nje kwa kuzitengea fedha za kutosha
ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi
2. Kutoa
idadi ya majengo ya balozi zetu nje (nyumba za mabalozi, nyumba za maafisa wa balozi
na ofisi za balozi) kwa mchanganuo wa idadi ya nyumba katika nchi na kama
nyumba hizo zina hati miliki au la.
3. Kutoa
taarifa ya namna kila ubalozi ulivyotekeleza sera ya Diplomasia ya uchumi kwa
kuzingatia kwamba balozi nyingi ziko hoi kifedha kiasi cha kwamba waambata wa
kiuchumi wanakosa fedha za kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa ajili
ya upelelezi wa masuala ya kiuchumi.
4. Kulikarabati
jengo la ubalozi wa Tanzania huko Msumbiji lililokuwa limechakaa kwa
kutofanyiwa ukarabati tangu 1975 ingawa jengo hilo tulipewa bure na Serikali ya
Msumbiji chini ya FRELIMO.
5. Kujenga
kitega uchumi katika kiwanja cha
Tanzania kilichopo Dubai na kukiendeleza kiwanja namba 19 tulichopewa bure na Serikali ya Uingereza
kilichopo Uingereza (Central London) ambavyo vimekuwa maficho ya wezi kwa
kutoendelezwa kwa muda mrefu na kusababisha Serikali za nchi hizo kutaka
kutaifisha viwanja hivyo.
6. Kufanya
uchunguzi kuhusu tuhuma za balozi zetu nchini China, na Uingereza kutoa hati za
kusafiria kwa mataifa mengine hasa ya Afrika Magharibi ili kubaini ukweli na
kuliondolea taifa aibu kutokana na tuhuma hizi.
7. Kukarabati
jengo la ubalozi wetu nchini China ambalo lilikuwa na nyufa na kuvuja nyakati
za mvua, na kununua samani na vifaa vya
ofisi kama mashine za nukushi na za kurudufu ambazo zilikuwa hazipo,
8. Kununua
magari mapya ya ofisi ya ubalozi wetu nchini China kwa kuwa magari matatu yaliyokuwepoyalikuwa
yameshapitiliza muda wa miaka 10 ambao kwa mujibu wa sheria za China hayapaswi
kutumika tena,
9. Kupeleka
mwambata wa kiuchumi (economic attaché)
nchini China ili kufuatilia fursa mbalimbali za kiuchumi katika
kutekeleza diplomasia ya uchumi kutokana na mahusiano makubwa ya
kibiashara kati ya nchi yetu na China
10. Kuwawekea
zuio wahusika wa kashfa ya rada kuwa viongozi wa shughuli za kiserekali ili
walau kuonesha uwajibikaji wa kimaadili (moral accountability) baada ya
kushindwa kuwawajibisha kisheria, ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa
jamii kwamba dola imetekwa na mafisadi.
11. Kuchunguza
na kuwachukulia hatua watanzania (wafanyabiashara na wanasiasa) waliotorosha
kiasi kikubwa cha fedha za nchi yetu (zaidi ya shilingi bilioni 315) na
kuzificha katika mabenki ya uswisi
12. Kutoa
mchanganuo wa jinsi fedha za rushwa ya rada (chenji ya rada) zilivyotumika
13. Kueleza
bayana faida za kiuchumi tunazopata kama taifa kwa kushirikiana na jumuiya
mbalimbali za kimataifa ili kuthibitisha kwamba mashirikiano hayo hayatumiki
kupora rasilimali za nchi yetu kwa hila ya “uwekezaji”
Mheshimiwa Spika,
kabla sijajielekeza kwenye mambo mahsusi kwa kipindi hiki cha bajeti ya
2013/2014, napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kuitaka Serikali kutoa majibu mbele ya Bunge
hili tukufu, kwamba imetekeleza kwa kiwango gani masuala yaliyoorodheshwa hapo
juu, tuliyoitaka iyatekeleze (moja baada ya jingine) kwa mwaka wa fedha
unaomalizika wa 2012/2013?