Mheshimiwa Spika, dira
ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha kuwa raslimali za
mifugo na uvuvi zinaendelezwa na kutunzwa katika mazingira endelevu kwa ajili
ya ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi. Aidha dira inalenga kuhamasisha ufugaji wa
kisasa na uvuvi endelevu ili kujenga uchumi endelevu kwa jamii nzima ya
wafugaji na wavuvi na taifa kwa jumla.
Mheshimiwa Spika, Licha
ya ukweli kwamba wafugaji na wavuvi wana mchango mkubwa katika uchumi wetu,
Serikali hii ya CCM imeshindwa kuwapatia maeneo maalum kwa ajili ya malisho kwa
maendeleo ya mifugo yao. Wafugaji wamekuwa wakihamishwa na au wakifukuzwa
kutoka eneo moja la nchi hadi eneo lingine kama vile hawana haki ya kufanya
shughuli za kiuchumi kama ufugaji katika nchi yao. Ni aibu kwa Serikali kushindwa kuwapatia wafugaji mahitaji
muhimu ambayo yangepelekea ufugaji wao kuwa wa kisasa, kibiashara na endelevu
kama ilivyobainisha katika dira ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, haioni sababu ya
Serikali
kuwapatia wafugaji maeneo ya kufugia kwa
kuwa wafugaji wangeweza kuingia ubia na mashamba
makubwa ya mifugo ambayo yalikuwa yanamilikiwa na Ranchi za Taifa,
lakini kutokana
na ubinafsi na ufisadi uliofichwa kwenye kivuli cha cha sera ya
ubinafsishaji, Serikali ya CCM imesimamia zoezi la viongozi wa
serikali na Chama cha Mapinduzi
wakigawiana ranchi hizo na kuwaacha wafugaji wakifukuzwa ovyo na kupewa
jina la
wachungaji.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa wavuvi hali ni hiyo hiyo, kwani mapato mengi ya Serikali yanayokusanywa kutoka katika sekta ya uvuvi
yanatokana na wavuvi wadogo ambao mara zote wao ndio waathirika wa mfumo
kandamizi wa Serikali. Zana za uvuvi
zinapokamatwa, wao ndio wanapata hasara, lakini wauzaji wa zana hizo za
uvuvi wala hawaulizwi na wala hakuna
hatua zinazochukuliwa dhidi yao.
Mheshimiwa
Spika, changamoto kubwa inayozikabili sekta hizi za ufugaji na uvuvi ni kwamba
sekta zote mbili hazina bima dhidi ya majanga ambayo yanaweza kutokea. Katika mazingira kama haya, dhana ya kuwa sekta
za kisasa, kibiashara na endelevu inakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mwaka wa fedha
2012/2013 liainisha mapungufu makubwa katika ya kiutendaji na kiuwajibikaji kwa
wizara hii na kuitaka Serikali kufanya mambo yafuatayo:
1.
Kuwajibika kwa uzembe wa kuitelekeza meli ya
uvuvi ya Tawariq iliyokamatwa ikifanya uvuvi haramu katika ukanda wa bahari ya
hindi hadi meli hiyo kuharibika kabisa na kuanza kuzama bila faida yoyote?
2.
Kuchukua hatua dhidi ya mwekazaji wa Kagera
Sugar kwa kushindwa kuendeleza shamba la ukubwa wa hekta 45,000 (sawa na ekari
112,500) kinyume na mkataba.
3.
Kueleza sababu za kuwapa mashamba makubwa
wawekezaji wa kigeni na kuwanyanyapaa wafugaji wa asili kinyume cha sheria.
4.
Kutatua migogoro ya ardhi baina ya wakulima na
wafugaji ambayo mara kadhaa imesababisha uvunjifu wa amani na umwagaji damu
miongoni mwa wananchi.
5.
Kujenga viwanda vya kusindika nyama katika
mikoa ya wafugaji ili kuongeza thamani ya bidhaa ya nyama na hivyo kukuza
uchumi.
6.
Kuweka wazi kiasi cha fedha kinachopatika kama
mrahaba kutokana na uvuvi katika bahari kuu, pamoja na fedha za leseni kwa meli
zinazofanya uvuvi katika ukanda wa bahari kuu.