ISHARA YA VIDOLE
VIWILI, PEOPLES POWER VYATAWALA
RAIS Jakaya
Kikwete jana alipata wakati mgumu, baada ya kukutana na nguvu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Mwanza katika ziara yake,
huku Waziri wake wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, naye akijikuta akizomewa
mbele yake.
Mbunge wa
Nyamagana, Ezekia Wenje, alivunja mwiko baada ya kujiunga katika msafara
huo wa raia akiwa na gari lenye alama za Movement for Change (M4C)
lililokuwa limefungwa bendera mbili za CHADEMA.
Hata hivyo
maofisa usalama walipata wakati mgumu kulizuia gari hilo lisiwepo katika
msafara huo, jambo lililozua tafrani kidogo katika uwanja wa Furahisha
ambapo Kikwete alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara.
Awali wakati
wa uzinduzi wa wodi ya wazazi iliyoko eneo la Butimba, Rais alilazimika
kumpa Wenje nafasi ya kuwasalimia wananchi baada ya Mkuu wa Mkoa,
Evarist Ndikilo, kutaka kufanya hila ya kumnyima haki hiyo kama mbunge
wa jimbo husika.
Baada ya
viongozi wote kutambulishwa bila Wenje kutajwa, wananchi walianza kupaza
sauti wakitaka mbunge wao naye atambulishwe.
Wenje baada ya
kusimama alimshukuru Rais Kikwete kwa kumpa nafasi hiyo lakini
akamwomba amvumilie kidogo atoe salamu maalumu ya wana Mwanza.
Kama kawaida
ya CHADEMA kwenye salamu yao, Wenje aliwaomba wananchi wakunje ngumi
kisha akawasalimu kwa kibwagizo cha peoples… nao wakamwitikia power!
Akiwa katika
viwanja vya Furahisha ambapo Rais Kikwete alichelewa kuanza mkutano
wake, Wenje alifika hapo na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi huku
polisi wakiwazuia bila mafanikio.
Ilipofika saa
12 jioni kabla Rais hajaingia uwanjani, wananchi hao walimtaka Wenje
awahutubie huku wakidai bendera ya taifa ishushwe kwani muda wake
ulikuwa umefika.
Kikwete
aliingia uwanjani hapo saa 12:10 akiongozana na viongozi mbalimbali wa
chama na serikali lakini wananchi hawakuonyesha kumshangilia badala yake
walikuwa wakimwonyesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na CHADEMA
wakiimba ‘peoples…power’.
Katika hatua
ya kushangaza wananchi hao walimshangilia kwa nguvu mbunge wa Ilemela,
Highness Kiwia, aliyekuwa ameongozana na Rais huku wakiwazomea Meya wa
Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, ambaye hakufika kabisa mkutanoni
hapo.
Matata
alionekana mapema wakati Rais Kikwete akisomewa taarifa ya maendeleo
makao makuu ya wilaya hiyo lakini hakufika uwanjani kabisa katika viti
vya mbele alionekana naibu wake, Swila Dede.
Baadhi ya
wananchi hao walisikika wakisema chini kwa chini kuwa Matata ni mwizi
hawataki kumsikia lakini shangwe na nderemo zikajiri pale
walipotambulishwa Wenje na Kiwia.
Rais Kikwete
akiwa wilaya ya Ilemela, wananchi wengi waliokuwa wamesimama njiani
walimwonyesha vidole viwili ikiwa ni alama CHADEMA.
Hata hivyo,
hali hiyo ilionekana kumkera kiongozi huyo wa nchi pamoja na maofisa wa
usalama, ambapo wana usalama wakiwemo polisi walionekana wakiwatisha na
kuwazuia wananchi kunyoosha vidole viwili.
Magufuli
azomewa
Waziri wa
Ujenzi, Dk. Magufuli, alikumbana na jinamizi la kuzomewa mbele ya Rais
baada ya kusimama jukwaani na kutaja jina la Matata, ambapo wananchi
wengi walimzomea kwa miluzi huku wakimnyooshea vidole viwili.
Adha Magufuli
alizomewa pia aliposema wabunge wa Ilemela na Nyamagana jijini hapa ni
wana CHADEMA lakini ndani ya roho zao ni wana CCM.
Pia aliendelea
kuzomewa aliposema kuwa iwapo Rais angehitaji kupokea kadi za CHADEMA
zilizorudishwa angepokea nyingi.
“Mheshimiwa
Rais, nampongeza Meya Matata (akazomewa), lakini pia wabunge wa Ilemela
na Nyamagana wanachapa kazi vizuri, nje CHADEMA lakini ndani wao CCM
(akazomewa).”
Akizungumza
katika mkutano huo, Rais Kikwete alimpongeza mbunge wa Nyamagana kwa
uchapakazi mzuri hasa kusimamia sekta ya elimu na kwamba wabunge wa
namna hiyo wanastahili kuigwa.
Hata hivyo,
alisema serikali yake imejipanga vizuri kuhakikisha usafiri wa reli,
ndege, majini na barabara za lami vinaboreshwa maradufu kwa ajili ya
maendeleo ya wananchi.
“Serikali
yangu imeweka nguvu kubwa katika kuboresha sekta ya uchukuzi, ujenzi na
nyinginezo. Hii ni kutaka kuwaletea wananchi wetu maendeleo ya kisekta,”
alisema.
Baadhi ya
mawaziri walioongozana na Rais mbali na Magufuli ni Naibu Waziri, Ofisi
ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga, Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe,
Naibu Waziri wa Ujenzi na Dk. Charles Tizeba.