Maafisa wakuu wa ujasusi wametakiwa kufika mbele ya
kamati ya ulinzi ya bunge ili kuhojiwa kuhusu mashambulizi ya kigaidi
dhidi ya jumba la Westgate mjini Nairobi.
Taarifa kwenye vyombo vya habari nchini humo
zinaonyesha kuwa hali ya kulaumiana imeanza kuibuka huku mashirika ya
usalama yakinyosheana kidole.
Watu 67 waliuawa kwenye shambulizi
hilo huku zaidi ya miamoja sabini na tano wakipata majeraha mabaya.
Shirika la Red Cross nalo linasema kuwa watu 61 wangali hawajulikani
waliko.
Wataalamu wa uchunguzi wa mauaji wangali
wanafanya uchunguzi wao wakitafuta miili na dalili za kilichosababisha
shambulizi hilo.
Kamati ya bunge inataka maafisa wanaohusika na
maswala ya usalama waweze kuwajibishwa.
Kundi la kigaidi la nchini Somalia, al-Shabab
limedai kufanya mashambulizi hayo yaliyodumu siku nne kama hatua ya
kulipiza kisasi kwa Kenya kujihusisha nchini Somalia kijeshi.
Hii leo ni siku ya tatu ya maombolezi kwa
wathiriwa wa shambulizi hilo wakiwemo raia na wanajeshi.
Rais Uhuru Kenyatta amehudhuria mazishi ya mpwa
wake na mchumba wake mjini Nairobi ambapo aliwahutubia waumini.
Walipuuza onyo?
Hatua ya kuwataka maafisa hao wa usalama kufika
mbele ya tume ya bunge siku ya Jumatatu, inakuja kutokana na wasiwasi
miongoni mwa wakenya kuhusu kiwango cha maafisa hao kujiandaa kwa tukio
lolote la kigaidi sawa na lililotokea Westgate.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari mmoja wa maafisa
waliotakiwa kufika mbele ya kamati hiyo ni mkuu wa shirika la ujasusi
Michael Gichangi, anayesema alitoa taarifa za ujasusi kuhusu shambulizi
hilo kwa polisi.
Lakini, afisaa mmoja mkuu katika idara ya polisi
alikana kuwa taarifa hiyo ilitolewa kwa polisi.
Chanzo: BBC